Ofisi
ya Bunge inapenda kuwatangazia wanahabari wote na wananchi kwa ujumla
kuwa Mkutano wa Saba wa Bunge utaanza tarehe10 Aprili, 2012 na
unatarajiwa kumalizika tarehe 21 Aprili, 2012. Orodha za shughuli
zinazotarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano huo ni kama ifuatavyo:
KIAPO CHA UTII KWA WABUNGE WAPYA:
Kwa
mujibu wa masharti ya Kanuni ya 24(1) ya Kanuni za Bunge, toleo la 2007
kutakuwa na Kiapo cha Utii kwa Wabunge wapya wawili. Wabunge hao ni
Mheshimiwa Cecilia Danieli Paresso (Viti Maalum CHADEMA) aliyeteuliwa
kujaza nafasi iliyoachwa wazi Kufuatia kifo cha marehemu Regia Estalatus
Mtema aliyefariki kwa ajali ya gari, na Mheshimiwa Joshua Nassari
(CHADEMA) aliyechaguliwa katika Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru
Mashariki uliofanyika tarehe 1 Aprili, 2012 kufuatia kifo cha aliyekuwa
Mbunge wa Jimbo hilo marehemu Jeremiah Solomon Sumari (CCM).
SHUGHULI ZA SERIKALI:
kwa
Mujibu wa Kanuni ya 17 (1) (d) Toleo la 2007, Serikali
ilikwishaziwasilisha kwa Katibu wa Bunge na shughuli za Serikali Bungeni
katika Mkutano Ujao na kuorodheshwa kwenye Kitabu cha Shughuli za Bunge
kama ifuatavyo:-
MISWADA YA SHERIA YA SERIKALI:
Miswada
ya Sheria ya Serikali Minne(4) ambayo ilishasomwa kwa mara ya kwanza
katika Mikutano ya Bunge iliyopita itawasilishwa Bungeni katika Mkutano
ujao wa Bunge.. Miswada inayotarajiwa kusomwa kwa Mara ya Pili na
kuendelea na hatua zake zote ni hii ifuatayo:-
(Kusomwa kwa Mara ya Pili na Hatua Zake Zote Kwa Mujibu wa Kanuni ya 86 ya Kanuni za Bunge):
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania wa Mwaka 2011 [The Tanzania Livestock Research Institute Act, 2011];
Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa
Mwaka 2012 [The Social Security Laws (Amendments) Act, 2012 (No.2) Act,
2011];
Muswada
wa Sheria ya Marekebisho wa Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2011 [The
Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 2) Act, 2011];
Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Biashara wa Mwaka
2011. [The Business Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2011].
HOJA ZA SERIKALI:
Bunge kukaa kama Kamati ya Mipango:
Kwa
Mujibu wa Kanuni ya 94, Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango ili
kutekeleza matakwa ya Ibara ya 63(3)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya Mwaka 1977, kujadili na kuishauri Serikali juu ya
mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali
katika Mwaka wa Fedha 2012/2013.
Taarifa ya Serikali ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge:
Katika
Mkutano wa Tano wa Bunge Serikali ilipokea Mapendekezo yaliyotolewa na
Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wa utaratibu wa
Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha
Bajeti Bungeni. Hivyo basi katika Mkutano huu Serikali itatoa Bungeni
Taarifa ya utekelezaji wa Maazimio hayo.
SHUGHULI NYINGINE:
MASWALI:
Maswali kwa Waziri Mkuu:
Kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 38, Waziri Mkuu anatarajiwa kuulizwa na Wabunge maswali 16 ya msingi.
(ii) Maswali ya Kawaida:
Kwa
mujibu wa Masharti ya Kanuni ya 39, Jumla ya Maswali 125 ya kawaida
yanatarajiwa kuulizwa na Wabunge na kujibiwa na Serikali katika mkutano
ujao wa Saba.
TAARIFA ZA KAMATI ZA BUNGE:
Kwa
mujibu wa Kanuni ya 114 (15), Kamati za Bunge zitawasilisha Taarifa za
kazi za Kamati kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2010/2011 na Taarifa hizo
zitajadiliwa na Bunge kwa kadri itakavyoonekana inafaa. Hivyo Taarifa
hizo zitawasilishwa mezani tarehe 10 Aprili, 2012 ili kutoa fursa kwa
Wabunge kuzipitia kabla ya kuanza kuchangia Bungeni.
UCHAGUZI WA WABUNGE WA BUNGE LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI:
Kufuatia
kufika ukomo wa kipindi cha Ujumbe wa Bunge la Jumuiya ya Afrika
Mashariki na kwa kuzingatia masharti ya Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya
Afrika Mashariki na Kanuni za Bunge, katika Mkutano wa Saba wa Bunge
kutakuwa na Uchaguzi wa Wabunge Tisa watakao iwakilisha Tanzania katika
Bunge hilo. Hivyo kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, siku ya uteuzi
itakuwa ni Jumanne tarehe 10/4/2012 saa kumi jioni na Uchaguzi
utafanyika siku ya Jumanne tarehe 17/4/2012.
HOJA BINAFSI ZA WABUNGE:
Kwa
mujibu wa Kanuni ya 54, Katibu wa Bunge amepokea makusudio mawili ya
Wabunge kutaka kuwasilishwa Hoja binafsi. Aidha, kwa mujibu wa fasili ya
(1) na (2) ya Kanuni ya 55 Wabunge hao wameshaandikiwa barua ya
kuwataka wawasilishe Taarifa za Hoja zao kwa Katibu wa Bunge. Endapo
hoja hizo zitakidhi matakwa ya Kanuni za Bunge zitatengewa muda wa
kuwasilishwa Bungeni katika Kikao kijacho cha Saba.
MAMBO MENGINE:
SEMINA ZA WABUNGE WOTE:
Ofisi
ya Bunge imepokea maombi mawili kutoka Taasisi mbili za Umma ya kufanya
Semina kwa Wabunge katika Mkutano wa Saba wa Bunge. Semina hizo ni kama
ifuatavyo:-
Semina
kwa Wabunge wote kuhusu Anuani Mpya za Makazi na Simbo za Posta pamoja
na Mabadiliko ya Teknolojia ya Utangazaji kutoka Analojia kwenda
Dijitali;
Semina kwa Wabunge wote kuhusu Sensa ya Watu na Makazi.
Imetolewa na
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge
Dar es Salaam
7 Aprili, 2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)