Na Nova Kambota,
Namkumbuka
mwanamuziki wa kizazi kipya Seleman Msindi maarufu kama Afande sele na
kile kibao chake cha “Darubini kali” anapohoji “kama unapenda pepo kwanini uogope kifo?”
Tungo
hii kwa namna ya pekee inamgusa waziri mkuu wa Tanzania Mh Mizengo
Pinda maarufu kama “mtoto wa mkulima” ndiyo namuuliza Pinda ataonaje
pepo pasipo kufa kwanza?
Tangu
kuteuliwa kwake mara baada ya Edward Lowassa kujiuzulu, Kwa wale
wanaomjua Pinda walishasema kuwa “Pinda atapwaya sana”, sasa ikiwa ni
takribani miaka mitatu na nusu tayari mambo hadharani kuwa Pinda
“kashindwa kazi”
Kwa
wasiomjua Mizengo Pinda tafuteni ukweli mtamjua tu, ni Mizengo Pinda
huyu amebaki kuwa mshauri wa Kikwete badala ya waziri mkuu kufikia hatua
ya kutamka bungeni kuwa hana mamlaka, ni Pinda huyu asiye na makundi
lakini anakubali kumezwa na mitandao na makundi ya CCM na bosi wake
Kikwete na sasa nimeanza kusikia watu wakimwita ni “mtoto wa mkulima anayeishi kibilionea”
Hakuna
ubishi kuwa hata watetezi wachache wa Pinda waliobaki sasa
wamefadhaishwa na udhaifu wake kama sio uwoga wa kupindukia, “jeuri” ya
Luhanjo na sakata la Jairo limemwaka njia panda Mizengo Pinda, amebaki
kujiumauma na kutapatapa tu, kadhalilishwa lakini hataki kuchukua hatua,
katukanwa lakini anachekelea! Huyu ndiye Mizengo Pinda.
Waziri
mkuu Pinda akiongelea sakata la Jairo akajiapiza kuwa angekuwa na
mamlaka angemfukuza kazi Jairo kwa maana nyingine Pinda amekiri kuwa
Jairo anastahili adhabu na serikali haikutaka kumwangusha waziri mkuu
“ikamtwanga likizo ya malipo” Bw Jairo lakini ghafla katibu mkuu
kiongozi anaibuka na kumdhalilisha waziri mkuu eti Jairo hana kosa arudi
kazini, wakati Pinda akisita kuchukua hatua wabunge kwa umoja wao
wameamua kumtetea waziri mkuu kwa kudhalilishwa sasa Bunge limeunda
kamati.
Hivi
katika mduara huu wa “kudhalilishana na kushushiana heshima” ipi nafasi
ya Pinda? Yapi maamuzi ya Pinda? Kichekesho ni kuwa Pinda “yupoyupo tu”
hajachukua uamuzi na dalili zinaonyesha kuwa kwa mara nyingine tena
Pinda amekubali kupiga magoti na kujishusha sehemu aliyotakiwa apigiwe magoti
yeye huyu ndiye Pinda ambaye bilashaka hata “ukimpiga ngumi” yeye
wakati wa kukurudishia lazima atavaa gloves ili asikuumize.
Pinda
anataka pepo? Anataka watanzania tumkumbuke kuwa ni kiongozi jasiri?
Basi hana budi kufa ili aione hiyo pepo! Naam amedhalilishwa sana,
ameshushiwa hadhi yake, na sasa ni wakati wayeye kufikiria kujiuzulu.
Haiwezekani
Luhanjo na Pinda waendelee kuitumikia serikali moja, hiki kitakuwa ni
kiinimacho , ni lazima mmoja wao atoke, na kwa vile wote tunakubaliana
Pinda anaitamani pepo, anataka kukumbukwa mioyoni mwa watanzania, lazima
aachane na serikali hii ya akina Luhanjo na Jairo, hana budi kumwachia
Kikwete ateue waziri mkuu mwingine ambaye atakubali kuvunjiwa heshima,
Naam! Pepo haiji hivihivi, ni lazima Pinda afe leo ili aione pepo kesho!
Nova Kambota Mwanaharakati,
Tanzania, East Africa,
Alhamisi, September 1, 2011.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)