WAZIRI MKUU AKEMEA VIONGOZI WASIOJALI SHIDA ZA WATANZANIA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

WAZIRI MKUU AKEMEA VIONGOZI WASIOJALI SHIDA ZA WATANZANIA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Mke wa Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanga, Frida Mdolwa katika sherehe za Kumweka wakfu Askofu wa Dayosisi hiyo, Maimbo WIlliam Mndolwa (katikati) zilizofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu cha Korogwe, Septemba 4, 2011.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglican nchini, Valentino Mkokiwa (kulia) katika Ibada ya kumweka wakfu Askofu Maimbo William Mdolwa (kushoto) wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Tanga iliyofanyia kweye viwanja vya Chuo cha Ualimui cha Korogwe, Septemba 4, 2011. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda amekemea viongozi wasiojali na kushughulikia kero za watu na umaskini unaowazunguka watu wanaowaongoza na akawataka viongozi wa madhehebu ya dini waisaidie Serikali katika kupambana na hali hiyo.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Septemba 4, 2011) wakati akitoa salamu za Serikali kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Maimbo Mndolwa wa Kanisa la Anglikana Tanzania iliyofanyika kwenye kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu Korogwe jirani na Kanisa la Mt. Mikaeli na Malaika Wote mjini Korogwe, Tanga.
Alisema viongozi wote wakiwemo Maaskofu, Wachungaji, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya kila mmoja hana budi kuumia kutokana na matatizo yanayowakabili Watanzania ili kurudisha imani ya wananchi.
“Tuna kazi kubwa ya kuwatoa Watanzania katika lindi la umaskini… kila mmoja adhamirie kujiondoa katika ubinafsi, mmezungumza suala la upendo. Katika hali ya kawaida, mtu huwezi kukosa upendo kwa jirani halafu ukadai kuwa wewe ni muadilifu…”, alisema.
Alisema kila mmoja anapaswa kuhakikisha anasimamia jambo hilo kwa sababu ni la Watanzania wote. “Tukiwa waadilifu ndipo nchi itakwenda kwa amani,” alisisitiza.
“Mtu akishapata nafasi ya uongozi ni rahisi sana kushawishika kuitumia vibaya nafasi aliyonayo kwa kujilimbikizia mali… kama hakuna uadilifu iko siku tutachapana viboko. Ni lazima dini zote tuendelee kusema lugha moja ya kusisitiza uadilifu,” alisema.
Alisema viongozi wa dini wanasikilizwa zaidi na jamii hivyo wana nafasi kubwa ya kutoa ushawishi ili waumini wao wasijihusishe na vitendo viovu na kwamba wana uwezo mkubwa wa kuisaidia serikali kupambana na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
“Ninawaomba tushirikiane kutokomeza maovu yanayoiandamana jamii, ninawaomba mtumie nafasi yenu katika jamii hasa ile ya kuponya kiroho kuwarudisha Watanzania wengi waliopotoka katika maadili mema…,” alisema.
Aliwaomba viongozi wa kanisa watumie fursa ya ufugaji nyuki kwa kuhimiza kila familia iwe na mizinga walau mitatu hadi mitano kwani ni njia ya uhakika ya kuleta kipato kwa wananchi wa kawaida.
“Kila mzinga mmoja unaweza kumpatia mkulima au mfugaji lita 10 katika miezi mitatu na kila lita moja ni sh. 10,000/-. Kwa hiyo ni sh. 100,000/- kwa kila mzinga. Tuhimize waumini wetu wafuge nyuki sababu Tanga mna uoto mzuri wa asili na maji yapo. Kwa njia hii tutawawezesha wananchi kumudu kulipa ada za watoto…,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages