Na Joachim Mushi, Thehabari-Kisarawe
WAKATI Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi nchini ikijipanga kuanza kufundisha kwa kutumia
teknolojia ya kompyuta katika shule mbalimbali, wanafunzi wa darasa la
tano na sita wa Shule ya Msingi Mengwa bado wanatumia darasa moja kwa
wakati mmoja.
Hali hiyo imejulikana juzi baada ya mwandishi wa habari
hizi kutembelea shule hiyo, iliyopo Kata ya Maneromango, Wilaya ya
Kisarawe mkoani Pwani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwalimu Mkuu wa Shule ya
Msingi Mengwa, Peter Gadie alisema kitendo cha wanafunzi hao kutumia
darasa moja kimefanya wapunguziwe muda wa vipindi wa kawaida ili
kupishana kwa zamu kutumia darasa hilo.
Alisema badala ya kila kipindi kufundishwa kwa dakika harobaini
walimu wameamua kufundisha kwa dakika ishirini kila kipindi ili kupeana
zamu kuwafundisha wanafunzi hao.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia darasa hilo likiwa na wanafunzi wote yaani wa darasa la tano ambao wapo 24, na darasa la sita wakiwa 29 wakiendelea na masomo kwa pamoja huku wakitenganishwa kwa mistari ya madawati.
Akizungumzia staili ya ufundishaji wa walimu kwa kutumia darasa moja,
Gadie alisema mwalimu wa darasa la tano anapoingia darasani huendelea
na kipindi kwa dakika 20 huku akiwataka wanafunzi wa darasa la sita
kujiinamia na kujisomea ama kuendelea na kazi walizoachiwa na mwalimu
aliyetoka punde.
"Anapoingia mwalimu kufundisha darasa moja uwaamuru wanafunzi wa
darasa lingine wajisomee ama kuendelea kufanya kazi ambazo wameachiwa na
mwalimu aliyetoka...kweli wanapata usumbufu lakini haina namna maana
tunaupungufu wa madarasa shuleni kwetu," alisema Gadie akizungumza na
mwandishi wa habari hizi.
Aidha alisema tatizo hilo halipo kwa wanafunzi wa darasa la sita na
la tano pekee, kwani wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili nao usomea
darasa moja kwa kupokezana saa; ambapo darasa la kwanza huingia saa
mbili hadi saa sita na baadaye kuwapisha darasa la pili ambao huingia
saa sita na kuendelea hadi mchana.
Alisema upungufu wa vyumba vya madarasa umeifanya shule hiyo
kukodisha ukumbi wa kuoneshea video kijijini Mengwa na kulifanya darasa
la awali kwa wanafunzi wa shule hiyo wanaosoma darasa la awali kabla ya
kujiunga na darasa la kwanza.
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)