Ndugu zangu, JUMATANO hii ya leo kuna kusanyiko
kubwa la watu kule Ifakara. Ni WaTanzania wanaoshiriki kumsindikiza
kwenye safari yake ya mwisho, ndugu yetu mpendwa, Regia Estelatus Mtema.Ni Jumatano hii ya leo, WaTanzania
kwa mamilioni, nao, kwa kuelekeza fikra zao kwa Regia, wanashiriki
kumsindikiza ndugu yetu Regia Mtema kwenye safari yake ya mwisho hapa
duniani.
Katika maisha kuna
visivyoshikika,visivyogusika, lakini vipo. Hisia, kwa mfano, zipo na
zinaishi. Jumatatu usiku ya wiki hii nilifika nyumbani kwa wazazi wa
Regia pale Tabata- Chang’ombe. Nilikwenda kutoa pole kwa wafiwa.
Regia alikuwa ni mmoja wa rafiki na
dada zangu. Pale Tabata nilimwambia Remija, pacha wa Regia, kuwa
niliongea kwa simu na Regia mara ya mwisho Jumapili iliyopita. Remija
akanijibu;
” Nilikuwa nae wakati mkiongea!”
Ndio, mazungumzo yangu ya mwisho na
Regia yalihusu ombi langu la yeye Regia, kwenye siku ya kutoa tuzo ya
washindi wa mchakato wa kumtafuta mbunge bora kijana kwa mwaka 2011,
mchakato ulioendeshwa na mtandao wangu wa kijamii wa Mjengwablog. com,
atoe mada ya nusu saa juu ya nafasi ya mwanamke katika kushiriki
uongozi na changamoto zake.
Kwamba mada hiyo ivuke mipaka ya
siasa za vyama. Ilenge kwenye kuwajengea ari na moyo wa kujiamini
wanawake vijana wa nchi hii. Regia alinikubalia ombi langu.
Ni Regia Mtema ambaye pia
alipendekezwa na wadau wa mtandao wangu wa kijamii kushiriki na
hatimaye kushika nafasi ya pili katika mchakato husika. Ni kwenye kundi
la wanawake akiwa nyuma ya Halima Mdee. Nafasi ya tatu ilishikwa na
Esther Bulaya.
Na hapa naungana na mwanasiasa kijana
Nape Nnauye aliyesema; Regia Mtema alikuwa ni daraja kwa vijana bila
kujali tofauti zao za kiitikadi.
Ni kweli, Regia alikuwa ni daraja.
Katika dunia hii ni nadra sana kukutana na wanadamu wengi wenye urafiki
na watu wawili walio kwenye uadui huku watu hao walio kwenye uadui
wakilifahamu hilo na wakaendelea na urafiki wao na mtu huyo.
Nadharia iliyozoeleka ni ile ya ;
rafiki wa adui yangu ni adui yangu. Kwa Regia Mtema nadharia hiyo
haikufanya kazi. Regia ameweza kudhihirisha kinyume chake, kuwa adui
yako anaweza kuwa rafiki wa Regia na wewe na Regia mkabaki kuwa
marafiki. Ni watu wachache sana duniani waliojaliwa kuwa na sifa hizo.
Na kifo cha Regia kinathibitisha
hilo. Kimewakusanya pamoja hata mahasimu. Kimewaleta pamoja hata
wagombanao. Hakika, kumuenzi Regia kuliko na maana, ni kuendelea
kuliimarisha daraja alilotujengea. Tuache sasa siasa za ubaguzi.
Wanadamu tunaweza kutofautiana katika hoja, lakini hatuna sababu za
kuchukiana na kutakiana mabaya.
Na kuna wanaotaka kuutumia msiba wa
Regia kujijenga kisiasa au kuwabomoa wenzao kisiasa. Naamini, Regia
asingependa msiba wake utumike kwa kuendeleza ajenda za siasa za
uhasama; kupandikiza chuki, kuleta migongano na hila nyingine.
Naam, katika maisha kuna
visivyoshikika, visivyogusika, lakini vipo. Maana, jua laweza
kuliangazia jiwe. Nalo jiwe likapata mwanga. Likapata joto pia. Lakini,
jua laweza kuliangazia jicho lako, nalo likapata joto. Hata hivyo, kwa
mwanadamu, kuna unachoweza kukifanya ambacho jiwe kamwe haliwezi
kukifanya. Ndio, unaweza kulitazama jua kwa jicho lako. Jiwe huangaziwa
mwanga wa jua, litapata joto, lakini jiwe haliwezi kulitazama jua.
Juzi usiku pale Tabata nilipokaa na
kuzungumza na Remija, pacha wa Rejia, kuna mwanga niliouona. Nilimwona
Remija akiinamisha kichwa na kufikicha macho yake yaliyokuwa yakilengwa
na machozi.
Kisha nikamwuliza; wewe na Regia mlikuwa mkigombana utotoni? Na kwanini wewe hupendi siasa na mwenzako alipenda sana siasa?
Remija akanitazama kwa macho yake makubwa na yenye mvuto. Kisha akaangua kicheko. Hapo nikamwona Regia. Wamefanana sana.
Niliuona mwanga unaongazia jiwe,
nalo jiwe likapata joto. Ni vile visivyoshikika, visivyogusika. Lakini,
ni vyenye kuamsha hisia. Vyenye kuleta mwanga kunako giza. Vyenye
kuleta matumaini katika hali ya kukata tamaa.
Regia amewapigania wengi. Amewaletea matumaini walo wengi. Ni wale walio katika hali ya kukata tamaa. Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi, Amen.
-
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)