Naibu Waziri wa Viwanda
na Biashara Mh Lazaro Nyalandu( Wa Sita Kulia)akizungumza na wafanyakazi wa
Mamlaka mbali mbali za serikali katika vituo vya mipakani
---
Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Lazaro Nyalandu, awetaka wafanyakazi
wa Mamlaka mbali mbali za serikali katika vituo vya mipakani
kuhakikisha kuwa, hakuna biashara yoyote ya magendo inayopenya katika
mipaka hiyo.
Akizungumza na watendaji wa Mamlaka hizo katika ziara
yake ya kukagua masoko na vituo vya biashara mipakani katika Eneo la
Horohoro ambalo ni mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Mkoani Tanga, Mh
Nyalandu amesema, biashara za magendo zinainyima serikali mapato
mengi na kuneemesha watu wachache hali ambayo haikubaliki na lazima
ikomeshwe mara moja.
“Serikali
imepiga marufuku uvushaji wa sukari kwenda sehemu yoyote nje ya
nchi, serikali pia imepiga marufuku uingizaji wa bidhaa zozote
hafifu, mifuko ya plastiki, silaha na dawa za kulevya,
ndio maana Mamlaka zote za udhibiti zipo katika vituo vyote vya
mipakani, ninawakumbusha wajibu wenu na kuwasihi muwe wazalendo,
muipiganie nchi yenu kwa kuhakikisha kuwa wadau wenu wote
wanazingatia sheria.”
Kwa upande
wake Mkuu wa kituo cha forodha cha Horohoro Bw Paul Kamukulu,
amemuomba Naibu Waziri kusaidia kutatua kero zinazowakwaza watendaji
wa serikali katika mpaka huo hali inayofanya utendaji wao wa kazi kuwa
mgumu.
“Mh Waziri hali ya maisha katika eneo hili ni ngumu
sana, hatuna vifaa vya kutosha kufanya kazi zetu, eneo hili halina
maji, tunanunua dumu moja la maji kwa shilingi mia nane, maji
yanatoka Kenya, hatuna uhakika na usalama wake, nyumba za wafanyakazi
ni chache. Pamoja na yote hayo, bado tunajitahidi kwa uwezo wetu
wote na kuikusanyia nchi wastani wa shilingi bilion i mbili kwa
mwaka, tunaomba tusaidiwe”.
Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Nyalandu ameahidi
kufikisha kilio hicho kwa mamlaka husika ili kwa pamoja zishirikiane
kutatua kero hizo na kuwawezesha watendaji hao kutimiza wajibu wao
kikamilifu.
Ziara ya Mh Nyalandu kutembelea masoko na vituo vya
biashara mipakani ilianzia katika Mpaka wa Tanzania na Kenya katika
Mji wa Namanga Mkoani Arusha, ikaendelea katika vituo vya Himo na
Holili Mkoani Kilimanjaro, na kituo cha Horohoro Mkoabni Tanga.
Pamoja na kukagua na kuhamasisha shughuli za
biashara katika masoko na vituo vya biashara mipakani, ziara hizi ni
mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Mh Mizengo Pinda
aliewataka viongozi na Mamlaka zote za ulinzi na Usalama nchini
kuhakikisha kuwa, sukari na bidhaa nyingine zozote zilipopigwa
marufuku kutoka na kuingia nchini hazivuki mipaka yetu.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)