Baraza la Habari Tanzania:Acheni Mahakama ifanye Kazi Yake Juu Ya Kifo Cha Steven Kanumba - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Baraza la Habari Tanzania:Acheni Mahakama ifanye Kazi Yake Juu Ya Kifo Cha Steven Kanumba

Kutoka kulia ni Katibu wa MCT Kajubi Mukajanga katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili Baraza la Habari MCT  Jaji Thomas B. Mihayo na  Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili pia Mjumbe wa Bodi Rose Haji. Picha: Blasio Kachuchu
---

KAMATI ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) leo  mchana imetangaza  imesikitishwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili uliojitokeza hivi karibuni kwa baadhi ya vyombo vya Habari ambavyo wakati vikiripoti kuhusu kifo cha Msanii Steven Charles Kanumba, vimemhukumu msichana Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, kuwa amemuua msanii huyo.

Ukiukwaji huo umejitokeza hasa baada ya msichana huyo kufikishwa Mahakamani, ambapo baadhi ya magazeti yanayoheshimika katika jamii jana Alhamisi, Aprili 12, 2012 yaliandika vichwa vikubwa vilivyosomeka: Lulu Kortini kwa kumuua Kanumba na Lulu Kizimbani kwa mauaji ya Kanumba.

Kwa mujibu wa sheria na maadili ya Uandishi wa Habari mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ile ni mtuhumiwa mpaka atiwe hatiani na mahakama.

Kanuni hii ya siku nyingi katika fani ya uandishi wa habari inafahamika na waandishi na wahariri wote wanaoheshimu kazi yao.

Baraza pia limeshatoa matamko mara kadhaa kuwakumbusha wanahabari kujiepusha na uandishi wa habari au vichwa vya habari vinavyohukumu.

Baraza linafahamu fika kuwa kesi zilizoko Mahakamani ni kivutio kwa umaa kutaka kujua kinachoendelea ili kuona haki ikitendeka na pia wanahabari wana haki ya kujua na kuripoti yanayojiri huko na katika vyombo vingine vya sheria.

Lakini lazima ifahamike kuwa wakati wakitumia fursa na haki hiyo Wanahabari wanapaswa kuzingatia kanuni, miongozo na sheria zinazolinda haki za msingi zxa watuhumiwa na uhuru wa Mahakama.

Ni wazi kuwa vichwa vya habari vilivyoitajwa hapo juu vimeliingilia uhuru wa Mahakama kwa kuchapisha habari ambazo zinaonekana kushawishi au kushinikiza uamuzi wa Mahakama.

Wanahabari ni lazima watambue kuwa kuna taratibu na makubaliano ya kijamii juu ya namna gani taarifa zinavyopaswa kuripotiwa ili kutowadhuru watu wengine.

Hivyo basi , Baraza la Habari Tanzania linapenda kuwakumbusha tena wahariri kuhakikisha kuwa wanafanya kazi yao kwa kuzingatia maadili na weledi katika kuripoti mkasa huu unaogusa hisia za watu.

Imesainiwa na
Jaji Thomas B. Mihayo
Mwenyekiti,Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages