Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza wakati wa mkutano wa majadiliano wa Viongozi wakuu 194 wa nchi wanachama wa
Itifaki wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya Tabianchi, juu ya
kupunguza uzalishaji wa gesijoto Duniani kabla ya kuanza kwa mkutano
mkuu wa 17 wa umoja huo uliofanyika jana Desemba 6 mjini Durban, Afrika
ya Kusini
....................................
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
anahudhuria mkutano wa dunia wa Mazingira unaofanyika nchini Afrika
Kusini katika jiji la Durban ukiwa na agenda nzito kuhusu mchango wa matafia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Tangu
maandalizi ya mkutano huu kuanza mwanzoni mwa mwaka, kumekuwa na
makundi mbalimbali yanayozungumzia namna ya kuiweka dunia katika hali
shwari sambamba na kuhakikisha uharibifu wa mazingira hauendelei kwa
kuwa madhara yake yanaonekana katika kila kona ya dunia, japokuwa ukweli
unabakia kuwa mchango wa kila taifa katika kuharibu hali ya mazingira
ya dunia si sawa na wachangiaji wakubwa wa uharibifu wanabaki kuwa
mataifa makubwa yaliyoendelea kiuchumi.
Makamu
wa Rais Dkt. Bilal aliungana na viongozi wa nchi mbalimbali wakiongozwa
na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma katika meza ya mjadala kuhusu dunia
tunayoitaka mjadala ambao pia ulimshirikisha Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa Ban Ki Moon na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Jean
Ping. Katika mjadala huu mataifa yaliyoshiriki yalikubaliana kwa kauli
moja kuwa, COP 17 itoke na maamuzi ambayo yatasawiri safari ya maamuzi
yaliyosainiwa katika Protokali ya Kyoto na sio kumaliza maamuzi ya
protokali hiyo.
“Nikiwatazama
wote mliopo hapa naona suluhisho la mabadiliko ya tabia nchi, naona
kuna kila sababu ya mkutano huu kutoa majibu ya siku zijazo na hivyo
kuondoa hofu inayokabili dunia kwa sasa na siku zijazo,’ alisema Rais
Zuma wakati akifungua kikao cha COP 19, CMP 7 ambacho kinahusisha utoaji
wa kauli za kila nchi mshiriki wa mkutano huo, zilizoanza kutolewa
jana.
Katika
mkutano huu Tanzania licha ya kuwa na ushiriki wa Makamu wa Rais ambaye
pia anasimamia Mazingira na Muungano, pia yupo Waziri katika Ofisi ya
Makamu wa Rais Mazingira Dkt. Terezya Huvisa ambaye
amekuwepo hapa kufatilia vikao katika ngazi ya mawaziri akiwa na
wataalamu wake sambamba na Mkurugenzi wa Mazingira Dkt. Julius Ningu.
Pia yupo Waziri wa SMZ katika Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Fatma
Fereji na wataalamu wengine katika eneo hili la mazingira pamoja na
asasi za kiraia kutoka Tanzania.
Mkutano
wa COP 17, unakabiliana na ugumu kufuatia nchi tajiri hasa Marekani,
Japan na Umoja wa Ulaya kutoonyesha kukubaliana kwa haraka kuhusu
kusaini Protokali ya Kyoto. Mataifa haya ndiyo yaliyonufaika na
yanayonufaika na uchangiaji wa gesi zinazoharibu hali ya hewa duniani,
jambo linalofanya mataifa maskini sasa kukabiliana na changamoto kubwa
kama ile ya mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha ukame na mafuriko
na kuhatarisha maisha ya wananchi wengi duniani. Nchi za Afrika
zinahitaji mataifa makubwa kulipa kutokana na madhira waliyosababisha na
kilio hiki kinaonekana bado kinachukua muda mrefu kupatiwa jibu, kwa
kuwa nchi tajiri sasa hivi nazo zinajitetea kutokana na kukabiliana na
mporomoko wa uchumi katika nchi zao.
Mkutano
huu ni wa kwanza kufanyika Afrika na unaonyesha namna bara hili
linavyokua kwa kasi huku likiwa na watu walio tayari kutafuta mabadiliko
licha ya kuwa nchi nyingi katika bara hili bado zinakabiliwa na
umaskini unatokana na sababu nyingi na kubwa zikiwa hizi za
kusababishiwa umaskini na mataifa nje, ambayo yamegeuza nchi za Afrika
kuwa sehemu za kutupia taka ambazo huangamiza mazingira.
Imetolewa na: Idara ya Habari Ofisi ya Makamu wa Rais
Durban, Desemba 07, 2011





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)