Msama Promotions yatoa msaada wa Sh. Milioni 2, mifuko 50 ya saruji kwa Kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Msama Promotions yatoa msaada wa Sh. Milioni 2, mifuko 50 ya saruji kwa Kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda


Eneo wanalosali kwa muda waumini wa kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda wakati ujenzi wa kanisa lao ukiendelea.
Paroko Katoliki la Mashahidi wa Uganda, Sigfrid Rwechungura (kushoto), akipokea msaada wa sh. milioni mbili kutoka kwa Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa kanisa hilo. Katikati anayeshuhudia ni Padri, Dismas Kimboi. Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Msama Promotions, waandaaji wa tamasha la Pasaka, imetoa msaada wa fedha taslimu sh. milioni 2 na mifuko 50 ya saruji kwa Kanisa Katoliki Parokia ya Magomeni.

Akikabidhi msaada huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, alisema hatua hiyo ni sehemu ya kutekeleza majukumu ya dhamira ya kampuni hiyo kama ilivyokusudiwa.

Msaada huo ulipokewa na Padri Sigfrid Rwechungura wa Kanisa Katoliki Parokia ya Magomeni, alisema anaamini utasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.

"Hatuna budi kuishukuru Kampuni ya Msama Promotions kwa msaada huu na pia tunatoa mwito kwa wengine wenye uwezo wajitokeze kusaidia kuinua kazi ya Mungu," alisema Padri Rwechungura.

Padri Rwechungura alitoa mwito kwa wadau mbalimbali bila kujali itikadi zao za dini, kujitokeza kwa wingi kuhudhuria matamasha ya Pasaka mwaka huu.

Tamasha hilo linatarajiwa kurindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 8 mwaka huu na pia litafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu.

Tayari kundi la muziki wa Injili la Glorious Celebration Spirit of Praise 'Gospel Live' linalotamba na albamu ya Niguse, limethibitisha kushiriki tamasha la Pasaka. Mbali na Glorious, waimbaji wengine waliothibitisha kushiriki mpaka sasa ni Upendo Kilahiro, Upendo Nkone na Atosha Kissava.

Msama aliyeanzisha tamasha hilo mwaka 2000, alisema limelenga kuwasaidia Watanzania milioni 1 mwaka huu kwa kuwapatia misaada anuwai.

Walengwa katika misaada hiyo ni wasiojiweza, walemavu, wajane na watoto yatima ambao wanasaidiwa fedha za ada na matumizi mbalimbali ya shule.

Mwaka jana walisaidiwa wanawake wajane 25 fedha za mitaji ya biashara sh. 150,000 kila mmoja na ilitoa sh. milioni 3 kwa waathirika wa milipuko ya mabomu iliyotokea kwenye kambi ya jeshi Gongo la Mboto, Dar es Salaam.

Msama alisema wamedhamiria kutekeleza kwa vitendo jukumu la Serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete la kupambana na ukosefu wa ajira, kwa kuwasaidia watoto yatima.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages