Na Nova Kambota Mwanaharakati,
Nianze makala yangu kwa kutamka wazi kuwa sikubaliani
na kauli mbiu ya miaka hamsini ya uhuru wa Tanzania bara ‘’tumeweza, tumethubutu, tunasonga mbele’’ sikubaliani na dhana hii na kamwe sitakubaliana nayo
kwasababu kila Mtanzania anayejua ukweli tena ni mzalendo anatambua wazi jinsi
taifa letu linavyorudi nyuma kwa kasi ya ajabu ndani ya miaka hii hamsini, sasa
watu wanahoji tumethubutu nini? Kama sio porojo hizi?
Baada ya utangulizi
huo sasa nije kwenye hili nalotaka kulizungumzia leo, hili ni maalumu kwa rais
wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mh Jakaya Kikwete , sina uhakika ni mara
ngapi huwa anasoma makala zangu lakini nachoamini kuwa kila anapopata nafasi
hiyo huwa anapitia maandiko yangu hivyo naandika makala hii nikiwa na imani
kuwa ataisoma kama si yeye basi wapambe wake wataipitia.
Baada ya
kumalizika kwa kikao cha CCM huko Dodoma naona watanzania wamerejea katika
majukumu yao ya kila siku na maisha yanataka kulazimishwa kuendelea kama
kawaida huku akili za kawaida zikitushawishi pasi na shaka kuwa hali haipo
kawaida hasa kwa upande wa rais wetu Kikwete
kutokana nayeye kutajwa kwenye kashfa ya Richmond.
Nisingependa
kurudia kile ambacho tayari kimeshazungumzwa na waandishi wengine juu ya
alichofanya Lowassa kwa kumtaja waziwazi rais Kikwete na uhusika wake ndani ya
kashfa hiyo ya kampuni hewa ya ufuaji umeme ya Richmond ambayo hakuna ubishi
kuwa itachukua karne nyingi mpaka mzimu wa kampuni hii ufutike kabisa kwenye
akili za watanzania.
Tuhuma dhidi
ya Kikwete zimekuwepo kwa muda mrefu lakini tofauti na sasa ambapo alichofanya
Lowassa si tu kumtuhumu Kikwete bali kumtaka akumbuke kile ambacho kinaweza
kutafsiriwa ni ‘’UCHAFU WAKE’’. Tuhuma za Lowassa zimesemwa ndani ya kikao cha
CCM tena mbele ya Kikwete mwenyewe ambaye angeweza kuzijibu au la, lakini kwa
hiyari yake amekaa kimya, je hii
inatafsiri gani? Lowassa amesema ukweli? Kikwete anamwogopa Lowassa? au
tusubiri vita kati ya maswahiba hawa wawili? ambao kadri muda unavyoenda dalili
zinaonyesha watazidi kuraruana na mwishowe watatangaza kuwa ‘’WALIKUTANA TU
BARARANI’’ tofauti na awali ambapo walijifanya ni marafiki wa kweli.
Juhudi zozote za CCM, Ikulu au Kikwete mwenyewe
kutosema wazi ushiriki wa Kikwete katika
sakata hilo haziwezi kutufanya watanzania tuamini kuwa ‘’Kikwete hahusiki’’
huku tunajua wazi ni kwa kiasi gani Lowassa anamfahamu Kikwete kwa undani?.
Wimbo ni huu kama kuna ‘’mpuuzi’’ anayedhani jalada la Richmond limefungwa basi
ajue anajidanganya, sisi watanzania hatuwezi kukubali kumaliza mjadala mpaka
pale uchunguzi wa kina utakapofanyika dhidi ya mtuhumiwa mpya kwenye sakata
hilo ambaye ni rais Kikwete. Naam! Kikwete yakupasa utambue kuwa watanzania
hatuwezi kukubali sakata la Richmond liishe kirahisi hivi , tunataka
‘’UCHUNGUZI HURU NA WAHAKI.
A luta Continua!
Nova Kambota,
+255717 709618
novakambota@gmail.com
www.novakambota.com
Tanzania, East Africa
Monday 5, December 2011.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)