Mke
wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA Mama Salma Kikwete (kulia) leo
akibadilishana mawazo na Seneta JACKIE WINTERS kutoka Marekani
(kushoto) alipomtembelea ofisini kwake jijii Dae re Salaam.
Na Anna Nkinda –
Maelezo
12/07/2011 Mke wa Rais
Mama Salma Kikwete amewataka wanawake kujenga mazoea ya kubadilishana ujuzi wa
kazi jambo ambalo litasababisha vizazi vijavyo kuwa na utaalamu wa kutosha na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha na
kuinua kipato cha familia.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ameyasema hayo leo
wakati akiongea na wanawake walioshiriki mafunzo ya kusindika vyakula yaliyoandaliwa
na WAMA walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kumshukuru na kumuonyesha bidhaa ambazo wanazizalisha.
Aliendelea kusema kuwa
kwa kuwafundisha wenzao kutakuwa na wigo
mpana wa kuzalisha bidhaa bora na kupata masoko ya kutosha kwani kuna wanawake ambao
hawana ujuzi wa kuzalisha lakini ni washawishi wazuri katika kutafuta masoko ya
bidhaa husika.
“Hivi sasa mnajua jinsi
ya kusindika vyakula jambo linalotakiwa ni kujipanga kwa pamoja ili muweze
kujitangaza na kutafuta masoko ya bidhaa zenu, muwe na lugha nzuri kwa kufanya hivyo mtapata wateja na faida ya kutosha”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
alimalizia kwa kusema kuwa hivi sasa ni wakati wa wanawake wa kusonga mbele kimaisha
na kuachana na tabia ya kutegemea kufanyiwa kila kitu na waume zao na wakitaka kufanikiwa katika kazi ni lazima wawe na moyo
wa kujituma.
Akiongea kwa niaba ya
wenzake Mwenyekiti wa wanafunzi wa mafunzo ya usindikaji Bertha Natai alisema
kuwa wameweza kuhudhuria mafunzo hayo ya siku tano ambayo yalitolewa wezi wa
tano mwaka huu na kufaulu na tayari wameshaanza kutengeneza siagi ya karanga na
juisi ya nyanya.
“Ni kazi nzuri na
imeweza kuwasaidia kina mama kunyanyuka kimaisha hivi sasa tumeunda umoja wetu
ambao uko chini ya WAMA na tumeshaanza kuwaelimisha wenzetu ili nao waweze kutengeneza bidhaa kama hizi na
kupata pesa ambazo zitawasaidia kimaisha”, alisema Natai.
Jumla ya wanawake 30
walihudhuria mafunzo hayo ya kusindika vyakula ambayo yalitolewa
na SIDO kwa vikundi vya wanawake 14 ambavyo viko chini ya usimamizi wa WAMA
kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la
watu wa Marekani (USAID) kutoka wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke na Mkuranga.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)