Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wananchi wa Tumbatu
alipofanya ziara ya kichama ya siku moja katika kisiwa hicho jana
19/11/2011.
Maalim Seif akiwa ndani ya boti ndogo kuelekea kisiwa cha Tumbatu kwa ziara ya siku moja ya kichama tarehe 19/11/2011
Maalim Seif akisalimiana na wazee wa Tumbatu alipofika kisiwani humo kwa ziara ya kichama ya siku moja
--
Katibu
mkuu wa Chama cha Wananchi CUF amesema cha chake hakiwezi kukubali
kuona baadhi ya wazanzibari wanaendelea kunyimwa haki yao ya kupatiwa
vitambulisho vya uzanzibari ukaazi.
Amesema
kuwanyima vitambulisho hivyo ni kuwanyima haki yao ya kisheria, jambo
ambalo linakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu, jambo ambalo
haliwezi kuvumiliwa na chama chake.
Maalim
Seif ambaye pia ni makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa indhari
hiyo katika kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja alipofanya
ziara ya siku moja kisiwani humo kuangalia uhai na maendeleo ya chama
hicho.
“Hatuwezi
kukubali nchi ikaendeshwa katika njia za ubaguzi namna hii, tumefikia
maridhiano ili kusudi kila mwananchi apatiwe haki zake za kisheria,
iweje leo wengine wapewe, wengine wanyimwe haki hizo”, alifoka Maalim
Seif akibainisha kuwepo kwa baadhi ya vijana kutoka Tanzania bara ambao
hupewa vitambulisho huku Wazanzibari wengine wenye sifa wakinyimwa.
“Naiambia
serikali yangu, namwambia rais wangu kwamba kwa hili hatukubali hata
siku moja, na nawambia wananchi kuwa hili nimelivalia njuga”, aliongeza
kiongozi huyo wa CUF.
Amesema
licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuundwa kwa serikali
ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ikiwa ni
pamoja na kusimamia amani na utulivu uliopo nchi, lakini changamoto
iliyopo kwa sasa ni kwa baadhi ya watendaji kutotekeleza majukumu yao
ipasavyo kwa wananchi wakiweka mbele itikadi za vyama vyao.
“Bado
wapo watendaji hasa katika ngazi ya shehia wanawahudumia wananchi kwa
itikadi za vyama, nakwambieni masheha hivyo sivyo, na tukayembaini
akifanya hivyo tutamchukulia hatua za kisheria.
Akielezea
umuhimu wa vitambulisho hivyo Maalim Seif alisema baadhi ya watu
wanalichukulia suala hili kisiasa zaidi lakini suala hilo lina umuhimu
katika nyanja zote za maisha ya wazanzibari.
“Mbali
na vitambulisho hivyo kutumika zaidi kwa ajili ya kura lakini kama
huna Zan ID huwezi kupata ajira, huwezi kuendelea na elimu ya juu na
kama polisi wanafuata sheria basi wanao uwezo kisheria wa kukusimamisha
njiani na kukuomba kitambulisho, ikiwa huna inakuwa kosa la jinai”,
alifahamisha.
Maalim
Seif aliongeza kuwa wakati Taifa linajiandaa kuchukua maoni ya
wananchi juu ya Katiba mpya wanayoitaka, kila Mzanzibari lazima awe na
kitambulisho cha Ukaazi, ili aweze kushiriki kikamilifu na kulinda
maslahi ya Zanzibar.
Amesema
wakati wa kutoa maoni hayo juu ya mfumo wa Muungano wananchi wa
Tanzania Bara na Wazanzibari kila upande utatakiwa kutoa maoni yao,
ambapo kwa Zanzibar kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kitakuwa kigezo
cha kumjua Mzanzibari na hatimaye kuweza kushiriki katika kura ya
maoni.
Akizungumzia
nyanja za maendeleo, Makamu wa kwanza wa Rais alisema serikali
inakusudia kuziendeleza sekta za uvuvi na kilimo ili ziweze kuleta tija
kwa wananchi na kuongeza kipato chao, sambamba na kuongeza nafasi za
ajira kwa wananchi.
Alisema
viwanda vya usindikaji wa matunda na mazao ya baharini vitajengwa
ambapo viwanda vya aina hiyo na vyengine vitachangia kutoa ajira kwa
vijana.
“Ni
matumaini yangu kuwa kutokana na mipango imara ya serikali ya umoja wa
kitaifa, katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, zaidi ya nusu ya
vijana wa Zanzibara watakuwa tayari wamepata ajira za kuendesha maisha
yao”, alisema.
Aidha
alisema serikali inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni ya ununuzi
wa mwani ili kuangalia uwezekano wa kuongeza bei kufikia angalau
shilingi 1000 kwa kilo, sambamba na kuwawezesha wavuvi ili waweze kuvua
katika bahari kuu.
Hassan Hamad
Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)