MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda
--
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UTANGULIZI
Itakumbukwa kwamba Desemba 15 mwaka huu, Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi aliniteua kuwa mjumbe katika
Kamati ya Kitaifa ya Kukamilisha Mchakato wa Kupata Vazi la Taifa.
Siku chache baada ya uteuzi huo, nilipokea wito wa kuitwa na kuhojiwa na
Jeshi la Polisi kutokana na makala ambayo ilichapishwa katika gazeti la
Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 30 mwaka 2011.
Kufuatia mahojiano hayo, Desemba 21 nilifikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, ambako polisi na wanasheria wa serikali
walinifungulia mashtaka ya kuwachochea askari kutoitii Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nilipata dhamana katika kesi hiyo ambayo imeahirishwa hadi Januari 19, 2012 itakapotajwa tena.
MSIMAMO NA UAMUZI WANGU
Baada ya kutafakari kwa kina kuhusu uteuzi wa Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo sambamba na uamuzi wa serikali kunihoji na
kunifungulia mashitaka, busara yangu binafsi na kwa kuzingatia ushauri
nilioupata kutoka kwa wahariri wenzangu, nimefikia uamuzi wa kujitoa
katika Kamati ya Kutafuta Vazi la Taifa.
Nimelazimika kufikia uamuzi huo kwa sababu zifuatazo:
1. Mosi, uamuzi wa serikali kupitia Jeshi la Polisi na Waendesha
Mashitaka kunifungulia kesi ya kuchochea uasi inanifanya niamini kwa
dhati kwamba, haina imani nami binafsi na ina nia ya dhati ya
kuhakikisha ninaadhibiwa na hivyo kukinzana na imani ambayo Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ameionyesha kwangu kupitia uteuzi
wake.
2. Pili, nimelazimika kufikia uamuzi huo wa kujitoa katika kamati hiyo
baada ya kujiridhisha pasipo shaka kwamba mchakato mzima uliohusisha
sakata langu kama Mhariri Mtendaji kuhojiwa na kufunguliwa mashitaka na
polisi na hatimaye kufikishwa kwangu mahakamani usingeweza kufikiwa
pasipo kuishirikisha Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
ambayo inaongozwa na Waziri Nchimbi.
3. Tatu, kwa kuyatambua hayo nimeona itakuwa ni uamuzi wenye hekima
kujitoa katika kamati hiyo kwa kuzingatia uhalisia kwamba nitashindwa
kutimiza wajibu wangu ipasavyo nikiwa mjumbe katika kamati hiyo, sababu
kubwa ikiwa ni kuwapo kwa hali ya kutoaminiana na kutiliana shaka kati
ya wizara na waziri Nchimbi kwa upande mmoja na mimi mteule katika
kamati huyo kwa upande mwingine.
4. Mwisho, wakati nikichukua uamuzi huo mgumu, napenda kuchukua fursa
hii kumshukuru sana Waziri Nchimbi kwa kuonyesha imani nami hata
kuniteua kuwa miongoni mwa wajumbe wanane wanaounda Kamati ya Kitaifa ya
Vazi la Taifa.
Imetolewa na Absalom Kibanda Mhariri Mtendaji Free Media Ltd Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)