Na Anna Nkinda – Maelezo
21/08/2011
Ili kuboresha elimu na kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hapa nchini
walimu wametakiwa kuwa karibu na wanafunzi wao na kuwapenda kwa kufanya
hivyo wanafunzi watayapenda masomo wanayoyafudhisha na kuwaheshimu.
Wito
huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiwaaga walimu
wanafunzi kutoka chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino tawi la Mtwara
waliokuwa wanafanya mazoezi ya kufundisha katika shule za Sekondari za
WAMA – NAKAYAMA na Nyamisati zilizopo wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Hafla
hiyo fupi ya kuwaaga wanafunzi hao ilifanyika jana katika ofisi za
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizopo ikulu jijini Dar es
Salaam.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA alisema kuwa kama mwalimu
hatakuwa karibu na wanafunzi wake ni vigumu kwa wanafunzi kuyapenda masomo anayoyafundisha pamoja na kumpenda mwalimu huyo.
“Ninyi hapa ni walimu wanafunzi ipo siku mtakuwa walimu kamili na mtakuwa walimu
wa darasa au walimu wa zamu hivyo basi ni lazima muwe karibu na
wanafunzi , msikae nao mbali na kuwachukia kwa kufanya hivyo
hawatawapenda hata kama mtakuwa mnafundisha vizuri kiasi gani”, alisema.
Aidha Mama Kikwete aliwataka walimu hao kufuata maadili yao ya kazi ikiwa
ni pamoja na kuvaa mavazi ya heshima jambo ambalo litawafanya wafanye
kazi zao vizuri huku wakipata heshima kutoka kwa wanafunzi pamoja na
jamii inayowazunguka.
Wakiongea
kwa niaba ya wenzao Hango Tatu na Magoa Kaiza walisema kuwa licha ya
wao kwenda kujifunza kufundisha katika shule hizo pia wamejifunza mambo
mengi zaidi ambayo yatawasaidia katika kazi yao ya ualimu na maisha yao
kwa ujumla.
Walisema, “Tumeona jinsi walimu wanavyofundishana namna ya kuwafundhisha wanafunzi jambo ambalo hatujawahi kuliona , wanaandaa program, namna ya kuandaa somo na kutengeneza skimu ya kazi hakika inapendeza.
Sisi
kama walimu shida kubwa inayotusumbua ni lugha ya kiingereza na somo la
hesabu tulipata bahati ya kuhudhuria mafunzo ya Peaceful start ambayo
yametusaidia sana, tunahakika kuwa mafunzo haya licha ya kutusaidia katika kazi yetu ya ualimu pia yatatusaidia katika maisha yetu ya baadaye”.
Kwa
upande wa wanafunzi waliokuwa wanawafundisha walisema kuwa wanafunzi
hao wananidhamu , hawahitaji kusukumwa huku wakifuata ratiba
wanayopangiwa ukilinganisha na wanafunzi wa shule zingine
ambazo wamewahi kufundisha kwani mwanafunzi bila kuwa na nidhamu hawezi
kusoma vizuri.
Kutokana
na utaratibu wa vyuo kuwapa fursa wanafunzi wake kwenda kufundisha kwa
vitendo katika shule mbalimbali hapa nchini shule hizo zilipokea walimu
wanafunzi saba kutoka chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine tawi la
Mtwara ambao walifundisha kwa kipindi cha mwezi mmoja.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)