SIKU LIYUMBA ALIPOACHIWA HURU - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

SIKU LIYUMBA ALIPOACHIWA HURU


Gari ikitoka kumpokea liyumba 
Hapa akiingia nyumbani kwakemtoto wa Liyumba akiongea na dreva tax

NA MWANDISHI WETU
Hatimaye aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Amatus Liyumba, amemaliza kifungo chake cha miaka miwili gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma na Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini Dar es Salaam.

Liyumba ambaye alihukumiwa kifungo hicho Jumatatu ya Mei 24, 2010 amekaa gerezani kwa mwaka mmoja na miezi minne baada ya kuachiwa huru Ijumaa iliyopita saa 3:00 asubuhi.


Mara baada ya kutoka katika Gereza la Ukonga, Dar, Liyumba aliingia katika gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 366 BUH na moja kwa moja alielekea nyumbani kwake Kawe bila ya makeke yoyote.


The Biggest IQ Paper, Ijumaa Wikienda lilipata fursa ya kupenya hadi ndani ya nyumba hiyo na kujaribu kumdodosa Liyumba maisha yake ya gerezani.


Awali, mkurugenzi huyo mstaafu wa Benki Kuu, hakutaka kuzungumza kuhusu kesi na hukumu yake na kuwataka waandishi wetu kwenda kwa mawakili wake ili kupata ufafanuzi wa maswali yake.


DODOSO ZA MAISHA YAKE GEREZANI

Hata hivyo, katika kudodosa maisha yake ya gerezani, Liyumba alisema hawezi kusahau aliyokutana nayo humo kwani hayazoeleki.
Alisema kuwa si aina ya maisha ambayo aliyazoea na katu hakutegemea kama siku moja angeingia garezani ukizingatia kwamba siku zote alikuwa ni mtu wa kufanyakazi za ofisini.

Alisema wafungwa wanafanya kazi tofauti kama za shambani na viwanda vidogovidogo na siku za Jumapili huwa wanacheza mpira.


“Wakiwa wanacheza mpira unaweza kudhani labda wana furaha sana, lakini wapi? Jamani gerezani si sehemu ya mchezo, nyinyi hamjawahi kufungwa eeeh? Msiombee yawakute. Niulizeni mimi,” alisema huku akicheka.


Liyumba aliwataka watu kuwa makini na maisha yao ya kila siku ili wasivunje sheria na kujikuta wakilazimika kuingia gerezani.

“Kuna wafungwa wengine wamenishangaza sana, utakuta mtu anaachiwa huru lakini baada ya miezi mitatu anarudi tena, nadhani wamezoea maisha ya kule. Kwa kweli ni magumu sana,” alisema.

KUTAFUNWA NA MBU NI KAWAIDA

Alisema kuwa ndani ya gereza kuna sehemu tofauti za wafungwa kukaa na kuendesha maisha yao, pamoja na yeye kuishi katika chumba ambacho kilikuwa kikijitegemea kwa kila kitu ‘self contained’ lakini alikuwa akisumbuliwa na mbu.

“Chumba kilikuwa hakina madirisha, ni nondo tu ambazo zinapitisha mbu na kusumbua sana,” aliongeza.


HAWEZI KUSAHAU MABOMU YA GONGO LA MBOTO

Liyumba alisema katika siku ngumu anazozikumbuka alipokuwa gerezani ni ile yalipolipuka mabomu ya Gongo la Mboto.

“Cha kushangaza, tulisikia watu wakitangaziwa kwamba waondoke maeneo ya Ukonga na Gongo la Mboto na kwenda Uwanja wa Taifa, lakini sisi ndiyo kwanza tulikuwa tukiongezewa ulinzi, mlangoni kulikuwa na kufuli kubwa lenye usawa wa kiganja cha mkono cha mtu mzima.


“Tulishuhudia mabomu yakipita juu ya gereza lakini askari magereza walikuwa wakituambia kuwa kama kufa tutafia mlemle na katu haturuhusiwi kutoka nje,” alisema.


Katika hukumu ya kesi yake, Liyumba alikuwa akitetewa na Mawakili, Majura Magafu, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo.


Hukumu yake ilitolewa na jopo la mahakimu wakazi watatu wakiongozwa na Edson Mkasimongwa ambaye alimwachia huru mtuhumiwa na wengine Lameck Mlacha na Benedic Mwingwa waliomkuta na hatia.

Credit: Global Publisher Tanzania

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages