BREAKING NEWS:Kesi ya Hosni Mubarak yaanza MJINI Cairo - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

BREAKING NEWS:Kesi ya Hosni Mubarak yaanza MJINI Cairo

Bw Hosni Mubarak alipokuwa kizimbani
Bw Hosni Mubarak alipokuwa kizimbani

Kesi ya aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak, ambaye alilazimishwa kuondoka madarakani kutokana na maandamano makubwa mwezi wa Februari, imeanza mjini Cairo.

Bw Mubarak alipelekwa mahakamani katika chuo cha polisi akiwa kwenye machela huku wapinzani wakishangilia. Anashtakiwa kwa tuhuma za rushwa na kuamuru mauaji kwa waandamanaji - mashtaka ambayo adhabu yake ni hukumu ya kifo.Wanawe Alaa na Gamal, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Habib al-Adly na maafisa wengine sita wa zamani pia wanakabiliwa na mshtaka. Kiasi cha wanajeshi na askari polisi 3,000 wamewekwa kudhibiti usalama katika chuo hicho cha polisi wakati kesi ikiendelea.

Awali kesi hiyo ilikuwa imepangwa ifanyike mjini Cairo kwenye kituo cha mikutano, lakini maafisa wa serikali waliamua kesi hiyo isikilizwe katika mahakama ya muda iliyotengenezwa ndani ya chuo cha polisi kwa sababu za usalama.

Kizimba kilijengwa na watu wanaokisiwa kufikia 600 waliangalia mwenendo wa kesi hiyo. Bw Mubarak, mwenye umri wa miaka 83, alipelekwa Cairo akitokea hospitali kwenye mji wa kitalii wa Sharm el-Sheikh, ambako amekuwa akishikiliwa huku akipatiwa matibabu tangu mwezi wa Aprili kutokana na maradhi ya moyo.

Aliingizwa kizimbani akiwa katika machela, ambapo alifuatilia kesi ilivyokuwa ikiendeshwa pamoja na washtakiwa wengine, wakiwemo wanawe wawili. Jaji Ahmed Refaat alifungua kesi hiyo kwa kuomba utulivu, akisema "raia wastaarabu wa Misri nahitaji utulivu....ili kazi za mahakama zinakwenda vizuri na kwa ukamilifu, kwa hiyo tunaomba hayo kwa Mwenyezi Mungu na nafsi zetu".

Mwandishi wa BBC Jon Leyne amesema, kila mtu amekuwa katika hofu, kwa sababu huu ni wakati ambao kila mmoja nchini Misri na Mashariki ya Kati kwa ujumla, wanatazamia kushuhudia. Mapema nje ya mahakama hiyo, vurugu zilizuka baina ya mamia ya wafuasi na wapinzani wa Rais huyo wa zamani, huku mamia ya askari polisi na wale wa kutuliza ghasia wakijihami kwa na ngao na kofia za chuma wakiingilia kati kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakirushiana mawe na chupa.

Rais huyo wa zamani wa Misri alijiuzulu tarehe 11 mwezi wa Februari, baada ya siku 18 za upinzani kwenye bustani ya Tahrir mjini Cairo, ambapo watu 850 waliuawa.

Wakili wa Bw Mubarak alisisitiza Rais huyo wa zamani ni mgonjwa sana. Mwandishi wa BBC anasema raia wengi wa Misri wana mashaka na hoja hiyo.

Source: BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages