Meneja Uhusiano na Habari za Mtandao wa
Vodacom Tanzania Matina Nkurlu akizungumza na waandishi wa habari jana
katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusiana na udhamini
wa Vodacom wa milioni saba kwa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
na Burudani Tanzania(TASWA) kwa ajili ya udhamini wa semina kwa
wanachama wake, pembeni yake ni katibu mkuu wa Taswa Amiri Mhando na
katibu Mkuu wa TASWA, George John.
*******************************
|
MAFUNZO kwa ajili ya waandishi wa habari za michezo
yatafanyika mkoani Morogoro Oktoba 1 na 2 mwaka huu chini ya udhamini
wa Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania.
Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari
za Michezo Tanzania (TASWA), Amir Mhando, amesema leo wakati
akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa maandalizi ya
mafunzo hayo yanaenda vizuri na wana matumaini yatakuwa na manufaa
makubwa.
Aliishukuru
Vodacom Tanzania kwa udhamini wake na kusema ni hatua nzuri katika
kutekeleza mikakati ya TASWA kuendesha mafunzo kwa wanachama wake na
waandishi wa habari za michezo kwa ujumla chini ya kauli mbiu ya chama
hicho isemayo: TASWA Mafunzo Zaidi.
Alisema mafunzo hayo
yatahusisha washiriki 40 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na
Pwani na kuongeza kuwa mwanzoni mwa Novemba pia wataendesha mafunzo kama
hayo mkoani Arusha yakihusisha washiriki kutoka Tanga, Arusha,
Kilimanjaro, Manyra, pamoja na baadhi ya washiriki kutoka Dar es Salaan.
Alieleza mwishoni mwa
Novemba TASWA itaendesha pia mafunzo kwa wahariri wa habari za michezo,
ambayo yatakuwa nje ya Dar es Salaam na kwamba mkoa husika utatangazwa
baadaye.
Alielezea
kuwa mafunzo ya Morogoro na Arusha yatahusisha masuala ya maadili ya
uandishi wa habari,, masuala ya sheria za mambo ya habari na sheria za
michezo mbalimbali.
Alisema washiriki
wataelimishwa namna ya kuripoti habari za michezo ya mpira wa wavu,
kikapu na riadha na kwamba kama mambo yataenda vizuri pia utaingizwa na
mchezo wa ngumi.
Alieleza kuwa
wakufunzi katika mafunzo hayo ni baadhi ya walimu wa mambo ya habari,
wahariri wazoefu, wanasheria na pia wakufunzi wa michezo mbalimbali
nchini.
Kwa
upande wake Meneja Uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania,
Matina Nkurlu, alisema kampuni yake inajisikia fahari kubwa kudhamini
mafunzo hayo na kuwa itaendelea kufanya hivyo kadri watakavyoweza na
kuwa mafunzo ya Morogoro yatagharimu kiasi cha sh. Milioni saba.
“Vodacom
Tanzania inajisikia fahari kwa kudhamini mafunzo haya kwani hii siyo
mara ya kwanza kwa Vodacom kudhamini mafunzo ya aina hii, ambapo mwaka
jana tuliendesha mafunzo na wahariri wa habari za michezo.
“Mwaka huu tunadhamini
mafunzo ya TASWA yote haya tukiwa na lengo la kuboresha tasnia ya
habari, mafunzo ya Arusha pia tutadhamini, lakini bajeti yake
itaongezeka zaidi ya hii,” alisema Nkurlu.
Naye Katibu Msaidizi
wa TASWA, George John alisema katika mkutano huo kuwa, chama chake
kimeamua kuendesha mafunzo hayo kwa ajili ya kuwoangezea uelewa zaidi
waandishi wa habari za michezo.
“Mafunzo yatasaidia
sana kwani kwenye ripotingi yetu mfano mchezo wa mpira wavu huwa wengine
wanauliza wameshinda kwa mabao mangapi? Wakati kule huwa ni mambo ya
seti si mabao,” alisema John ambaye pia ni Katibu Msaidizi wa Chama cha
Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA).
|
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)