Hapo nyuma nilitoa ushuuda wangu kuhusiana na kikombe cha
babu. Baada ya kupata kikombe changu, nilirudi zangu DAR. Siku 12 zikapita
nikawa situmii ARV's matokeo hali yangu ikawa mbaya sana ikabidi nikimbizwe
hospitalini. Ilinibidi kuzirudia ARV na sasa hali yangu imeimarika kiasi. Rafiki
yangu, mwenye virusi vya ukimwi naye alienda kwa babu, aliporudi alianza
kutangaza kwamba kapona. matokeo yake hali yake ikawa mbaya ghafla na kufariki
dunia.
Nadiriki kusema wazi kwamba sidhani yupo hata mmoja
aliyepona kwa babu. Kule loliondo nilikutana na watu wengi zaidi ya 10 ambao
walifariki wakiwa kwenye foleni, na wengi wao kutokana na ugumu wa maisha
walisogea umbali mfupi na kuzitupa miili ya ndugu zao. Nashangaa hadi leo
serikali haijatoa tamko kuhusu watu wanaopoteza maisha yao loliondo, wala
haijatoa tamko rasmi kuhusu tiba ya babu. Mbaya zaidi, Synnovate wamedandia hili
sakata kwa kudanganya umma kwamba 78% ya waliokunywa dawa
wamepona
Kabla sijaenda loliondo, ndugu zangu pamoja na marafiki
walikatiza sana moyo kwenda, ila kutokana na hali yangu ya kuichungulia mauti,
sikuwa na jinsi. Nililazimika kwenda kutafuta tiba ya loliondo. Cha kushangaza
zaidi, baadhi ya hawa ndugu na marafiki nao ni waathirika wa virusi vya ukimwi
ambao wanatafuta tiba.Wiki chache baadaye, magazeti na vyombo vingine vya habari
vilipambwa na viongozi wa kitaifa waliokwenda kwa babu wakionyesha umma kwamba
dawa ya babu kweli ilikuwa tiba kwa mafano "Augustino Mrema" alisema kapona
kisukari.
Matokeo yake hata wale waliokuwa wakinikejeli waliondoka
na kwenda kwa babu. Hadi naandika hii barua, wawili kati yao wamefariki baada ya
kurudi wakiamini wamepona. mwingine kapandwa na ukichaa baada ya hali yake
kuzorota zaidi, na mda wowote anaweza kututoka.Bila viongozi wa serikali kwenda
loliondo ndugu zangu na mafariki wasingekufa haraka hivi.
Nadiriki kusema kwamba, naifungulia serikali yetu
mashtaka kutokana na vifo vya ndugu zangu wawili na marafiki watatu kutokana na
kuudanganya umma. Nazifungulia vyombo vya habari vilivyoshirika kuiadaa umma,
pamoja na kampuni ya Synnovate ambayo imezidi kuikoroga jamii wakidai kwamba 78%
ya waliokunya kikombe cha babu wamepona. Kwanza serikali ilitudanganya ikisema
kwamba ingepima dawa hiyo ya babu na kutujulisha kama kweli inatibu magonjwa
sugu anayodai babu.
Hadi leo serikali imekaa kimya. Viongozi wengi wa kitaifa
wamekimbilia loliondo, kitu ambacho kiliwafanya ndugu zangu ambao hali yao
ilikuwa nzuri kuamini kwamba, kama viongozi wanakimbilia loliondo basi nao
waende ili wapone, matokeo yake wakafa. Kwa maana hiyo naifungulia serikali
makosa mengi ya jinai na udanganyifu. Navishtaki vyombo vya habari pamoja na
serikali kwa kutokuwajali wananchi wake. Nakumbuka Maggid mjengwa, John mashaka,
pamoja na kaka mmoja anayeitwa mwilima walileta mijadala mikali sana kuhusiana
na loliondo tukidhania serikali ingechukua jukumu la kuiambia umma ukweli
kuhusiana na loliondo ambalo limegeuka kuwa machinjo ya watanzania wasio na
hatia.
mdau
mallya
Habari kwa hisani ya
Jiachie Blog
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)