Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akipata maelezo
kuhusiana na hali ya uchimbaji wa mchanga katika eneo la Kwarara
Wilaya ya Magharibi Unguja, karibu na nguzo ya umeme mzito unaopokelewa
kutoka gridi ya Taifa. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Mhe.
Abdallah Mwinyi Khamis.
Eneo
linalochimbwa mchanga na kusababisha uharibifu wa mazingira huko
Kwarara Wilaya ya Magharib Unguja. Eneo hili liko karibu sana na nguzo
ya umeme mzito unaopokelewa kutoka gridi ya Taifa. (Picha, Salmin
Said-Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
----
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka
viongozi wa Shirika la Umeme, Idara ya Mazingira na Polisi kudhibiti
vitendo vya baadhi ya wananchi kuchimba mchanga maeneo yenye nguzo za
umeme mzito, ili kuepusha hatari ya kukosekana umeme au kutokea maafa.
Makamu
wa Kwanza wa Rais aliyasema hayo wakati alipotembelea eneo la Kwarara,
Wilaya ya Magharibi Unguja kujionea athari kubwa zilizosababishwa na
vitendo vya uchimbaji wa mchanga chini ya nguzo za umeme mzito
unaopokelewa kutoka kituo cha Fumba.
Alisema
iwapo vitendo hivyo havitadhibitiwa kuna hatari nguzo hizo zikaanguka
kabisa na kusababisha Zanzibar kukosa umeme kwa kipindi kirefu, lakini
pia vinaweza kusababisha maafa, iwapo nguzo ya umeme mzito itaanguka.
Makamu
wa Kwanza wa Rais alisema taasisi hizo pamoja na Wilaya ya Magharibi
hazina budi kulifanyia tathmini ya kina tatizo la uchimbaji wa mchanga
chini ya nyaya hizo, katika kipindi cha wiki mbili na baadaye kuchukua
hatua zinazofaa kukomesha tabia hiyo.
Alisema
sheria za Mazingira pamoja na kanuni za miji ziko wazi, hivyo wale
wanaothibitika kujihusisha na uchimbaji wa mchanga bila ya kufuata
sheria, wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Akitoa
maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Sheha wa Shehia ya Kwarara, Haji
Pandu Jecha alisema pamoja na uongozi wa Shehia kuwachukulia hatua
baadhi ya wananchi waliokamatwa wakichimba mchanga katika maeneo hayo,
bado vitendo hivyo vinaendelea kwa kasi.
Alisema
hivi sasa watatumia ulinzi shirikishi chini ya utaratibu wa polisi
jamii, kukomesha vitendo vya uchimbaji wa mchanga vinavyofanywa chini
ya nguzo hizo zinazosafirisha umeme kutoka Gridi ya Taifa, ambapo
wahusika huchimba mchanga huo nyakati za usiku.
Meneja
Operesheni wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Abdalla Haji Steni
alisema vitendo vya uchimbaji mchanga chini ya nguzo nyingi za umeme
vinaendelea kwa kasi kubwa, licha ya kuwa na madhara makubwa kwa nchi.
Alieleza
kwamba katika kufanikisha maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Kwanza wa
Rais, Shirika la Umeme litashirikiana na wadau wengine kufanikisha
upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuzilinda nguzo hizo zisiathiriwe.
Na
Na Hassan Hamad
Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)