Na Mohammed Mhina
Serikali imesema inafanya mazungumzo na
muungano wa Shule za binafsi hapa nchini (TAMOSO) ili kuangalia upya
viwango vya ada vinavyotozwa kwa wazazi na walezi wenye watoto
wanaosoma katika shule za msingi na sekondari.
Akizungumza wakati wa mahafali ya saba ya
wahitimu wa elimu ya msingi kwenye shule ya St. Theresa Ukonga Jijini
Dar es Salaam, Afisa Elimu Mkuu, Idara ya Elimu ya Msingi nchini Bw.
Clarence Mwinuka, amesema hatua hiyo itasaidia kuweka uwiano sawa wa
viwango vya ada ili kuwapa unafuu wazazi na walezi wenye watoto
wanaosoma kwenye shule hizo.
Bw. Mwinuka alikuwa akizungumza kwa niaba ya
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini Mh. Philip Malugo,
wakati wa mahojiano maalum na Mwandishi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi
nchini ambaye pia ni Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Inspekta Mohammed Mhina.
Amesema kuwa kutokana na kutofautiana kwa
ada kati ya Shule moja na nyingine, Serikali inaendelea na mazungumzo
na muungano wa shule hizo ingawa amekiri kuwa shule za binafsi zimekuwa
msaada mkubwa kwa serikali katika kukuza kiwango cha elimu kwa
Watanzania.
Amesemesa pamoja na msaada huo, lakini bado
wananchi hasa wazazi na walezi hasa wale wa kipato cha chini
wameonekana kubeba mzigo mkubwa zaidi katika kuchangia elimu kwa watoto
waliopo kwenye shule hizo za binafsi hapa nchini.
Amesema majadiliano hayo
yatakapokamilika Serikali inaweza kuweka viwango sawa vya ada kwa shule
binafsi za msingi na za Sekondari ili kila mzazi aweze na fursa
na kupeleka motto wake katika shule anayoipenda.
Hata hivyo Bw. Mwinuka amesema kuwa
Serikali inaendelea na mikakati yake yakuziboresha shule zake za Msingi
na Sekondari kwa kukuza viwango vya taaluma ya walimu na kuboresha
mahitaji na miundombinu muhimu katika shule zake ili kusiwe na tofauti
ya elimu unayotolewa katika shule binafsi na zile za Serikali.
Awali Mkuu wa Shule hiyo Sr. Amelbberga
Rwezahura na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo Bw. Wilfred Kipondya,
walisema kuwa shule hiyo ina malengo ya kuhikia hatua ya juu ya utoaji
wa elimu ya msingi hapa nchini kwa kuboresha miundombinu na kuhakikisha
kuwa wanajenga mabweni kwa watoto wote ili kuondoa gharama za nauli na
usumbufu kwa watoto kusafiri masafa marefu kwa madaladala.
Shule ya St. Theresa iliyoanza na idadi ya
wanafunzi 20 wa darasa la awali, mwaka 1998 imefikia hatua hiyo baada
ya mawazo na fikra za aliyekuwa Mwalimu Mkuu mwanzilishi Sr. Pepetua
Mhana, za kuindeleza shule hiyo.
Sr. Mhana ndiye aliyeanzisha ujenzi wa
jengo la shule hiyo yenye ghorofa mbili ambazo zinavyumba vya madarasa,
ofisi za walimu na vyumba vya maabara ya sayansi.
Hivi sasa shule hiyo ina watoto 638 na
imekuwa ikifaulisha kwa aslimia 100 ya watoto wote wanaosoma na kufanya
mitihani ya kuingia darasa la nne na kidato cha kwanza.
Naye mmoja wa wanafunzi wanaohitimu mwaka
huu darasa la saba shuleni hapo, Batuli Mhina, amesema matarajio yake
atakapokuwa Sekondari atasoma kwa bidii hadi kufikia elimu ya chuo
kikuu na lengo lake kubwa ni kuja kuwa Mwandhishi wa Habari.
Amesema anatamani sana kazi ya uandishi wa
habari ili aje aielimishe jamii na kuwa sauti ya watoto wanaoishi
mitaani kwa maisha ya kuombaomba ili nao waweze kupatiwa elimu na
wajipangie malengo yao maishani.
Amesema kama
wanawake wakiwezeshwa wanaweza ni vipi watoto hasa wanaoishi mitaani
nao wasiwezeshwe ili waweze kupata elimu bora? Kwani amesema watoto ni
Taifa la leo na wazazi wa kesho na hivyo kama mama zao wanawezeshwa nao
bila kuwawezesha hawatajiweza.Habari Kwa Hisani Ya Full Shangwe Blogu
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)