Na Joseph Senga
KATIKA
hali ya kutatanisha uongozi wa Jeshi la Polisi makao makuu jijini Dar
se Salaam, umemhamisha mmoja wa askari wake, Koplo Chale Yunus kutoka
Makao Makuu na kumpeleka katika Kikosi cha Mbwa na Farasi ambacho pia
kipo jijini humo, ukimtuhumu kuvujisha taarifa kwenye vyombo vya habari
kuhusu makazi yake.
Habari
za kuaminika kutoka ndani ya jeshi hilo zimeeleza kuwa, baada ya habari
zilizotolewa na gazeti hili toleo namba 2443 la Agosti 12, mwaka huu
katika ukurasa wa tatu, ikiwa na picha iliyoonyesha makazi ya askari
huyo yaliyoko kwenye mahema eneo la Ukonga Magereza mkabala na Kanisa
Katoliki, uongozi huo uliamua kumhoji na kufikia uamuzi wa kumhamisha
kama adhabu.
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya
jeshi hilo makao makuu kimedokeza kwamba, askari huyo mwenye mke na
watoto watatu alihamishwa siku mbili tu baada ya habari hizo kuandikwa
gazetini na kuhojiwa na wakubwa wake.
Chanzo
hicho kimebainisha kuwa maofisa wa polisi makao makuu walikerwa na
habari hizo wakidai zimelidhalilisha jeshi hilo.
“Huyu
bwana mnayemtafuta, amehamishwa tangu juzi, sasa hivi yuko kikosi cha
Mbwa na Farasi, alituaga japokuwa hakuweza kutueleza sababu ya kupewa
uhamisho wa ghafla, lakini tunadhani ameadhibiwa maana awali alitudokeza
kuwa aliitwa na bosi (hawakumtaja jina) ili ajieleze kwa tuhuma kwamba
alikwenda kwenye vyombo vya habari kulalamikia makazi yake,” alieleza
askari mmoja ambaye aliyekuwa akilinda Mkao Makuu.
Hivi
karibuni gazeti hili liligundua makazi ya polisi huyo na kubaini kuwa,
mahema hayo yalikuwa ni makazi ya askari polisi anayefanyakazi Makao
Mkuu jijini Dar es Salaam, kabla ya kufanya mahojiano na mkewe, Mariam
Chale ambaye alieleza kuwa, tangu nyumba waliyokuwa wakiishi kulipuliwa
na mabomu ya jeshi kutoka kambi ya Gongo la Mboto, wamekuwa wakiishi
hapo mpaka sasa.
Jitihada za kumpata Koplo Chale na
uongozi wa jeshi hilo, ili kujua sababu za askari huyo kuendelea kuishi
katika mahema ambayo hayana ubora, bado zinaendelea.
Akithibitisha
kutokea kwa taflani hiyo, msemaji wa mkuu wa jeshi hilo, ASP Advera
Senso alisema uhamisho wa askari huyo ulikuwa ni wa kawaida kwa kuwa ni
mtaalam wa mbwa na dereva.
“Ni
kweli nimethibitisha kuhamishwa kwa askari huyo, lakini ni jambo la
kawaida tu, kwanza kwa sababu alikuwa ameazimwa kutoka huko kuletwa
makao makuu, sasa amerudishwa alikotolewa wala halihusiani na suala la
yeye kutoa taarifa za makazi yake kwenye gazeti, naomba ieleweke hivyo”,
alibainisha msemaji huyo.
Alisema,
jeshi la Polisi limekuwa likifanya jitihada za kuhahakisha askari
wanapata makazi bora ikiwemo kuwajengea nyumba na hatimaye kuwaondoa
katika makazi yanayoingiliana na raia, ili waweze kutenda kazi zao kwaa
ufanisi na kujenga nidhamu kazini.
Katika
jitihada za kutafuta ukweli kuhusu sakata hilo, gazeti hili
lilifanikiwa kumpata askari huyo kwa njia ya simu ya kiganjani, lakini
alisita kuzungumzia kwa udani kwa maelezo kuwa haruhusiwi kuzungumzia
masuala yoyote ya jeshi hilo na kumtaka mwandishi kuwasiliana na
wahusika.
“Bwana mimi kweli naishi hapo na kweli
nimehamishwa kutoka makao makuu, sasa niko katika kikosi cha mbwa na
farasi, lakini nakuomba uwaone wahusika ndio watakupa maelezo zaidi,
nafikiri ndugu mwandishi unajua utaratibu wa jeshi kutoa taarifa, wapo
wanaohusika”, alisema askari huyo katika hali ya hofu.
Juhudi
za kumpata Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha ili kutolea
ufafanuzi sula hilo, hazikufanikiwa kwa vile simu yake ya mkononi
ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.
mwisho
Ziada: Picha iliyoatachiwa hapa ndio
iliyosababisha hali hiyo...hata hivyo mbali na kumuamisha kuwa kulikuwa
na vitisho na inadaiwa Wakubwa wa ngazi ya juu hawajashirikishwa juu ya
hilo na walioamua ni wa ngazi ya chini..sasa..kweli TANZANIA tutafika??






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)