Mwanafunzi wa chuo kikuu
cha DIT kilichopo Dar es Salaam , Marehemu Dickson Nswila, ambaye
alikuwa akielekea kwenye mazoezi ya vitendo TAZARA, jijini Mbeya.
Mfanyabiashara wa mitumba, mji mdogo wa Mbalizi Marehemu Charles Mwakanyuma.
Marehemu Mariam Side mwenye umri wa miaka 31.
Taswira ya mbele ya Lori hilo lililosababisha hasara kumbwa.
Polisi
wakiangalia gari aina ya roli lenye namba IT.9518, lililopata ajali
baada ya kugongana na gari jingine na hivyo kupinduka na kusababisha
vifo vya watu watatu watembea kwa miguu na kuvunja nyumba
Gari lenye T.438 BRT aina ya Landover, mali ya mchungaji Nduka wa kanisa la Uinjilist Mbalizi. Ambalo liligongana na Lori hilo.
---
Na mwandishi wetu
AJALI
mbaya ya lori iliyotokea eneo la Tarafani mji mdogo wa Mbalizi,
imesababisha vifo vya watu watatu waliokuwa wakitembea pembezoni mwa
barabara ya Mbeya kwenda mji mdogo wa Tunduma, wilayani Mbozi.
Ajali
hiyo iliyotokea jana saa 2:30 asubuhi, ilihusisha lori hilo , lenye
namba IT.9518, lililokuwa likitokea mjini Dar es Salaam , kuelekea nchi
jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Kongo (DRC).
Muuguzi
wa hospitali Teule ya Ifisi, wilaya ya Mbeya vijijini, Rhoda Kasongwa,
alisema wamepokea miili ya marehemu watatu akiwemo mwanamke mmoja pamoja
na majeruhi mmoja ambaye ni dereva wa lori hilo .
Alisema
dereva huyo ambaye bado hajatambulika jina lake, wala makazi amepoteza
fahamu na anaendelea kupatiwa matibabu, akiwa chumba cha wagonjwa
mahuituti (ICU), hospitalini hapo.
Aliongeza
dereva wa roli, ambaye jina halijatambulika amepoteza fahamu na
amelazwa chumba cha wagonjwa mahututi na kuwa ameumia vibaya maeneo ya
kichwani pamoja na miguuni, hivyo jitihada zaidi zinafanyika ili kuokoa
maisha yake.
Aliwataja
marehemu kuwa ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha DIT kilichopo Dar es
Salaam , Dickson Nswila, ambaye alikuwa akielekea kwenye mazoezi ya
vitendo TAZARA, jijini Mbeya na mfanyabiashara wa mitumba, mji mdogo wa
Mbalizi Charles Mwakanyuma.
Kwa
mujibu wa Muuguzi huyo wa hospitali Teule ya Ifisi, mtu wa tatu
aliyefariki katika ajali hiyo ni Mariamu Said (31), mkazi wa mji mdogo
wa Mbalizi.
Watu
walioshuhudia ajali hiyo walisema lori hilo lililokuwa limepakia
shehena ya Chokaa, lilikuwa katika mwendo kasi, na kabla ya kuwagonga na
kisha kupinduka, liligonga gari T.438 BRT aina ya Landover, mali ya
mchungaji Nduka wa kanisa la Uinjilist Mbalizi.
Walisema
dereva wa Landlover alikimbizwa hospitali ya Ifisi na aliruhusiwa
kurudi nyumbani baada ya kutibiwa na kuonekana hali yake ni nzuri, kwani
alipata michubuko kidogo.
Waliongeza
kabla ya kuligonga Landrover, lori hilo lilikwepa basi lililokuwa
limewabeba wafanyakazi wa hospitali Teule ya Ifisi, ndipo liligonga gema
lililopo pembeni ya barabara, kupaa hewani kisha kwenda kuingia kwenye
karakana ya mafundi seremala, iliyopo eneo la Tarafani.
Wananchi
hao walisema polisi walifika eneo la tukio mapema, na hivyo kuweza
kunusuru wananchi wasiendelee kupakua shehena ya Chokaa, ambayo walikuwa
wakibeba mifuko na kutokomea nayo majumbani kwao.
Aidha,
mwanamke mmoja alijitolea kwa kivua kitenge chake, kumfunika dereva
aliyekuwa amepoteza fahamu na kisha kusaidia kumpakia kwenye gari ili
kumuwahisha hospitalini.
Aidha,
kabla ya polisi hawajafika eneo la tukio, baadhi ya watu wasiofahamika
walifanikiwa kufungua tenki la mafuta la lori hilo na kisha kutokomea
nalo.
Baadhi
ya wananchi walisema wanasikitishwa na kitendo cha baadhi ya watu
waliowahi kufika eneo la tukio, kuanza kugombania mifuko ya Chokaa,
badala ya kusaidia kuwaokoa majeruhi na kuondoa miili ya marehemu.
Miili ya marehemu wote watatu imehifadhiwa hospitali Teule ya Ifisi, iliyopo wilaya ya Mbeya vijijini.
Kaimu
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Anaclet Malindisa, alipotafutwa kwa
simu yake ya mkononi, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwa
polisi wanaendelea na uchunguzi.
Mwisho
*Habario hiii imeletwa Hapa na Latest News





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)