
Bi. Vick Kimaro ambaye ni mmoja wa viongozi wawakilishi wa watu wenye ulemavu wilayani na Mratibu wa vikundi vya Pambazuko Klabu

Mwalimu Mratibu wa Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru, Loitusho Yamat akionesha hesabu wanazofundishwa

Kikundi cha Wanapambazuko Klabu cha Shule ya Msingi Iliboru wilayani Arumeru, kikundi hichi hufanya kazi ya kuelimisha jami
----
Na Joachim Mushi-Arumeru
BAADHI
ya Walimu Waratibu wa Vitengo vya Wanafunzi Walemavu vilivyopo katika
shule za msingi Wilaya ya Arumeru wameiomba Serikali kuvisaidia vituo
hivyo kifedha ili viweze kutekeleza programu zake anuai kwa lengo la
kuboresha elimu kwa watu wenye ulemavu.
Wakizungumza
katika mahojiano kwa nyakati tofauti hivi karibuni na mwandishi wa
habari hizi kwenye vituo vyao, wamesema utaratibu wa wazazi kuchangia
vituo hivyo umekuwa mgumu kwani wazazi/walezi wengi wa watoto walemavu
wana uwezo mdogo kiuchumi.
Mratibu
wa Kituo cha Walemavu cha Shule ya Msingi Iliboru, Loitusho Yamat
alisema kitendo cha vituo hivyo kutokuwa na fungu maalumu hasa upande
wa huduma ya chakula shuleni kimezifanya shule nyingi kutegemea
wafadhili, watu ambao wanaweza kujiondoa muda wowote na vituo kuwa na
hali mbaya.
“Unajua
huduma ya chakula kwa wanafunzi walemavu ni muhimu zaidi, kwanza
kundi hili haliwezi kuvumilia na kuendelea na masomo kama wana
njaa…wakati mwingine wengine wanavutiwa na programu za chakula kisha
anajikuta anapata na elimu…chakula ni muhimu kwa wanafunzi wa aina
hii,” alisema Yamat.
Alisema
tangu kituo hicho kianzishwe mwaka 2001 fedha ambayo Serikali imewekeza
kihuduma haijafikia sh. 300,000; huku huduma ya chakula ikitolewa na
mfadhili mmoja raia wa Marekani tangu 2005 hadi sasa.
Aidha
Mkuu wa Kitengo cha Wanafunzi Walemavu cha Shule ya Msingi Naurei,
Tuzie Mtenga alisema mbali na changamoto za kupungukiwa na vifaa vya
kufundishia kama rangi, karatasi na vibao upande wa chakula kwa watoto
limekuwa tatizo kwa vipindi tofauti.
Bi.
Mtenga alisema chakula huwa wazazi husika wanachangia pamoja na
wengine wanaoguswa na wanafunzi hawa, lakini wakati mwingine inakuwa
ngumu kupata kutokana na wazazi wengi wa watoto wenye ulemavu kutokuwa
na uwezo kiuchumi (kipato).
“Kwa
mfano watoto wengi walemavu wengine wametelekezwa na wazazi wao kwa
bibi zao, sasa watu hawa hawana uwezo sana wa kuchangia chakula ndiyo
maana inakuwa tabu wakati mwingine kupatikana kwa huduma hiyo…sasa kama
kungelikuwa na bajeti kutoka serikalini kupitia wizara husika hali
ingelikuwa ni tofauti kidogo,” alisema.
Akizungumzia
mwamko wa jamii kuhusiana na elimu kwa watoto wenye ulemavu eneo hilo
amesema, kuna mafanikio kwani kikundi cha ‘Pambazuko Klabu’
kilichoanzishwa na shule hiyo kwa ushirikiano na Kituo cha Habari
Kuhusu Ulemavu (ICD) kinaeneza kwa kutumia sanaa juu ya umuhimu wa
elimu kwa watoto wenyeulemavu.
Habari
hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com kwa ushirikiano na Kituo
cha Habari Kuhusu Ulemavu (ICD) cha jijini Dar es Salaam.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)