
Naibu
Mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya nchi za nje kutoka Wizara ya
Biashara ya Jamhuri ya watu wa China Bi. Xiao LU (kushoto) akizungumza
na wadau wa Biashara kutoka China na Tanzania wakati wa mkutano wa
kutangaza maonyesho makubwa ya Bidhaa kutoka nchini China ya mwaka 2012
yaliyoandaliwa na Wizara ya Biashara ya Jamhuri ya Watu wa China jijini
Dar es salaam.Maonyesho hayo yatafanyika mwezi Julai katika viwanja vya
maonyesho vya kimataifa Dar es salaam
Wadau
wa Biashara kutoka China na Tanzania wakifuatilia masuala mbalimbali
yaliyojili wakati wa mkutano wa kutangaza maonyesho makubwa ya ya mwaka
2012 ya bidhaa kutoka nchini China yaliyoandaliwa na Wizara ya
Biashara ya Jamhuri ya Watu wa China jijini Dar es salaam.
--
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Serikali
ya Jamhuri ya watu wa China kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara ya
nchi hiyo imeandaa maonyesho makubwa ya Afrika ya bidhaa zinazozalishwa
na kutengenezwa nchini China kwa lengo la kuinua na kuimarisha
ushirikiano wa kibiashara katika nchi za Afrika. Akizungumza na
wadau wa biashara kutoka China na Tanzania jijini Dar es salaam naibu
mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya nchi za nje kutoka Wizara ya Biashara
nchini humo Bi. Xiao LU amesema kuwa maonyesho hayo katika nchi za
Afrika kwa mwaka huu yatafanyika nchini Tanzania kutokana na uhusiano
mzuri wa kibiashara uliopo baina ya China na Tanzania.
Amesema
Tanzania ni moja ya eneo muhimu kibiashara katika Afrika Mashariki
linalozungukwa na nchi za Ethiopia ,Kenya, msumbiji, Uganda, Burundi,
Rwanda, Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ameongeza
kuwa bidhaa za China zinatambulika duniani kote kutokana na upatikanaji
wake, bei nzuri na ubora wake huku akifafanua kuwa kuwa nchi hiyo
imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kiteknolojia. “Hivi sasa bidhaa
zetu zinatambulika dunia nzima kutokana na ubora mzuri zilizonao pamoja
na bei nzuri,kwa maendeleo makubwa ya teknolojia tuliyonayo tumekuwa
tukiongeza ubora wa bidhaa zetu kimataifa” amesema Bi. LU. Kuhusu
maonyesho hayo amesema yatawashirikisha wafanyabishara wakubwa na wadogo
yakihusisha bidhaa mbalimbali kutoka China zikiwemo bidhaa za vyakula
,magari,mitambo ya viwandani na kilimo , vifaa vya umeme, vifaa vya
mawasiliano, vifaa vya ujenzi pamoja na bidhaa nyingine nyingi yamelenga
kuinua na kuimarisha ushirikiano kibiashara kutokana na mabadiliko ya
uwekezaji na mabadiliko ya uchumi yanayotokea duniani.
Mbali
na bidhaa hizo zitakazoonyweshwa Bi. LU amesema maonyesho hayo
yataimarisha ushirikiano wa kiutamadauni baini ya Tanzania na China na
nchi nyingine za Afrika ya mashariki. Kwa upande wake Rais wa Chama
Cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda nchini Tanzania (TCCIA) Bw. Aloys
Mwamanga amesema maonyesho hayo ni changamoto kwa wafanyabishara,
wakulima na wenye viwanda wa Tanzania kuongeza uzalishaji na ubora wa
bidhaa zao ili waweze kusafirisha bidhaa nyingi zaidi kwenda nchini
China na kuongeza pato la Taifa.
Pia
ametoa wito kwa washiriki hao kutoka nchini China kujikita katika
kuonyesha bidhaa za uzalishaji zinazoweza kuongeza thamani ya mazao
zikiwemo bidhaa za kilimo na kuwataka kuongeza juhudi ya upambanaji wa
bidhaa zisizokidhi viwango.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)