Kumekuwa
na tafsiri zisizosahihi juu ya baadhi ya maamuzi yaliyofanywa na kikao
cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichoketi mjini Dodoma tarehe
12/02/2012 chini ya uenyekiti wa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti
wa CCM Taifa.
Jambo
kubwa ambalo linapotoshwa sana ni la uamuzi wa NEC kuunda baraza la
Ushauri la Wazee. Uamuzi ambao kimsingi ulifikiwa kwenye kikao cha NEC
cha mwezi Aprili mwaka 2011 Mjini Dodoma kikao ambacho kiliridhia
kufanyika kwa mageuzi ndani ya Chama.
Kikao
cha tarehe 12/02/2012 cha NEC kiliridhia tu mabadiliko ya katiba ya CCM
ya mwaka 1977 toleo la 2010 ili kuruhusu kuundwa kwa baraza hilo.
MSINGI WA UAMUZI HUU.
#. Ni ushauri wa wastaafu wenyewe.
Wazo
la kuundwa kwa baraza hili lilitokana na ushauri wa baadhi ya wazee
wenyewe wastaafu wakizingatia wingi na urefu wa vikao husika, na si
mpango au mkakati wa kuwaengua makusudi wastaafu hao kama inavyodaiwa na
baadhi ya wapotoshaji.
Ilikuwa
ni ushauri wao kwamba baada ya kustaafu badala ya kulazimika kuhudhuria
vikao vya kitaifa kila mara basi wapewe muda wa kupumzika na
wanapotakiwa kutoa ushauri watumiwe badala ya utaratibu wa sasa wa
kulazimika kuhudhuria vikao ambavyo kwakweli ni vingi na wakati mwingine
huisha usiku wa manane.
#. Umuhimu wa busara zao kwa Chama.
Baada
ya wazo la wazee wetu kupumzika, huku tukizingatia kuwa busara zao bado
ni muhimu sana kwa Chama na Taifa, busara ikatumika badala ya kupumzika
kabisa basi tuunde Baraza la Ushauri la Viongozi wa Kitaifa wastaafu.
Na
hii haina maana kuwa hawaruhusiwi kuhudhuria vikao vya Chama na kuwa
hawatatumika kwa kazi za Chama na Taifa kwa ujumla, isipokuwa mabadiliko
haya yanaondoa ulazima wa wao kuhudhuria vikao hivyo kama ilivyokuwa
mwanzo.
#. Ni namna bora ya kuwaenzi kwa mchango wao kwa Chama.
Chama
makini chochote kitatafuta utaratibu bora wa kuwaenzi waasisi wake na
kuendelea kuvuna busara na hekima zao katika kuendelea kukijenga Chama.
Katika hili CCM imeonyesha mfano mzuri unaostahili kuigwa na vyama
vingine. Kuundwa kwa baraza hili na kutambuliwa rasmi na katiba ya Chama
ni uthibitisho tosha wa namna CCM inavyothamini wastaafu hawa.
Kwa kuwaundia baraza la ushauri ni namna nzuri ya kuendelea kutumia busara zao kwa kutumia chombo kinachotambulika kikatiba.
Wajumbe wa baraza hili.
Kwa mujibu wa uamuzi huo wajumbe wa baraza hili ni:
1.
Wenyeviti wastaafu wa CCM Taifa ambao kwa utamaduni wa CCM huwa pia
ndio Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2.
Makamu wenyeviti wastaafu bara na visiwani, ambapo kwa Zanzibar kwa
mujibu wa utamaduni wa CCM ndio huwa pia marais wastaafu wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwenyekiti
wa baraza hili atakuwa ni Mwenyekiti yule aliyewatangulia wenzake
kustaafu. (seniority). Na watakutana pale tu wanapoona ipo haja ya
kukutana.
Wanaweza kuombwa kuhudhuria vikao vya Kitaifa au wao kuomba kuhudhuria kulingana na mazingira na mahitaji ya wakati husika.
Kazi
kubwa ya baraza hili ni kushauri Chama na serikali zake zinazotokana na
CCM na si kudhibiti Chama, Serikali na Viongozi kama inavyotafisiriwa
na baadhi ya wapotoshaji.
CCM
inawasihi wale wanaoendelea kupotosha maamuzi haya kwa makusudi au kwa
bahati mbaya kuacha mara moja upotoshaji huo, kwani una lengo la
kuonyesha kuna mgogoro mkubwa kati ya Chama na wazee wetu wastaafu
wakati ukweli si huo.
Chama
Cha Mapinduzi kinathamini sana busara na mchango wa wastaafu hawa
katika ujenzi wa Chama na Taifa kwa ujumla hakiwezi kuwaong'oa au
kuwatupa kama inavyojaribu kupotoshwa na baadhi ya watu. Tuwatendee haki
wazee wetu hawa badala ya kutumia majina yao na uamuzi wa Chama ambao
una baraka zao vibaya.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye
KATIBU WA NEC ITIKADI NA UENEZI CCM TAIFA
15/2/2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)