Maalim Seif Sharif Hamad:Mazoezi ni Muhimu Katika Kuimarisha Afya - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Maalim Seif Sharif Hamad:Mazoezi ni Muhimu Katika Kuimarisha Afya

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi zawadi maalum kwa mwanamichezo mahiri na mbunifu wa ufundi maarufu kwa jina la Sugu, huko uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar ambako kulikuwa na kilele cha bonanza la tatu la mazoezi. Kushoto ni mwenyekiti wa ZABESA Mohd Ziddy.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi zawadi maalum kwa mwanamichezo mahiri na mbunifu wa ufundi maarufu kwa jina la Sugu, huko uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar ambako kulikuwa na kilele cha bonanza la tatu la mazoezi. Kushoto ni mwenyekiti wa ZABESA Mohd Ziddy.Picha na Salmin Said-Ofisi ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
--
Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar imetakiwa kufanya kampeni maalum ya kuwahamasisha wananchi kufanya mazoezi ili kulinda afya zao.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika kilele cha Bonanza la tatu la mazoezi ya viuongo huko uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.

Amesema mazoezi ni muhimu katika kulinda na kuimarisha afya za binadamu na kwamba yanaweza kuokoza fedha nyingi ambazo zingetumika kwa matibabu.



Amefahamisha kuwa magonjwa mengi yakiwemo ya presha, moyo, figo na unene yanaweza kuepukwa iwapo wananchi watahamasika kufanya mazoezi, na kutoa changamoto ya kuwepo na kikundi cha mazoezi katika kila shehia Unguja na Pemba.

Sambamba na hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa wito kwa vijana kushirikiana na ofisi yake katika kupiga vita majanga mbali mbali yanayoikabili jamii hasa vijana yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya, maambukizi ya virusi vya UKIMWI na uchafuzi wa mazingira.
Amesema ofisi yake iko tayari kushirikiana na nguvukazi hiyo ya vijana katika kutekeleza mipango ya serikali ambayo lengo lake ni kuwaondoshea usumbufu wananchi.

Katika risala yao, wanachama wa vikundi hivyo vya mazoezi vipatavyo 32, wameiomba serikali kuwatafutia eneo maalum la kufanya mazoezi kama ilivyo kwa michezo mengine, ili kuepusha usumbufu wanaoupata wakati wakifanya mazoezi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mazoezi Zanzibar ZABESA Bwana Mohd Ziddy, amesema chama hicho kinajipanga ili kupata wanachama wengi zaidi, sambamba na kuandaa Bonanza la Kimataifa katika siku zijazo.

Kauli mbiu ya Bonanza hilo ambalo limevihusisha vikundi vya mazoezi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara ni Fanya Mazoezi, Imarisha Afya yako.

Pia Makamu wa Kwanza wa Rais ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuliingiza suala la michezo katika mitaala yake ya Elimu ili kuibua vipaji kwa wanamichezo ambavyo vimekuwa vikipotea.

Amesema upo uwezekano kwa Zanzibar kupata ubingwa wa michezo mbali mbali kutokana na vipaji vya vijana wake, lakini vinahitaji kuibuliwa na kuendelezwa kwa maslahi ya vijana hao na taifa kwa jumla.

Amesema michezo ni ajira, kwani vijana wengi wa Afrika Magharibi na mataifa ya Magharibi wamekuwa wakinufaika kutokana na michezo, jambo ambalo pia huzitangaza nchi zao kimataifa.

Katika bonanza hilo Maalim Seif alitoa vyeti maalum vya ushiriki kwa viongozi wa vikundi hivyo, pamoja na kukabidhi zawadi maalum kwa ajili ya mwanamichezo mahiri maarufu kwa jina la SUGU ambaye amekuwa akibuni na kutengeneza gari kwa kutumia kipaji alichonacho.
Mapema Makamu wa Kwanza wa Rais aliungana na wanamazoezi hao katika matembezi yaliyoanzia viwanja vya muembe kisonge hadi uwanja wa Amaan.

 Na
Hassan Hamad 
Ofisi ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages