Msanii wa kizazi kipya Khamis Ramadhan aka
H-Baba (Katikati) akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika
kila wiki Kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).Kulia
kwake ni Afisa wa Sanaa kutoka BASATA Bw.Lawrance Hinju na Kaimu Mratibu
wa Jukwaa hilo Agnes Kimwaga
Afisa wa Sanaa kutoka BASATA,Bw.Lawrance Hinju
(Kushoto) akisisitiza jambo wakati akihitimisha mjadala kwenye Jukwaa la
Sanaa wiki hii
Mkongwe wa muziki wa dansi nchini Kassim Mapili
akimpa ushauri msanii H-Baba mara baada ya kumaliza kuwasilisha mada
yake kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.
Mdau wa Jukwaa la Sanaa akimuuliza
masuala mbalimbali Msanii H-Baba
Wadau wakifuatilia kwa
makini mada kwenye Jukwaa la Sanaa.
Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
limesema kwamba,tunzo mbalimbali zinazotolewa kwa wasanii zinalenga
kuthamini mchango wao katika tasnia na kujenga hali ya ushindani
miongoni mwao katika kubuni kazi zilizo bora.
Hayo yamesemwa na Afisa wa Sanaa
wa Baraza hilo,Bw.Lawrance Hinju wakati akiliahirisha Jukwaa la Sanaa
linalofanyika kila Jumatatu makao makuu ya BASATA eneo la Ilala Sharif
Shamba,Dar es Salaam.
Alisema kwamba,tunzo kama zile za
muziki zimekuwa zikitolewa miongoni mwa wasanii kwa kuzingatia vigezo
mbalimbali vya kitaaluma ambavyo mara kwa mara vimekuwa vikitangazwa na
Baraza katika kuhakikisha kweli wale wanaoshinda ndiyo wanaokuwa
wanastahili na wenye kazi bora.
“BASATA imebuni tuzo za muziki
kwa lengo la kuthamini mchango wa wasanii na kujenga ushindani miongoni
mwao.Tuzo inaweza ikawa cheti au kitu chochote lakini Baraza kwa
kushirikiana na mwendeshaji limeona liwe linatoa tuzo hizo maalum
inayoambatana na fedha taslimu” alisema Bw.Hinju.
Aliongeza kwamba,kulingana na
idadi ya maeneo yanayoshindaniwa si rahisi kwa wasanii wote kupata
ingawa kuna kila sababu ya wao (wasanii) kujikita katika kutengeneza
kazi zenye ubora, zenye maadili ndani yake na zilizo na uhalisia ndani
ya jamii ili mchango wao uonekane na kutuzwa.
Awali akiwasilisha mada kwenye
Jukwaa la Sanaa kuhusu Umuhimu wa Kubuni Vitu vipya kwenye Muziki wa
kizazi kipya,Msanii Khamis Ramadhan aka H-Baba alisema kwamba,wasanii wa
kizazi kipya wanatakiwa kubadilika na kupendana kwani kumekuwa na
tatizo sugu la kuhujumiana na kufitiniana miongoni mwao.
“Nasema wazi kabisa wasanii
hatupendani,tunatakiwa kubadilika ili kuweza kupata
mafanikio.Haiwezekani kufika kokote kwa hali hii” alilalamika H-Baba.
Jukwaa la Sanaa linalofanyika
kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA limekuwa ni eneo huru kwa wasanii,
waandishi wa habari na wadau wa sanaa kuelimishana na kupashana habari
kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo tasnia hiyo
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)