Rais Jakaya Kikwete
---
Katika
mahojiano yake leo, Alhamisi, Aprili 5, 2012, na Redio One, ikiwa ni
kauli yake ya kwanza baada ya Mahakama Kuu ya Arusha kutangaza kumvua
ubunge, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Bwana Godbless Lema, amedai
kwa jazba sana kuwa hukumu ya Mheshimiwa Jaji Gabriel Rwakibalira
imetokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Ikulu.Kauli hii ya Bwana Lema ni
upuuzi. Siyo Mheshimiwa Rais Kikwete wala Ikulu imeingilia kati kesi
yake kwa namna yoyote ile, iwe ni kwa kupiga simu ama kuzungumza na
Mheshimiwa Jaji Rwakibalira.
Kwa hakika, haijapata kutokea Mheshimiwa Kikwete, tokea alipoingia
madarakani, Desemba 21, 2005, akaingilia, kwa namna yoyote ile,
mwenendo wa kesi yoyote ile katika Mahakama yoyote na ya ngazi yoyote
katika Tanzania. Na wala hakusudii kufanya hivyo wakati wote wa muda
wake uliobakia wa uongozi. Siyo kazi ya Rais kutoa hukumu ama kuelekeza
namna ya kutoa hukumu katika kesi zilizoko Mahakamani. Rais hana
madaraka wala mamlaka hayo.
Aidha, kauli ya Bwana Lema ni ukosefu mkubwa wa adabu na heshima kwa
Mahakama ambao ni Muhimili Huru usioingiliwa na Serikali ama na
Muhimili mwingine katika maamuzi yake. Bwana Lema amekuwa kiongozi kwa
muda sasa, hivyo ni lazima atambue jambo hili kubwa na muhimu katika
mfumo mzima wa utawala wa nchi yetu.Ni jambo lisilokuwa na mshiko wala
tija, na kwa kweli ni bahati mbaya, kwamba Bwana Lema anajaribu kuingiza
mambo yasiyohusika katika jambo la dhahiri kabisa kuwa ni la kisheria
ambalo msingi ni hoja na maelezo mahakamani.
Bwana Lema asitafute visingizio kwa yaliyomfika kwa sababu hakuna
mtu mwingine wa kumbebea msalaba huu. Badala ya kutafuta mchawi
asiyekuwepo, ni vyema Bwana Lema angekaa chini na kuangalia ni sababu
zipi za kisheria zilizomfanya ashindwe na kama ameridhika kuwa
hakutendewa haki akate rufani kwa mujibu wa sheria nataratibu.Tunaomba
wananchi wampuuze. Ameshindwa kesi kwa makosa yake aliyofanya hana mtu
wa kumlaumu bali ajilaumu mwenyewe
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
05 Aprili, 2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)