Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Uongozi
wa Chuo cha elimu ya biashara (CBE) kampasi ya Dar es salaam umesema
kuwa hautasita kumchukulia hatua mwanafunzi au mfanyakazi yeyote
atakayefika chuoni hapo akiwa amevaa mavazi yasiyo ya heshima huku
ukitoa wito kwa wananchi kuunga mkono kampeni hiyo yenye manufaa katika
kujenga taifa lenye maadili mazuri.
Akizugumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Kaimu mkuu wa Chuo cha
Elimu ya Biashara Dar es salaam Bw. Athman Ally Ahmed amesema chuo hicho
kimefikia uamuzi huo kufuatia kukithiri kwa vitendo vya uvaaji wa
mavazi yasiyokuwa na staha vinavyofanywa na wanafunzi wa kike na wale
wa kiume wawapo chuoni hapo hali inayosababisha udhalilishaji wa utu wa
wanafunzi ndani na nje ya chuo.
Amesema
wanafunzi ambao wengi wao ni vijana chuoni hapo wamekuwa mstari wa
mbele katika kuiga kila aina ya vazi kutoka tamaduni za watu wa
magharibi hali ambayo ameielezea kuwa ni ukiukaji wa mila , desturi na
tamaduni za mtanzania .
“Mtindo
huu wa kuiga tamaduni za magharibi pasipokuangalia wapi tunakwenda
haukubaliki hata kidogo,ukiangalia katika vyuo vingi vya elimu hapa
nchini wanafunzi wamekuwa wakivaa mavazi ya ajabu na yasiyofaa kabisa
katika maeneo ya chuo” amesema.
Amesema kuwa Chuo
hicho kimekaa na kubuni sera ili kuyaondoa mavazi ambayo hayaruhusiwi
kuvaliwa katika maeneo ya chuo na kubuni sera ya mavazi kwa ajili ya
wanafunzi hali itakayowajengea nidhamu wasomi hao wa fani mbalimbali
pindi watakapomaliza masomo yao chuoni hapo.
Amefafanua kuwa adhabu
mbalimbali zitatolewa kwa wanafunzi watakaokiuka agizo la uvaaji wa
mavazi yenye heshima amabazo ni pamoja na kuzuiliwa kupita getini kwa
mwanafunzi husika kuingia katika eneo la chuo kwa wale wanaotoka nje ya
hosteli na wale wanaoishi ndani ya eneo la chuo hawatapewa huduma yoyote
kama vile kuingia darasani,kantini , maktaba au ofisi yoyote ya chuo.
Aidha amefafanua kuwa wanafunzi ambao hawatakua tayari
kufuata utaratibu huo watafikishwa mbele ya kamati ya nidhamu huku
akibainisha kuwa adhabu itakayotolewa ni mwanafunzi kusimamishwa chuo kwa muda wa miezi mitatu.
Kwa
upande wake makamu mkuu wa chuo hicho ambaye pia ni mkurugenzi wa
mafunzo Bi. Bertha Kipillimba amesisitiza kuwa zoezi hilo litawahusu
wafanyakazi wote wa kampasi ya Dar es salaam na wanafunzi zaidi ya 6000 wa chuo hicho.
Amesema hivi sasa taratibu hizo za uvaaji wa mavazi yenye staha zimeingizwa kwenye kanuni za chuo na
kuongezwa kwenye masharti ya fomu za kujiunga na chuo hicho huku
akifafanua kuwa tayari wametoa kipindi cha wiki mbili kwa utekelezwaji
wa kanuni hizo na watakaokiuka kuadhibiwa kwa mujibu wa kanuni hizo.
Naye
mlezi wa wanafunzi wa hicho (Dean of Students) Bw. Faustin China
amefafanua kuwa umefika wakati wa wanafunzi hao kujitambua huku
akisisitiza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakinyoshewa vidole na jamii
kuhusu suala la uvaaji na mienendo ya wanafunzi chuoni hapo.
“Tumesemwa
vibaya kwa muda mrefu hatuwezi kuachia suala hili likaendelea, tunataka
wanafunzi wetu wavae vizuri kwa mujibu wa kanuni tulizojiwekea ili
kujenga heshima ya chuo” amesema.
Kwa
upande wao baadhi ya wanafunzi wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na
uanzishawaji wa sera ya mavazi chuoni hapo wakieleza kuwa inaingilia
uhuru wao wa kuamua huku wengine wakiupongeza uongozi wa chuo hicho kwa
kuliona suala hilo na kulichukulia hatua ili kuleta na kulinda heshima
ya chuo hicho.






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)