Mbunge Wa Bumbuli(CCM)Mh.January Makamba Awasilisha Hoja Binafsi Bungeni - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Mbunge Wa Bumbuli(CCM)Mh.January Makamba Awasilisha Hoja Binafsi Bungeni

MBUNGE wa Bumbuli, January Makamba (CCM),
--
Na Elizabeth John

MBUNGE wa Bumbuli, January Makamba (CCM), amewasilisha hoja zake binafsi katika ofisi ya Bunge akitaka mkutano ujao, Bunge liazimie kuitaka serikali ilete muswada wa sheria ya kudhibiti upangaji wa nyumba pamoja na sheria ya kuwalinda watumiaji wa huduma za kifedha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,Makamba alisema asilimia 60 ya wakazi wa mjini wanaishi katika nyumba za kupanga ambapo kwa wastani Chama cha Wapangaji Tanzania, hutumia zaidi ya asilimia 40 ya mapato kulipia kodi ya makazi yao.

Alisema kutokuwepo kwa sheria inayodhibiti biashara ya pango kumewapa wenye nyumba nguvu kubwa dhidi ya wapangaji ambapo wanaweza kuwafukuza bila notisi za kutosha na kuwawezesha kujiandaa kutafuta makazi mapya na unyang’anyi wa mali pale wanaposhindwa kulipa au kuchelewesha kodi.


“Kutokuwepo kwa udhibiti wa pango kumeongeza wahalifu kwa sababu watu wasiojulikana wanaweza kupanga kwenye nyumba na kufanya mambo ya uhalifu bila kufahamika, hii inatokana na kutokuwa na mikataba inayotambulika kati ya wapangaji na serikali,” alisema Makamba.


Alisema kunapotokea majanga kama vile mafuriko na moto, wapangaji hupoteza kila kitu na hawapati fidia yoyote ilhali serikali imekuwa ikiwafidia wenye nyumba ingawaje mara nyingi ndiyo wenye makosa ya kutoweka bima au kujenga maeneo hatarishi.
Kuhusu sheria ya kuwalinda watumiaji wa huduma za kifedha alisema taasisi za kibenki na zisizo za kibenki, vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa (saccos); na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) hutumia njia zisizo sahihi.

Alisema upanukaji huu wa huduma zinazotolewa na sekta ya kifedha hauendani na udhibiti wa haki za watumiaji wa huduma; kumekuwepo na ongezeko la ripoti za usumbufu, udanganyifu na dhuluma zinazofanywa na watoa huduma dhidi ya watumiaji.
“Wananchi wakiwa na upeo mzuri wa maswala ya kifedha watakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya busara ya kifedha kwa ajili yao na familia zao, ufahamu huo pia utawawezesha kutambua na kuchagua huduma za kifedha zitakazokidhi mahitaji yao bila kujiingiza katika hatari ya kudhulumiwa au kufilisika,” alisema Makamba.

Aliongeza kuwa ulinzi mahususi wa watumiaji wa huduma za kifedha utaongeza imani katika sekta ya kifedha na utawavuta wananchi wengi katika mfumo rasmi wa kifedha na kupunguza matatizo yanayowadidimiza wananchi kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages