Ndugu zangu,
Msanii Remmy Ongala alipata kuimba;
" Ukiwa na roho mbaya,kweli tutakuogopa,
Ukiwa na roho mbaya, huko unakokwenda nako ni kubaya!"
Siku zote, mwanadamu usijaribu kufanikiwa maishani kwa kuwa mbaya kwa wengine. Ndio, kuna waliofanikiwa maishani kwa kuwa wabaya kwa wengine.
Siku
zote, mwanadamu aliyefanikiwa kwa kuwatendea maovu wanadamu wenzake
hawezi kuwa ni mtu mwenye furaha na amani maishani. Ataandamwa na
jinamizi la maovu yake mpaka atakapoingia kaburini.
Je, mwanadamu huyo afanye nini?
Ajitazame
mwenyewe. Aache kuendelea kuwatendea mabaya wengine katika kiu yake ya
kukifikia ’ kilele cha mafanikio’- kama kweli kipo humu duniani! Hivyo
basi, mwanadamu huyo atakuwa amejitambua. Na kwa vile naye ni mwanadamu,
basi, hakuna mwanadamu asiyetenda makosa.
Dhambi
kwa mwanadamu huyo itakuwa ni hulka yake ya kuendelea kuwakanyaga
wanadamu wenzake katika juhudi za kuyafikia mafanikio yake. Misaada kwa
yatima na masikini haitasaidia kuzifuta dhambi zake, maana, amezifanya
na bado anaendelea kuzifanya.
Je, kwanini mwanadamu anakuwa ni mtenda maovu?
” Kwenda huko, utakufa kwa roho yako mbaya!”. Hiki kilikuwa ni kibwagizo katika moja ya matangazo ya kijamii redioni miaka ya karibuni.
Nilipata kumwuliza msanii Mrisho Mpoto swali la kifalsafa; ”Je, binadamu tunakufa kwa roho mbaya au roho chafu?”
Mpoto
ananijibu: ” Kaka Maggid, naiona mantiki ya swali lako. Kama nitakunjua
viganja vyangu na kuitema roho yangu kisha nikaiangalia... lakini
fafanua kwanza fikra zako.”
Nikafafanua,
kuwa binadamu hatukuumbwa kuwa wengine wana roho mbaya na wengine
nzuri. Sote tumeumbwa na roho nzuri isipokuwa mazingira ndio
yanayotufanya wengine tukawa na roho chafu na wengine roho safi. Ndio,
roho nzuri tulizoumbwa nazo zinachafuka. Tunakuwa ni binadamu wenye roho
chafu. Na hakika, Watanzania wengi tunakufa kutokana na roho chafu,
zetu wenyewe au za wenzetu.
” Mh!” Anaguna Mrisho Mpoto. Ananiacha niendelee.
Maana,
ni mtu mwenye roho chafu tu anayeweza kujaribu kuyazuia mabadiliko
yatakayomsaidia mwanadamu mwenzake atoke mahali alipo na apige hatua
itakayomsaidia maishani.
Ni
mtu mwenye roho chafu tu atakayeweza kuhujumu mradi wa kuangamiza
Malaria inayosababisha vifo vya maelfu ya watoto na watu wazima ili
apate mafanikio binafsi.
Ndio,
kuhujumu mradi wa kuzuia malaria ili apate fedha za kufanya mambo ya
fahari au hata kununua uongozi wa kisiasa au kuendelea kubaki
madarakani.
Kwa
mwanadamu, ni heri ufe kwa kupambana na anayehujumu mradi wa kuangamiza
malaria kuliko kufa kwa malaria inayotokana na mbu anayesababisha
malaria.
Naam, You do not win by being bad. Utakwama njiani. Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)