Na Maggid Mjengwa,
NIMEPATA kusimulia kisa cha kijana aliyehangaika sana kuusaka ukweli. Katika pitapita zake akaliona duka. Kibao kimeandikwa dukani; “Hapa tunauza ukweli”.
Dukani hapo ukweli unauzwa kwa kilo. Bei ya robo kilo ya ukweli imeandikwa, vivyo hivyo, bei ya nusu kilo ya ukweli. Lakini, mwenye duka hakuandika bei ya ukweli mzima, kwa maana ya kilo nzima ya ukweli.
Kijana yule akauliza; “Mie nataka ukweli kilo nzima, mbona hujaandika bei?”
“Alaa, unataka kilo nzima ya ukweli?” aliuliza mwenye duka. “Naam” Akajibu kijana yule.
“Basi, zunguka uje ndani nikuambie bei yake”.
Alipoingia ndani dukani, kijana yule akaambiwa; “Kijana, hatukuandika bei, maana, gharama ya ukweli mzima ni uhai wako. Je, uko tayari kulipa?”
Kijana yule akatimua mbio. Nyuma aliacha vumbi. Hakuwa tayari kulipa gharama ya ukweli mzima.
Yumkini ukweli utakaousema mwanadamu waweza usiwafurahishe wachache, walakini, ukawa wenye kuleta tija, furaha na matumaini kwa walio wengi.
Mimi nitasena hapa ukweli wangu, kuwa Baraza jipya la mawaziri ni mabadiliko ya sura ya Baraza lakini si mabadiliko ya mfumo uliosababisha udhaifu wa kiutendaji ikiwamo ‘madudu’ yale tuliyoyaona bungeni hivi karibuni. Na kauli za baadhi ya mawaziri zinathibitisha hilo; wengi wameahidi kuanzia na yanayotokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG).
Hakika, tatizo letu kubwa ni la kimfumo. Unaanzia na tunavyompata Rais wa nchi, unakuja na tunavyowapata wabunge wetu, unaendelea na mawaziri wetu wanavyopatikana na hata baadaye watendaji wetu.
Katika nchi hii Rais ana wakati mgumu sana. Maana, mfumo unamtaka awachague mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge wa chama chake. Si ajabu juzi hapa Rais amewateua wabunge wapya kutoka kwenye nafasi zake kumi na kuwafanya kuwa mawaziri hata kabla ya kuapishwa bungeni. Ilikuwa dhahiri, kuwa Rais aliwaona mawaziri wake wa kumsaidia miongoni mwa majina yale mapya ya wabunge aliowateua.
Kwa mantiki hiyo basi, mfumo ulio nafuu kwetu ni kumpa Rais uwezo wa kuchagua mawaziri nje ya Bunge. Kwamba Katiba ijayo iweke wazi kuwa mawaziri wasiwe wabunge kwa wakati mmoja. Kama Rais ataamua kumteua mbunge kuwa waziri, basi, mbunge huyo ajiuzulu kiti chake cha ubunge. Maana, mbunge ni mwakilishi wa wananchi ambaye moja ya majukumu yake bungeni ni kuisimamia Serikali. Mwanadamu huwezi kupanda farasi wawili kwa wakati mmoja.
Tuna tatizo jingine hatuliweki wazi lakini lipo na linakomaa; uteuzi wa Baraza la Mawaziri katika mfumo wetu wa sasa unaangalia pia jiografia ya nchi yetu. Inaangaliwa kama katika Baraza jipya Mbeya wamepata mawaziri? Dodoma? Mwanza….
Na tukitoka hapo tunakuja ni wangapi kwa kila mkoa? Ni mfumo mbaya unaozoeleka. Maana, mitaani watu wa Singida wanaweza kuhoji? Mbona sisi tumesahaulika kwenye Baraza jipya? Kana kwamba ni Baraza la mikoa wakati ni la taifa.
Na hii inatokana na tabia iliyojengeka ya baadhi ya mawaziri kuonyesha wazi wazi kuwa wanatumia uwaziri wao kuvutia maendeleo kwao- kwenye majimbo yao badala ya kuangalia nchi nzima. Waziri anakuwa waziri wa jimbo badala ya nchi nzima.
Ni katika mazingira haya, hata kama mbunge wa chama kilichotoa rais ni mgonjwa, lakini anakubalika sana kwenye jimbo, wilaya na hata kanda anayotoka, Rais anaweza kushauriwa ampe chochote kile ilimradi cheo cha ‘Mheshimiwa Waziri’ kisifutike. Maana, kikifutika hicho, basi, kuna kura nyingi za chama zitakazofutika kwenye uchaguzi ujao!
Ukabila na ukanda umeanza kunukia badala ya utaifa. Tumesahau kuwa miaka hiyo nchi hii imepata kuwa na wabunge na hata mawaziri wazungu na wahindi. Ni akina Derek Brysson, Leader Sterling, Al Noor Kassam, Ameir Jamal na wengine. Hawa walionekana kwanza kama Watanzania wazalendo.
Tatizo jingine la mfumo tulio nao sasa ni Rais wa nchi kushauriwa kufanya teuzi zinazoendana na mikakati ya siasa za vyama. Kwa mantiki hii, hata CUF au CHADEMA wakiingia madarakani kesho, na kwa mfumo huu huu, nao, kwa kiasi kikubwa, watafanya hivi hivi. Ndio maana ya kusisitiza, kuwa, tulilo nalo sasa ni tatizo la kimfumo ambalo ndiyo chimbuko la utendaji mbovu wa kuanzia mawaziri na walio chini yao. Ni mfumo unaomfanya waziri, awajibike zaidi kwa chama chake badala ya taifa kwa ujumla wake.
Na ni katika mfumo huu ambapo chama kinabeba jukumu la kumlinda waziri hata katika maovu. Ni kwa tafsiri hii, mathalan, wabunge wa CCM wakimwangusha Waziri aliyefanya maovu, huamini kuwa wamekiangusha chama chao na Rais, ambaye ni mwenyekiti wao na ndiye aliyemteua waziri husika. Hilo husababisha kujengeka kwa hofu miongoni mwa wabunge wa chama tawala katika kumjadili waziri na hata kumwajibisha.
Na hofu hiyo huimarika zaidi kutokana na mfumo wa chama tawala ambao yumkini Waziri anayejadiliwa aweza pia kuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama. Ni Kamati ambayo hupitisha uamuzi muhimu kwa chama ikiwamo kupitisha majina ya wagombea nafasi mbalimbali ndani ya chama ikiwamo ubunge. Kuna wabunge wenye kuhofia kuukata mkono unaowalisha. Hatima yake? Ni madudu kama yale tuliyoyaona kwenye ripoti ya CAG.
Na kwa vile mfumo uliosababisha madudu yale ungalipo, basi, yumkini madudu yale yatatafuta namna nyingine ya kuishi, badala ya kutambaa sakafuni, yataanza kujichimbia zaidi. Dawa mujarab ya madudu yale tuliyoyaona kwenye ripoti ya CAG ipikwe na kuchanganywa vilivyo kwenye Katiba yetu mpya tunayokwenda kuitengeneza.
Na tatizo la mfumo tulionao tutaliona pia kwenye teuzi za wakuu wa wilaya ndani ya mwaka huu. Maana, katika mfumo wetu huu, wakuu wa wilaya ni makada wa chama tawala.
Wakuu wa wilaya katika mfumo ulio nafuu wangepaswa wabaki ‘kiserikali’ zaidi kuliko ‘kichama’. Kwenye maeneo yao wangesimamia masuala ya maendeleo bila kutanguliza maslahi ya chama ikiwamo kulinda maovu kwa kukiogopa chama kilicho madarakani.
Ni makosa, katika dunia ya sasa, pale mfumo unapofikiria kumpeleka DC wilayani aende akadhoofishe upinzani badala ya kusimamia maendeleo na kuhakikisha wadau wote wilayani, bila kujali tofauti zao za itikadi, wanashirikishwa katika kuinua uchumi wa wilaya, na hivyo kuiletea wilaya na wananchi maendeleo. Kubadilisha mfumo inawezekana.

Na Maggid Mjengwa
Iringa Tanzania
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)