Mmoja wa wakazi wa Kata ya Maneromango
Na Joachim Mushi,
Thehabari.com-Kisarawe
UKIWA wewe ni
mkazi wa Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani huenda siku zote
utakuwa ukiomba isitokee umeibiwa au kufanyiwa kitendo chochote cha uhalifu
kwani utagharamika na kama hauna uwezo kifedha unaweza kumsame mwizi wako bila
kupenda.
Hii ni kutokana
na utaratibu uliopo eneo hilo ambapo mtu anayeibiwa hulazimika kumgharamia
mtuhumiwa pamoja na mgambo fedha za nauli kwenda mjini Kisarawe ili
akafunguliwe mashtaka. Mwananchi aliyeibiwa atalazimika kumlipa pia posho
mgambo na nauli ya kurudi Maneromango baada ya kumkabidhi mtuhumiwa Polisi.
Kwa mujibu wa
taarifa kutoka kwa baadhi ya wakazi wa Maneromango mtu aliyeibiwa au kufanyiwa
uhalifu hulazimika kutoa kiasi cha sh. 35,000 fedha ambayo hugharamia nauli ya
mtuhumiwa kwenda Kisarawe, nauli ya mgambo anayeambatana na mtuhumiwa kwenda na
kurudi pamoja na posho kwa mgambo.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti juzi kutoka Maneromango, Rehema Zomboko mkazi wa Kijiji cha
Boga Kata ya Maneromango alisema utaratibu huo umewafanya wanakijiji wengi
kutotoa taarifa za wizi kwa kile kuogopa gharama za kumsafirisha mtuhumiwa
wako.
Akizungumza mkazi
mwingine wa Kijiji cha Mengwa, Ramadhan Kingungu alisema utaratibu huo umekuwa
kikwazo cha kuambana na vitendo vya kihalifu, kwani wengi wapo radhi kukubali
kuibiwa na kumalizana kwa mazungumzo na mtuhumiwa kuliko kutoa taarifa kwa
uongozi wa kijiji.
“Katika hali ya
kawaida unaweza kuangalia ndugu mwandishi hivi mtu anaweza kukuibia kuku alafu
ugharamie sh. 35,000 ili akashtakiwe mjini Kisarawe...? Wengi wameshindwa
wanaotoa gharama hizo ni watu wenye uwezo kifedha hapa kijijini,” alisema
Kingungu.
Naye Halima
Mwinyimkuu wa Kijiji cha Maneromango Kaskazini alisema wapo baadhi ya watu
ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya kihalifu mara kadhaa (hasa wizi wa kuku)
lakini wamekuwa hawachukuliwi hatua zozote kwa wahusika kuhofia gharama za
mashtaka.
Aidha akizungumzia
utaratibu huo Ofisa Mtendaji Kata ya Maneromango, Nicolaus Lemma alisema ni
kweli wananchi hulazimika kuchangia kiasi cha fedha pale wanapokuwa na
mtuhumiwa fedha ambazo hutumika nauli kwa mtuhumiwa, mgambo pamoja na
mlalamikaji.
“Ni kweli
wanalazimika kuchangia lakini si sh. 35,000 kama wanavyosema wao, kiasi cha
fedha mara nyingi huweza kufikia sh. 20,000 hivi...hii ni kutokana kwamba
hatuna kituo cha polisi katika kata yetu ya Maneromango, lakini juhudi
zinafanywa ili tuweze kuwa na kituo,” alisema Lemma.
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com
(www.thehabari.com) kwa kushirikiana na
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)