Rais
Jakaya Kikwete akimpongenza Balozi Liberata Mulamula kwa kazi nzuri
aliyoifanya katika sekreteriati ya Maziwa Makuu kwa miaka mitano.Pembeni
ni Dr Asha-Rose Migiro Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Mkutano
wa Nchi Maziwa Makuu(ICGLR) Unafanyika hoteli
ya Speke Commonwealth Resort kitongoji cha Munyonyo nje kidogo ya
Kampala ambapo Balozi Mulamula leo ndio amemaliza rasmi muda wake wa
kufanyakazi kama Katibu Mtendaji wa ICGLR na kumuachia kiti Prof Lumu
Alphonse Ntumba Luaba (59) wa DRC.
Picha ya Pamoja ya Viongozi Mbalimbali wanaoshiriki mkutano wa nchi za maziwa makuu Unafanyika hoteli ya Speke Commonwealth Resort kitongoji cha Munyonyo nje kidogo ya Kampala.Picha na IKULU
---
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Alhamisi, Desemba 15, 2011 ameungana na viongozi wenzake wa nchi
wanachama wa Umoja wa Nchi za Maziwa wa International Conference on
Great Lakes Region(ICGLR) kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka huu wa
Umoja huo kwenye Hoteli ya Munyonyo Resort, nje kidogo ya mji mkuu wa Uganda wa Kampala.
Rais
Kikwete na ujumbe wake amewasili nchini Uganda asubuhi ya leo na kwenda
moja kwa moja kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili.
Miongoni
mwa viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi wa mkutano huo ni pamoja na
Rais Michael Chifunya Sata wa Zambia ambaye amemaliza muda wake wa kuwa
mwenyekiti wa ICGLR na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, mwenyeji wa
mkutano huo na mwenyekiti mpya wa Umoja huo.
Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni Rais Mwai Kibaki wa Kenya na Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi. Nchi
nyingine wanachama wa ICGLR zilizowakilishwa na viongozi wa ngazi mbali
mbali ni Sudan ambayo imewakilishwa na Makamu wa Rais Dkt. Alhaj Adam
Yusuf, Angola, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Congo
Brazzaville na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).
Katika
siku ya kwanza ya mkutano huo leo, viongozi na wawakilishi wa nchi
wanachama wa ICGLR wamejadili suala zima la Ukatili wa Kijinsia na
athari zake katika nchi za Maziwa Makuu ambako kumekuwa na aina moja ya
vita na mapigano kwa miaka 17 iliyopita.
Ukatili
wa Kijinsia katika nchi ambazo zinakabiliwa na mapigano na vita ama
zimetoka katika hali hiyo unachukuliwa kuwa ni pamoja na ubakaji,
mashambulizi wa kijinsia, kupiga, utekaji nyara, mauaji ya makusudi,
utumwa wa kijinsia, ndoa za kulazimishwa na kufanya mapenzi na watoto
wadogo.
Kesho,
mkutano huo utajadili masuala mengine yanayohusiana na Umoja huo ikiwa
ni pamoja na kujadili hali ya usalama katika nchi wanachama wa ICGLR, na
kupokea na kujadili ripoti ya mkutano wa mawaziri wa usalama na ulinzi
kuhusu athari za majeshi hasi katika eneo hilo.Mkutano huo pia utajadili
na kutoa uamuzi kuhusu maombi ya nchi za Sudan Kusini kujiunga na
ICGLR.
Mkutano
huo wa mwaka huu pia utajadili maendeleo yaliyopatikana kutokana na
maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano maalum wa ICGLR uliofanyika Lusaka,
Zambia mwaka jana kuhusu mapambano dhidi ya uvunaji na biashara haramu
ya maliasili za nchi hizo.
Katika
kikao hicho, wakuu hao wa nchi pia watateua Katibu Mtendaji mpya wa
ICGLR kufuatia kumalizika kwa kipindi cha uongozi cha Balozi Liberata
Mulamula wa Tanzania.
Muhula
wa uongozi wa Balozi Mulamula ulimalizika tokea mwaka jana wakati wa
mkutano wa Lusaka, lakini wakuu wa nchi wanachama wa ICGLR walimwomba
balozi huyo wa Tanzania kuendelea kushikilia nafasi hiyo kwa mwaka mmoja
zaidi ili kutoa nafasi kwa nchi wanachama kutafuta watu wanaofaa kujaza
nafasi hiyo.
Ends
IMETOLEWA NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
DESEMBA 15, 2011
KAMPALA
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)