Wasimamizi wa sensa ya majaribio ya watu na
makazi 2011 kutoka Ofisi ya Takwimu Pemba wakifuatilia maendeleo ya
zoezi la ujazaji wa madodoso ya sensa katika maeneo mbalimbali
wilayani Michweni Pemba wakiongozwa na Msimamizi mkuu wa zoezi hilo na
Mkuu wa Ofisi ya Takwimu Pemba Bw. Haroub Ally Masoud (kulia).
Bibi Raya
Ally Hamad mkazi wa eneo la Sizini wilayani Micheweni, Pemba akiwa na
familia yake akitoa ushirikiano kwa kujibu maswali aliyoulizwa na
mdadisi/karani wa sensa ya majaribio ya watu na makazi ya mwaka 2011
Bi. Time Juma Hamad (kushoto).
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Micheweni, Pemba.
Zoezi la Sensa ya Majaribio ya Watu na Makazi 2011
linalofanyika katika wilaya ya Micheweni,Pemba limeonyesha mafanikio
makubwa baada ya wananchi kujitokeza na kushiriki kikamilifu kutoa
taarifa mbalimbali zinazowahusu katika maeneo yao.
Msimamizi mkuu wa zoezi hilo ambaye pia ni Mkuu wa
Ofisi ya Takwimu Pemba Bw. Haroub Ally Masoud amesema hayo leo mara
baada ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyochaguliwa kwa ajili ya zoezi
hilo wilayani humo.
Amesema maandalizi mazuri yaliyofanywa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu yamelifanya zoezi hilo kufanyika kwa ufanisi mkubwa. “
Zoezi la sensa linaendelea vizuri, mpaka sasa hakuna kwikwazo ambacho
tumekipata kutokana na mwitikio wa wananchi na ushiriki
wao tunaoupata kutokana na elimu tuliyoitoa juu ya umuhimu wa sensa na
upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya maendeleo ya taifa”
Ameeleza kuwa serikali imeyachagua maeneo ya Sizini
na Maziwang’ombe yaliyoko wilayani Micheweni kwa Pemba nzima kuwa
maeneo ya majaribio kutokana na utaratibu maalum wa kitaalam uliotumiwa
katika utafutaji wa takwimu kwa ajili ya mipango ya maendeleo.
Bw. Masoud amefafanua kuwa zoezi la utafutaji wa
takwimu katika maeneo yaliyoainishwa linaendeshwa kwa
ushirikiano kati ya karani na mtoa taarifa katika familia ambaye ni
baba au mama na kuongeza kuwa maswali yanayoulizwa ni yale ya kawaida
ambayo yanajibika kirahisi yakiwemo masuala yanayohusu uraia, shughuli
za kiuchumi, vifo, hali ya nyumba zao na vifaa vilivyotumika kujengea
nyumba hizo na upatikanaji wa huduma za jamii katika kaya husika.
Akifafanua kuhusu madhumuni ya sensa
ya majaribio 2011 inayofanyika katika mikoa ya Arusha,Dar es
Salaam,Kaskazini Pemba,Kigoma, Kilimanjaro, Manyara,Mara, Mjini
Magharibi, Mtwara, Njombe na Pwani na kuzihusisha kaya
5000 inalenga kupima na kutathmini maandalizi ya sensa ya watu na makazi
ya mwaka 2012.
“Madhumuni ya sensa hii ya majaribio pamoja na mambo
mengine ni kupima usahihi wa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali
zitakazotumika yakiwemo madodoso ,niongozo na fomu mbalimbali ”
Amesema.
Aidha amebainisha kuwa utaratibu wa
kuhesabu watu unaotumika katika sensa ya majaribio ndio huo huo
utakaotumika katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika nchi nzima
mwezi Agosti mwaka 2012.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa zoezi hilo
ambaye familia yake ilishiriki zoezi hilo la majaribio Bi.Halima
Komboisa amefurahia zoezi hilo na kueleza kuwa litatoa
takwimu halisi juu ya maisha ya mtanzania.
“Natoa wito kwa watanzania wenzangu kushiriki
kikamilifu katika zoezi hili la sensa ya majaribio ya watuna makazi
kwani ni zoezi zuri,rahisi halina matatizo kwa upande wangu nimelipokea
vizuri “ Amesisitiza Bi. Halima.
Naye diwani wa Wadi
Bw.Ahmed Ally Mwinyi ameishukuru serikali kwa kuichagua wilaya ya
Micheweni kushiriki zoezi hilo huku akisisitiza kuwa yeye kama kiongozi
wa jamii kwa kushirikiana na viongozi wengine waliwaelimisha wananchi
juu ya umuhimu na faida ya kuhesabiwa licha ya kuwepo changamoto chache
walizokutana nazo wakati wa zoezi la uelimishaji.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)