Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepatwa na majonzi makubwa na
kinasikitika sana kwa kifo cha Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa,
Mheshimiwa Regia Mtema
ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira.
Mheshimiwa
Regia Mtema amefariki leo tarehe 14 Januari 2011 kwa ajali ya gari
katika eneo
la Ruvu darajani.
Katika uhai wake marehemu Regia Mtema amefanya kazi
mbalimbali za kisiasa na kijamii katika taifa. Marehemu Regia Mtema amezaliwa
tarehe 21 mwezi Aprili mwaka 1980 na kusoma shule za sekondari kidato cha
kwanza mpaka cha sita katika shule ya sekondari ya Forodhani na Shule ya
Wasichana ya Sekondari ya Machame. Marehemu Regia Mtema alipata shahada yake ya
kwanza (Bsc Home Economics and Human Nutrition) katika Chuo Kikuu cha Kilimo
cha Sokoine.
Mara baada ya kuhitimu masomo yake marehemu Regia Mtema
alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na CHADEMA na
kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA na
baadaye kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya CHADEMA
nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa mbunge wa viti
maalum.
Viongozi wakuu wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Katibu Mkuu Dr.
Wilbroad Slaa, wajumbe wa kamati kuu, wakurugenzi wa chama makao makuu na
wabunge wamejumuika hivi sasa na familia ya marehemu katika kipindi hiki
kigumu.
CHADEMA inatoa pole kwa familia ya marehemu Regia Mtema,
wanachama wote na wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususani wa Jimbo la Kilombero
kutokana na msiba huu wa ghafla katika wakati ambapo mchango wake ukihitajika
kwa chama na kwa taifa.
Taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada
ya kukamilisha majadiliano baina ya familia ya marehemu, chama na Ofisi ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mipango ya mazishi ya marehemu inapangwa nyumbani kwa
Baba wa Marehemu Regia Mtema, Ndugu Estelatus Mtema, Tabata Chang'ombe.
Ratiba ya maziko itatolewa baada ya kukamilika kwa taratibu zinazopangwa
na familia ya marehemu, Ofisi ya Bunge na chama.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Regia Mtema, mahali pema peponi. Amina.
Imetolewa
na:
John
Mnyika(Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)