RAIS JAKAYA KIKWETE AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA MALAYSIA NCHINI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

RAIS JAKAYA KIKWETE AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA MALAYSIA NCHINI


Waziri Mkuu wa Malaysia, Najib Abdul Razak akimkabidhi Rais Jakaya Kikwete mfano wa mpira ikiwa ni ishara ya kuitunuku Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Langkawi (LID) mwaka 2013. Hafla ya makabadhiano hayo ilifanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Putrajaya, Malaysia.Picha na Freddy Maro-IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameiomba Serikali ya Malaysia kuvishawishi Vyuo Vikuu vya nchi hiyo kuanzisha ama kuhamishia shughuli zao, hata ikiwezekana kujenga majengo ya vyuo hivyo, katika nchi ya Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete ameiomba Serikali ya nchi hiyo kuwashawishi wawekezaji wa nchi hiyo iliyopo Kusini Mashariki mwa Asia kuja kuwekeza katika uchumi wa Tanzania kwa lengo la kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliotangazwa na Rais Kikwete na hatimaye kuridhiwa na Bunge.

Maombi hayo ya Tanzania yamewasilishwa kwa Malaysia na Rais Kikwete mwenyewe wakati wa mkutano wake na Waziri Mkuu wa Malaysia,Mh. Dato’ Sri Mohd Najib Tun Abdul Razak.
Viongozi hao wawili walikutana, Jumatatu, Juni 21, 2011, kwenye Cyberview Lodge, iliyoko Cyberjaya, mjini Kuala Lumpur baada ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi, Serikali na viongozi wa nchi mbali mbali  walioshiriki katika mkutano wa mwaka huu wa taasisi ya maendeleo ya Langkawi International Dialogue (LID) 2011, uliomalizika, Juni 21, 2011.

Katika mkutano huo, Rais Kikwete amemwomba Waziri Mkuu Razak kuwashawishi Wakuu wa vyuo vikuu na makampuni ya Malaysia kukubali kuja kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Rais Kikwete amemwelezea Mheshimiwa Razak kuhusu Mpango huo wa maendeleo ambao ni sehemu ya mtazamo wa Maendeleo ya 2025 inayolenga kuitoa Tanzania katika umasikini na kuifanya nchi yenye uchumi wa kati.

Rais Kikwete pia amemweleza Mheshimiwa Razak kuwa Mpango wa Maendeleo mpya wa Tanzania ni mpango mzuri na kwamba changamoto kubwa ni kuhakikisha kuwa mpango huo unatekelezeka na hivyo kuleta matunda na matokeo mazuri kwa Watanzania.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini,
KUALA LUMPUR, MALAYSIA.
22 Juni, 2011.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages