"Uchaguzi
wa Ubunge Arumeru Mashariki ni kipimo cha namna wananchi mnavyoridhika
na watawala, namna mnavyoridhika na mgawo wa Ardhi na namna
mnavyoridhika na mgawanyo wa Maji katika Wilaya yenu". Haya yalikuwa
baadhi ya maneno yangu katika hotuba ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Taifa
CHADEMA ndugu Freeman Mbowe kuzindua kampeni za chama chetu katika
viwanja vya Leganga katika mji mdogo wa USA River wilayani Arumeru.
Siku
moja kabla ya siku ya uzinduzi nilikuwa najisomea makala mbalimbali
kuhusu Wilaya ya Arumeru. Pia nilitumia muda mrefu kuzungumza na
wananchi wa Meru ili kujua uchaguzi huu una maana gani kwao. WaMeru
wengi niliozungumza nao waliniambia namna wanavyochukizwa na ukosefu wa
Ardhi kwa wananchi. Baadhi waliniambia kwamba Kama Serikali
haitachukulia suala la Ardhi kwa uzito wake Meru kutatokea vurugu kubwa
sana.
Vurugu
Meru sio Jambo jipya kabisa. Inakumbukwa kwamba miaka ya 1950
kulitokea fujo na wananchi kuchomewa nyumba zao ili kupisha wakulima
wakubwa kutoka Afrika Kusini (makaburu) katika eneo la Engarananyuki.
Vurugu hizi ndio zilipelekea WaMeru kuchanga fedha kumpeleka ndugu
Jafet Kirilo huko Umoja wa Mataifa kutetea Ardhi ya Wameru mwaka 1952
kufuatia vurugu za mwaka 1951. Licha ya juhudi hizo bado Ardhi ni
tatizo kubwa kwa wananchi wa Meru.
Mashamba
makubwa ambayo walipewa walowezi wakati wa Uhuru yaligawiwa kwa
familia chache sana Meru. Wanasiasa walijipa mashamba makubwa na
mengine mpaka Leo hayakugawiwa. Ujamaa na utaifishaji wa mashamba
haukufanyika Meru kwa mshangao mkubwa sana na hata mashamba ambayo
Serikali ya Mwalimu Nyerere iliagiza wapewe wananchi walipewa Wabunge,
Madiwani, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri
(soma Brian Cooksey kuhusu uwekezaji katika Maua, June 2011).
Hivi
Leo Ardhi kubwa ya Meru imeshikwa na matajiri na kulimwa Maua. Kilimo
hiki cha Maua mwaka 2008 kiliingizia Taifa fedha za kigeni takribani
tshs 150bn. Hata hivyo kuna malalamiko makubwa sana ya wananchi
wanaofanya kazi katika mashamba haya kuhusu malipo duni na nyenzo za
kufanyia kazi. Kuna malalamiko kuhusu kemikali na madawa yanayotumika
na afya ya mfanyakazi kutozingatiwa.
Ifahamike
kwamba Benki ya Rasilimali Tanzania inasimamia mikopo ya zaidi ya tshs
50bn ambazo kampuni za Maua zilipewa kwa Dhamana ana ya Serikali.
Katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, suala
hili liliibuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa TIB kukiri kwamba hakuna kampuni
umeanza kulipa mikopo hii. Ni dhahiri Serikali itajikuta inalipa
madeni haya yaliyokopeshwa kwa kampuni binafsi! Hii pia inaonyesha
namna amabvyo serikali inafanya haraka na wepesi kusaidia wawekezaji
kuliko wananchi wanaoteseka na kukosa Ardhi ya kulima na kujipatia
ruziki.
Mwisho
kabisa nimeona makundi ya vijana wasio na ajira na hivyo kukosa
Kipato. Vijana wengi wanashinda kwenye stendi za mabasi na kuita
abiria. Ukosefu wa Ajira kwa vijana Kama tusemavyo kila wakati ni
changamoto kubwa sana kwetu viongozi na hasa viongozi vijana. Natumai
ndugu Joshua Nassari atahusisha suala la Ardhi na Maji katika muktadha
mzima wa Ajira na Kipato kwa wananchi wa Arumeru Mashariki. Uchaguzi wa
Arumeru ni uchaguzi kati ya kuwa na Ardhi au kuendelea kutokuwa nayo.
Ni uchaguzi muhimu kwa watu wa Meru. Wasio na Ardhi watamchagua mgombea
atakayesimamia mgawo wa Ardhi unaozingatia haki. Mgombea huyo ni
mgombea wa CHADEMA ndugu Joshua Nassari.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)