Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh (katikati) akiwa
ameambatana na wenyeviti wa kamati za kudumu za bunge akiwasilisha
taarifa ya ripoti tano za kaguzi maalum kuhusu Ukaguzi wa ufanisi na
Thamani ya Fedha kwa waandishi wa habari leo mjini Dodoma.
Kaguzi
hizo zimehusisha Ukaguzi maalum wa wilaya ya Kishapu, Usimamizi wa
matengenezo ya magari ya serikali, Usambazaji wa maji mijini, ukaguzi wa
mapato yatokanayo na uvunaji wa misitu na Mapato yanayokusanywa na
wakala katika Halimashauri.
Baadhi
ya watendaji wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
wakifuatilia ripoti mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na Mkaguzi
Mkuu Bw. Ludovick Utouh mjini Dodoma. Picha na Aron Msigwa – MAELEZO
******************************************************************
Na Aron Msigwa –MAELEZO.
Ofisi
ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini
ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali kiasi cha shilingi bilioni 7
kufuatia ukaguzi maalum uliofanyika katika Halmashauri ya wilaya ya
Kishapu, mkoani Shinyanga.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo mjini Dodoma wakati wa kuwasilisha ripoti za
matokeo ya kaguzi 5 za ufanisi/Thamani ya fedha Mdhibiti na Mkaguzi
mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Rudovick Utouh akiwa ameambatana na
baadhi ya wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge amesema kuwa Ofisi yake
imebaini matukio 14 yenye jumla shilingi bilioni 7 ambayo yana kila
dalili za ubadhirifu wa fedha za umma.
Bw.
Utouh amefafanua kuwa ofisi yake imebaini ubadhirifu huo kufuatia
uhakiki wa kina na ukusanyaji wa ushahidi kuhusiana na hati za malipo
zilizokosekana wakati wa ukaguzi uliopita wa mwaka wa fedha 2009/2010 na
pia kufanya mahojiano na viongozi na wahasibu ambao wanahusika na
utunzaji wa nyaraka za malipo ili kubaini ukweli kuhusiana na upotevu wa
hati hizo za malipo.
Amesema
wataalam wa ofisi yake katika kubaini ubadhirifu huo ilipitia hati zote
za malipo sanjari na kuhakiki stakabadhi za malipo ili kujua uhalali wa
malipo yaliyofanywa na Halmashauri bila kuidhinishwa na mkurugenzi wa
Halmashauri pamoja na kufanya mahojiano na viongozi mbalimbali wa
Halmashauri hiyo ili kupata maoni yao.
Amebainisha
kuwa ukaguzi huo maalum uliofanywa katika wilaya ya Kishapu ofisi yake
iligundua mambo mbalimbali yaliyojitokeza yakiwemo udhaifu katika mifumo
ya udhibiti wa ndani ,mabadiliko ya wakurugenzi watendaji wa
Halmashauri kila baada ya muda mfupi,Mabadiliko ya mara kwa mara katika
Idara ya fedha yakihusisha mweka Hazina, Udhaifu wa kitengo cha ndani
cha ukaguzi kutokuwa na mkuu wa kitengo pamoja na mabadiliko katika
Idara ya Mipango.
Mambo
mengine ni pamoja na udhaifu katika idara mbalimbali za wilaya hiyo
zikiwemo Ujenzi,Idara ya maji,kitengo cha Ugavi pamoja na udhaifu katika
kitengo cha Uhasibu ambacho kiligundulika kuandika vocha na kulipa
fedha taslimu bila idhini pamoja na kutumia makusanyo ya fedha kabla ya
kupelekwa benki.
Pia
amefafanua kuwa ofisi yake iligundua taarifa mbalimbali za kibenki
zilizoghushiwa na kutumika zaidi ya shilingi milioni 200 na hundi
zilizoghushiwa na kulipwa kiasi cha shilingi milioni 500 na uhamisho wa
fedha toka akaunti moja kwenda nyingine bila idhini ya mkurugenzi na
kutumika kinyume na malengo pamoja na uhamisho wa fedha kwenda kwenye
akaunti zisizofahamika.
Bw.
Utouh ameongeza kuwa kulikuwa na matumizi yaliyofanywa kinyume na
malengo yaliyokusudiwa katika miradi ya maji,mfuko wa afya wa pamoja
huku akifafanua kuwa ofisi yake imebaini kuwepo kwa ushirikiano kati ya
watumishi wa Halmashauri na watumishi wa benki katika kufanikisha
vitendo hivyo vya ubadhirifu wa fedha za halmashauri.
“Hali
hii ya ushirikiano kati ya watumishi wa Halmashauri na benki umeonekana
katika kaguzi zetu maalum tulizofanya huko nyuma kwenye Halmashauri za
wilaya ya Kilosa na Rombo” amesema.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
serikali za mitaa Augustino Mrema ambaye pia ni mbunge wa Vunjo
ameipongeza ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali kwa
kubainisha ubadhirifu huo na kusisitiza kuwa kuwa matokeo hayo lazima
yafanyiwe kazi na serikali.
“Naiomba
serikali izifanyie kazi ripoti hizi ili ili matokeo yake yazae matunda
na wahusika wote walioshiriki katika kufanya uharifu huu wakamatwe na
kufikishwa mahakamani na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi”
amesisitiza.
Naye
Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma Zitto
Kabwe ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini ameipongeza ofisi ya CAG
kwa kazi nzuri iliyofanyika na kuiomba ikamilishe ukaguzi wa Shirika la
Usafiri Dar es Salaam (UDA).
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)