Taarifa Rasmi Ya Jeshi La Polisi Nchini Juu Ya Katazo la Maandamano Tanzania - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Taarifa Rasmi Ya Jeshi La Polisi Nchini Juu Ya Katazo la Maandamano Tanzania


 Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Inspekta Jenerali Wa Polisi Said Mwema
--
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA

Anuani ya Simu “ MKUUPOLISI” 
Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi,
Simu : (022) 2110734 Makao Makuu ya Polisi,
Fax Na. (022) 2135556 S.L.P. 9141,
Unapojibu tafadhali taja: DAR ES SALAAM.

23/11/2011
TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KATAZO LA MAANDAMANO YALIYOKUWA YAMEPANGWA KUFANYIKA NCHI NZIMA TANZANIA BARA NA VISIWANI KUTOKA KWA MAKUNDI MBALIMBALI

Ndugu Wanahabari,

Kutokana na mchakato unaoendelea wa kupitishwa kwa muswaada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba Mpya hapa nchini, Jeshi la Polisi Tanzania limekuwa likipokea maombi kutoka taasisi mbalimbali ya kufanya maandamano ya nchi nzima. Maombi hayo yamekuwa na malengo tofauti tofauti yakiwemo ya kupinga muswaada huo na mengine kuunga mkono jambo ambalo linaashiria kuleta migongano na hatimae uvunjifu wa amani. Baadhi ya taasisi zilizowasilisha maombi hayo ni pamoja na; JUKWAA LA KATIBA TANZANIA lengo lao likiwa ni kutaka kuandamana nchi nzima kupinga Muswaada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya uliopitishwa na Bunge bila ushiriki wa wananchi wote wa Tanzania. Taasisi nyingine ni TAASISI YA UMOJA WA VIJANA CCM ambao waliomba kufanya Maandamano Nchi nzima, wakiwa na Lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu upotoshaji mkubwa unaofanywa na vyama vya siasa na washirika wao katika kuhakikisha Amani ya Nchi inapotea kwa kupitia mwamvuli wa mchakato wa Katiba mpya.

Pamoja na maombi hayo, pia, Jeshi la Polisi limepokea maombi ya UMOJA WA WANAWAKE TANZANIA CCM ambao lengo lao ni kufanya maandamano tarehe 26/11/2011 katika Wilaya na Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 11.00 jioni kwa lengo la kuipongeza Hotuba ya Mhe. Rais aliyoitoa tarehe 18/11/2011, na maombi kutoka TAYC YOUTH CAMP wakipinga mwenendo wa mchakato wa kudai muswaada wa Katiba kwamba hauendani na utaratibu na utamaduni wa mtanzania.

Kutokana na mwingiliano wa maombi hayo ya kila taasisi kutaka kuwasilisha mawazo ama hoja zake kwa njia ya maandamano Jeshi la Polisi limeona kuwa, kuna kila dalili za kuwepo kwa uvunjifu wa amani. Na kwa sababu hizo, Jeshi la Polisi Tanzania limesitisha maandamano yote na kuwashauri wahusika kutumia njia mbadala badala ya kufanya maandamano kama walivyopanga jambo ambalo litasaidia kudumisha amani na utulivu hapa nchini.

Uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi Tanzania umezungumza na taasisi zote zilizowasilisha maombi katika kikao cha pamoja kilichofanyika Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam leo tarehe 23/11/2011 na kwa pamoja taasisi zote zimekubali kwamba hoja zilizotolewa na Jeshi la Polisi ni za msingi na hivyo kuridhia kusitisha maandamano na kuahidi kwamba watatumia fursa zingine zitakazojitokeza katika kuwasilisha mawazo yao ambazo hazitakuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.

Ifahamike wazi kwamba Jeshi la Polisi halina nia mbaya ya kuzuia mikusanyiko au maandamano. Hata hivyo, katika utekelezaji wa sheria na kanuni zilizopo, pale Jeshi la Polisi linapopata taarifa ya mkusanyiko au maandamano hulazimika kuzingatia mambo mengine muhimu kabla ya kuruhusu mkusanyiko ama maandamano kama vile: migongano inayoweza kusababisha vurugu au fujo, haki ya raia wengine ambao hawatahusika na mikusanyiko au maandamano hayo, njia ya kupita, mahali pa mkutano au maandamano ili kuwasaidia watu wengine kuendelea na shughuli nyingine za kujiletea maendeleo.

AHSANTENI SANA.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA INSPEKTA JENERALI WA POLISI POLISI MAKAO MAKUU
DAR ES SALAAM.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages