Baadhi
ya walimu waliopo katika mafunzo ya vitendo katika Kituo cha Walemavu
cha Shule ya Msingi Iliboru wakifundisha darasa la watoto wenye ulemavu
wa kusikia.
Na Joachim Mushi, -Arumeru
BAADHI
ya walimu wa wanafunzi wenye ulemavu anuai wilayani hapa wameitaka
Serikali kuacha utaratibu wa kuwataini wanafunzi wenye ulemavu katika
mitihani ya taifa kwa vigezo sawa hasa upande wa muda wa kufanya
mitihani husika.
Wamesema
hali hiyo inawanyima baadhi ya wanafunzi wenyeulemavu kujipima
kiusahihi kutokana na dosari zao na wanafunzi wa kawaida hivyo kujikuta
wengi wakifanya vibaya au kutopata daraja stahili kwenye matokeo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini hapa,
Mwalimu Mkuu wa Kituo cha Wanafunzi wenye ulemavu, Shule ya Msingi
Naurei wilayani Arumeru, Tuzie Mtenga amesema kitendo cha kuwachanganya
wanafunzi hao baadhi yao wameishia kufanya vibaya katika masomo yao hasa kwenye mitiani ya mwisho kitaifa.
“Mwanafunzi
mwenye ulemavu baada ya kumaliza mafunzo kwenye vitengo vyao tumekuwa
tukiwachanganya kwenye madarasa ya kawaida shule za msingi, wanaendelea
na baadaye wanafanya mitihani ya taifa kwa muda sawa na wengine hiki
si kipimo sahihi kwa kweli,” alisema Mtenga ambaye kituo chake
kinawalemavu wa akili na viungo.
Naye
mwalimu, Rams Mosha wa Chuo cha Mafunzo kwa Watu wenye Ulemavu Usa
River amesema wapo wanafunzi wenye ulemavu ambao kasi yao ya uandishi ni
tofauti na mwanafunzi wa kawaida na wanauelewa lakini wamekuwa
hawapati haki pale wanapotahiniwa kwa vigezo sawa hasa muda na
wanafunzi wengine.
“Walemavu
wengine wanaandika huku wakitetemeka sasa mtu kama huyu waweza kukuta
anafanya vizuri darasani lakini kwa kuwa baadaye anafanya mtihani wa
taifa kwa muda sawa na watahiniwa wa kawaida anaweza asimalize mtihani au kutofanya vizuri…hili aliangaliwi na mamlaka husika,” alisema Mosha ambaye naye ni mlemavu wa viungo.
Kwa upande wake Mwalimu Mratibu wa Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru,
Loitusho Yamat ipo haja ya wanafunzi walemavu kufuatiliwa kwa karibu
tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wameshindwa kufanya vizuri kutokana
na usimamizi afifu uliopo kielimu.
Yamat
ambaye shule yake ina jumla ya wanafunzi walemavu 60, yaani wanafunzi
viziwi na wale wenye mtindio wa ubongo alisema kwa sasa kituo hicho
kimetafuta ufadhili kwa ajili ya ujenzi wa shule ndogo ya sekondari kwa
wanafunzi wenye ulemavu ili kuwafuatilia kwa karibu baada ya masomo ya
msingi.
Habari na picha zote zimeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com kwa ushirikiano na Kituo cha Habari Kuhusu Ulemavu Tanzania (ICD)
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)