RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya Wakuu wa Mikoa
nchini.
Katika mabadiliko hayo, amewateua Wakuu wa Mikoa wapya 15,
kuwabadilisha vituo vya kazi Wakuu wa Mikoa watano na wengine saba
wamestaafu kwa mujibu wa taratibu. Mkuu wa Mkoa wa Singida amebaki
kwenye kituo chake cha kazi wakati Wakuu wa Mikoa wengine wanne
watapangiwa kazi nyingine.
Aidha, Wakuu wa Mikoa mipya minne ya
Simiyu, Geita, Katavi na Njombe itakayoundwa baada ya taratibu
kukamilika watatangazwa baadaye.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, Wakuu wa
Wilaya 11 wamepandishwa Vyeo na kuwa Wakuu wa Mikoa kama ifuatavyo: Bw.
John Gabriel Tupa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara; Bw. Saidi Thabit
Mwambungu (Ruvuma); Bi. Chiku S. Gallawa (Tanga); Bw. Leonidas T. Gama
(Kilimanjaro); Dk. Rehema Nchimbi (Dodoma); Bw. Elaston Mbwillo
(Manyara); Kanali Fabian Massawe (Kagera); na Bibi. Fatma Abubakar
Mwassa (Tabora). Wakuu wa Wilaya wengine walioteuliwa ni Bw. Ali Nassoro
Rufunga, (Lindi); Eng. Ernest Welle Ndikillo, (Mwanza); na Bw. Magesa
Stanslaus Mulongo Mkuu wa Mkoa (Arusha).
Walioteuliwa nje ya
nafasi hizo ni Eng. Stella Manyanya (Rukwa); Bibi Mwantumu Mahiza,
(Pwani); Bw. Joel Nkaya Bendera (Morogoro) na Bw. Ludovick Mwananzila
(Shinyanga).
Waliobadilishwa vituo vya kazi ni Bw. Abbas Kandoro anayekwenda Mbeya
akitokea Mwanza; Bw. Said Mecki Sadiki anayekwenda Dar es Salaam
akitokea Lindi; Bibi Christine Ishengoma anayekwenda Iringa akitokea
Ruvuma; Lt. Kanali Issa Machibya anayekwenda
Kigoma akitokea Morogoro; na Kanali Joseph Simbakalia anayekwenda
Mtwara akitokea Kigoma. Dk. Parseko Ole Kone ataendelea kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Singida.
Waliostaafu ni Bw. Mohammed Babu, aliyekuwa Mkuu wa
Mkoa wa Kagera; Bw. Isidore Shirima aliyekuwa Arusha; Kanali (mst.)
Anatory Tarimo aliyekuwa Mtwara; Bw. John Mwakipesile, aliyekuwa Mbeya.
Wengine ni Kanali Enos Mfuru aliyekuwa Mara; Brig. Jen. Dk. Johanes
Balele aliyekuwa Shinyanga; na Meja Jen. Mst. Said S. Kalembo aliyekuwa
Tanga.
Wakuu wa Mikoa wanne waliostaafu ambao watapangiwa
vituo vingine vya kazi ni Bibi Amina Mrisho aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Pwani; Dk. James Msekela aliyekuwa Dodoma; Bw. Abeid Mwinyimusa
aliyekuwa Tabora na Bw. Daniel Ole Njoolay aliyekuwa Rukwa.
Wakuu
wote wa Mikoa waliopo sasa wameagizwa kuandaa Hati za Makabidhiano (Handing
Over Notes) katika muda wa siku 14 kuanzia siku ya kuapishwa kwa
Wakuu wapya wa Mikoa. Aidha Wakuu wa Wilaya ambao wamepandishwa vyeo
kuwa Wakuu wa Mikoa nao wanapaswa kufanya hivyo hivyo kwa ajili ya Wakuu
wa Wilaya watakaopangiwa vituo vitakavyokuwa vimeachwa wazi kutokana na
uteuzi wao.
Wakuu wa Mikoa ile minne mipya na Wakuu wa Wilaya
watakaoteuliwa hapo baadaye nao watatakiwa kuandaa Hati za Makabidhiano
ndani ya siku 14 tangu kuapishwa.
Makabidhiano
hayo lazima yahusishe pia kutembelea kwa pamoja baadhi ya maeneo na
miradi ambayo ni muhimu kama sehemu ya makabidhiano yao. Wakuu wote wa Mikoa walioteuliwa na Wakuu wa Mikoa
minne mipya wakaoteuliwa pamoja na Wakuu wote wa Wilaya
watakaoteuliwa baada ya zoezi kukamilika watatakiwa kuhudhuria mafunzo
ya wiki tatu kwenye Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma kwa lengo
la kuwajengea uwezo zaidi wa kiuongozi na kiutendaji.
Wakuu hao
wapya wa mikoa wataapishwa siku ya Ijumaa, Septemba 16, 2011 saa 4.00
asubuhi kwenye viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)