NA MWANDISHI WETU
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kitahakikisha katika mabadiliko yake ya sasa
kinawarejesha katika kuujua ukweli vijana waliopotoshwa na wapinzani
hadi kufikia hatua ya kudhani hakuna mazuri yaliyofanywa tangu uhuru.
Mikakati
hiyo ilisemwa jana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape
Nnauye wakati akizungumza na baadhi ya viongozi na watangazaji wa
Clouds Media Group, Mikocheni Dar es Salaam, alipofanya ziara ya
kujitambulisha katika wadhifa wake huo na kueleza mabadiliko
yaliyofanywa na Chama, mapema Aprili mwaka huu.
Alisema,
wakati wapo vijana ambao hawakuipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu
uliopita kwa sababu zinazoonekana kuwa za msingi, lakini ipo idadi
kubwa ya vijana ambao walifanya hivyo kutokana na chuki tu kutokana na
kushibishwa na uongo na baadhi ya vyama vya upinzani.
Nape
alisema katika miaka ya karibuni hasa baada ya kupevuka kwa kiwango
kikubwa mawasiliano kwa njia ya mitandao kwenye kompyuta, baadhi ya
vyama hivyo vimetumia na vinaendelea kutumia mawasiliano hayo kueneza
uongo kwa njia hiyo na kufanikiwa kuwanasa vijana wengi kwa kuwa ndio
wanaopendelea zaidi kutumia mawasiliano hayo ya mtandao.
"Baada
ya vyama vya upinzani kujua kwamba vijana wengi wanapenda zaidi
upashanaji habari kwa njia ya mitandao kwenye kompyuta, kuliko mikutano
ya hadhara na njia nyingine za kawaida, baadhi ya vyama hivi
vimetumia sana njia hii kuwajaza uongo vijana", alisema Nape.
"Na
kwa sababu uongo ukizidi kuenezwa bila kupingwa huweza kuonekana
ndiyo ukweli, baadhi ya vijana wameamini uongo huo, na matokeo yake
wamejenga chuki kiasi cha kutoyaamini hata mambo ya maana na ya msingi
wanayoambiwa na CCM na serikali yake jambo ambalo ni hatari kwa hatma
ya taifa", alisema Nape.
Alisema
katika mikakati yake ya sasa CCM itahakikisha inawapa ukweli kupitia
njia hiyo ya mawasiliano ya mitandao ya kwenye kompyuta kama 'face
book' na kueleza matumaini yake kwamba hatua hiyo itazaa mafanikio kwa
kuwa yameanza kuonekana katika hatua za awali ambazo CCM imeanza
kufanya.
Nape
alisema, CCM inafanya hivyo kwa kuwa bado kina uwezo wa kuongoza huku
kukiwa hakuna chama cha upinzani ambacho kinaweza kujitapa kuwa
kinaweza kuongoza nchi kwa uhakika ikilinganishwa na hali inayojionyesha
katika vyama hivyo hadi sasa.
Alisema,
mbali ya kuyaendea makundi ya vijana, CCM pia imejipanga kuyafikia
kwa ufanisi zaidi makundi yote, kwa kutumia njia mbadala, ikiwemo
kufuatilia kwa karibu maoni ya vyombo vya habari hasa vile
vinavyoonekana kuwa makini zaidi katika kutoa habari zake.
Nape
aliahidi CCM kutoa ushirikiano mkubwa kwa vyombo vya habari katika
kuhakikisha vinapata habari za ukweli, sahihi na kwa wakati kuhusu
chama na hata za ndani ya serikali.
"Tunaamini
sisi CCM tukifungua masikio yetu vilivyo kwa vyombo vya habari
tuyaweza kuongoza nchi kwa usahihi zaidi, kwa sababu ninyi vyombo vya
habari ndiyo mliopo mitaani wakati mwingi, hivyo mnaweza kuwa mnayajua
mengi kuliko sisi, ni vizuri tukawa tunawasikiliza na kufanyia kazi
mnayosema", alisema Nape.
Katika
ziara hiyo, Nape alizungumzia kwa kina dhana ya mabadiliko ndani ya
Chama na utekelezwaji wake unavyoendelea na baadaye waandishi wa
Clouds Media Group walipata fursa ya kuzungumza na kumuuliza maswali
yaliyoona yanafaa.
Baadaye
Nape akiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni hiyo ambayo ni
walimiki wa vituo vya Clouds FM, Choice FM na Clouds TV, Ruge Mutahaba
alipata fursa ya kutembelea baadhi ya vituo hivyo kuona kazi
zinavyofanyika.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)