PRECISION AIR KUPATA NDEGE MPYA AINA YA BOEING 737 - 300 NA KUANZA SAFARI ZA COMOROS - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

PRECISION AIR KUPATA NDEGE MPYA AINA YA BOEING 737 - 300 NA KUANZA SAFARI ZA COMOROS

Dar es Salaam July 05th, 2011. Shirika la ndege la Precision leo limetangaza ujio wa ndege mpya aina ya Boeing 737-300 na pia limetangaza kuanza safari za visiwa vya Comoros-Hayaiya. Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari leo tarehe 5 mwezi wa July, uliofanyika katika ofisi za Shirika la Precision, mkurugenzi mkuu Bwana Alfonse Kiokoa alisema; “Tunafurahi kuwatangazia wateja wetu kwamba tunatarajia kupokea ndege mpya aina ya Boeing 737-300 yenye uwezo wa kubeba abiria 116, inayotarajiwa kutua nchini katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam tarehe 24 Mwezi wa July. Kwa sasa iko nchini Norwich katika hatua za mwisho za kupakwa rangi ya kampuni yetu. “Kuwasili kwa ndege hii kutatuwezesha kuboresha na kuimarisha huduma zetu za ndani na nje ya nchi. Na pia itatuwezesha kufungua njia mpya za kimataifa. Kwa kuanza tu, napenda kutangaza rasmi uzinduzi wa safari za visiwa vya Comoros utakaoanza tarehe 17 August 2011 . Kwa kuanza tutakuwa tukitoa huduma zetu mara tatu kwa wiki Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na nauli zetu zitakuwa ni za kiushindani sana. Wateja wetu watalipa kiasi cha dola za kimarekani 392 ikiwa ni nauli ya kwenda na kurudi ikijumuisha kodi zote za serikali”. Alisema Kioko. “Pia tuko katika hatua za mwisho za kuanza tena kutoa huduma zetu za kwenda Afrika ya Kusini katika mji wa Johannesburg. Njia ambayo tumeishawahi kutoa huduma zetu. Mipango na mikakati yote tayari imeishakamilika, na tunawahahidi wateja wetu kuwa tutawapatia huduma bora na za kiushindani kwa gharama za chini ambazo zitaufanya usafiri wa ndege kuwa wa kawaida na kwa kila mwenye kuhitaji kusafiri. Tarehe ya kuanza huduma itatangazwa hivi karibuni.” Alisema. “Kama nilivyosema hapo awali, ujio wa ndege hii utaimarisha na kupanua wigo wa huduma zetu ndani ya nchi na Afrika Mashariki na kutwezesha kufungua njia mpya na kuongeza idadi ya safari katika baadhi ya njia. Napenda kuwatangazia uzinduzi wa kituo kidogo (Min hub) cha huduma zetu ndani ya nchi katika mji wa Mwanza. Mwanza kitakuwa kituo chetu katika kuimarisha huduma zetu katika ukanda wa ziwa ambapo baadhi ya ndege zetu zitakuwa zikianzia na kumalizia safari zake katika mji wa Mwanza. Hii itatuwezesha kuongeza ufanisi na uhakika wa kutoa huduma kwa wakati na ubora zaidi. Pia tutaongeza idadi ya safari katika baadhi ya njia huku tukiendelea kutoa huduma bora kwa gharama za kiushindani zaidi. Kutokea Mwanza tukatkuwa tukiruka katika miji ya Dar esSlaam, Kigoma, Bukoba, Kilimanjaro, Shinyanga, Musoma, na Nairobi kwa idadi ya safari nyingi zaidi tukitumia ndege za Boeing na ATR. Wateja wetu wa Mwanza wataanza kufurahia huduma za Boeing kati ya Mwanza na Dar mara tatu kwa siku na pia ndege zetu zenye burudani ya sinema za ATR kwa mara mbili kwa siku na kufanya safari zetut kuwa mara tano kwa siku. “Pia wateja wetu wanaosafiri kati ya Dar na Nairobi, nao pia watafurahia huduma za Boeing kwa wakati wote mara nne kwa siku”. Alisisitiza Kioko. Pia tutaanza safari za jioni kati ya Dar na Mtwara mara nne kwa wiki huku safari za asubuhi zikiendelea kuwepo na kufanya huduma yetu kupatikana mara mbili kwa siku. Tuaanza kulaza ndege Bukoba na kutuwezesha kutoa huduma za mapema asubuhi kati ya Bukoba na Mwanza na wanaounganisha kwenda katika miji mingine. Wakazi na wasafiri wa Kigoma nao wataanza kufurahia huduma zetu mara nne kwa wiki wakiunganisha kutokea Dar, Nairobi na Kilimanjaro na pia tutakuwa na hudumakati ya Mwanza-Shinyanga-Dar, Dar-Musoma-Mwanza wakiunganisha safari za Dar kutokea Mwanza. Huduma za Mwanza zitakuwa mara mbili kwasiku anagalau mara nne kwa wiki. Pia tutaanzaisha safari za asubuhi mida ya saa nne kati ya Zanzibar na Nairobi mara nne kwa wiki. “Mipango yetu ya kuendelea kupanua wigo wa huduma zetu katika miji mingine ndani na nje ya nchi inaendela na tunapenda kuwahakikishia kuwa tutaendelea kutoa huduma bora na za kiushindani kwa gharama nafuu zaidi”. Alimalizia Kioko. Uzinduzi wa huduma katika visiwa vya Comoro na kituo kidogo katika mji wa Mwanza unaliwezesha shirika la Precision kutoa huduma zake katika miji zaidi ya kumi na tano ndani na nje ya nchi, ikiwana uhakika wa kuunganisha safari za kimataifa kupitia mshirika wake mkuu shirika la ndege la Kenya. Shirika la Precision limekuwa likitoa huduma zake kwa kwa ushindani wa hali ya juu, huku likiwazawadia wateja wake kupitia huduma yake ya wasafiri wa mara kwa mara ijulikanayo kama Paa Royal. Pia wasafiri wa shirika la Precison wamekuwa na wataendelea kufaidika na burudani za kwenye ndege wawapo safarini. Hivi karibuni Shirika limetajwa kuwa shirika la ndege bora ndani ya nchi katika hafla ya chakula cha usiku ya wanachama wa umoja wa huduma za wakala wa ndege (TASOTA) ilyofanyika katika hoteli ya Movenpick on 24 June 2011. Ujio wa ndege ya Boeing utalifanya shirika kuifikisha ndege kumi na moja, tisa zikiwa ATR na mbili Boeing 737-300. Shirika la Precision kwa sasa linatoa huduma zake katika miji ya; Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Zanzibar, Mwanza, Kigoma, Tabora, Musoma, Shinyanga, Mtwara, na Bukoba. Katika ukanda wa Afrika Mashariki linatoa huduma katika miji ya Nairobi, Mombasa na Entebbe, na sasa safari za kimataifa katika visiwa vya Comoros.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages