Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Watanzania
wametakiwa kununua bidhaa zenye nembo ya rafiki wa tabaka la hewa ya
Ozoni (Ozone friendly) ili kuungana na mataifa mbalimbali duniani
kuhifadhi tabaka la hewa hiyo ambalo liko hatarini kutoweka angani kutokana na uchafuzi wa mazingira unaoendelea.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuelezea maadhimisho ya
Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni yatakayofanyika kitaifa
mwezi huu jijini Arusha, kaimu mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Ofisi
ya Makamu wa Rais Bw. Stephen Nkondokaya amesema kuwa Tanzania licha ya
kukabiliwa na changamoto mbalimbali inaendelea kupunguza ongezeko la
matumizi ya vifaa vinavyotoa hewa zinazoharibu tabaka la Ozoni angani .
Amesema hali iliyoanza kujitokeza ya kuruhusu kiasi kikubwa cha mionzi ya kikiukaurujuani kufika kwenye uso wa dunia inasabishwa na matumizi
ya kemikali hatari zikiwemo “Chlorofluorocarbons”,Halons na Carbon
tetrachlorides zinazotumika katika sehemu mbalimbali zikiwemo kwenye
majokofu, viyoyozi , vifaa vya kuzimia moto, shughuli za usafishaji
chuma, utengenezaji wa magodoro, kilimo cha tumbaku na maua pamoja na
zile za kuhifadhia nafaka katika maghala zimekuwa chanzo cha uharibifu
wa tabaka la Ozoni.
Bw.
Nkondokaya amefafanua kuwa hali ya kuongezeka kwa magonjwa ya kansa ya
ngozi , uharibifu wa macho unaosababisha upofu, upungufu wa kujikinga
na maradhi na kujikunja kwa ngozi kuathirika kwa maumbile na michakato
ya ukuaji kunasababishwa na ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya
tabia nchi.
Ameeleza
kuwa Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi 196 zilizoridhia mkataba wa
kimataifa wa Vienna na Itifaki ya Montreal mwaka 1993 inaendelea kuweka
mfumo wa udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa tabaka la hewa ya Ozoni
ikiwemo kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku na vifaa
vinavyotumia gesi hizo kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwisha
tumika na vinavyotumia vipoozi aina ya R 11 na R 12,kuepuka kutupa ovyo
majokofu ya zamani na vifaa vya kuzimia moto zinazoharibu tabaka la
Ozoni aina ya CFCs na halon.
Kuhusu maadhimisho ya Kimataifa ya Tabaka la Ozoni ambayo kitaifa yatakayofanyika jijini Arusha amesema yataongozwa na kauli mbiu ya “Uondoshaji
wa Matumizi ya gesi za “Hydrochrolofluorocarbons” (HCFC): Mchango
muhimu katika kulinda Tabaka la Ozoni na kuzuia Mabadiliko ya Tabianchi”
na kuambatana na zoezi la utoaji elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa
kulinda tabaka la Ozoni pamoja na kugawa mitambo ya kutambua gesi
zinazoharibu tabaka la hewa ya Ozoni kwa wadau wa usimamizi wa sheria ya mazingira nchini.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)