YAH:
TAARIFA POTOFU YA GAZETI LA DIRA YA MTANZANIA TOLEO LA JUMATATU, 20 –
26 JUNI, 2011 ‘ SAKATA LA POSHO ZA WABUNGE’ SPIKA MAKINDA MBUMBUMBU
‘Utafiti wabaini anasimamia asichokijua magwiji wa Bunge washangaa tamko
lake’.
1.0UTANGULIZI
Pamoja na Vichwa vya habari hiyo, Katika taarifa hiyo Mwandishi wa gazeti hilo amedai kuwa;
i.Spika wa Bunge, Anne Makinda hana uelewa wa kutosha wa jinsi mbunge anavyoweza kupoteza wadhifa wake
ii.Pia Spika wa Bunge haelewi mfumo wa malipo ya Posho za Wabunge
iii.Spika hana mamlaka ya kumfukuza Mbunge yeyote anayekataa kusaini Fomu za kuchukua posho ya kikao.
2.0MAJIBU YA HOJA POTOFU ZILIZOTOLEWA
Ofisi
ya Bunge ingependa kuwaarifu wananchi kwamba habari hiyo iliyoandikwa
na gazeti la Dira ya Mtanzania ni ya dharau na haina ukweli wowote na
imeandikwa kwa nia mbaya ya uchochezi na kuharibu sifa aliyonayo Mhe.
Spika Bungeni na kwa watanzania kwa ujumla.
Ili
kuondoa upotofu wa taarifa iliyotolewa na gazeti hili, Ofisi ya Bunge
ingependa kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa kama ifuatavyo;
i.
Sio kweli kwamba Mhe. Anne Makinda hana uelewa kuhusu uendeshaji wa
shughuli za Bunge. Mhe. Makinda amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 30
Bungeni na kwa kipindi hicho chote ameshika nyadhifa mbalimbali Bungeni
na Serikalini. Aidha akiwa Naibu Spika ameongoza kamati ya Bunge
iliyoshiriki marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2007.
Kwa
mantiki hiyo anazifahamu vyema Kanuni za Bunge na ana uzoefu na
uendeshaji wa shughuli za Bunge kwa muda mrefu kuliko hata idadi kubwa
ya wabunge wapya waliopo Bungeni. Katika utendaji wake, hafanyi kazi
kwa kuvutwa na hisia bali husimamia uendeshaji wa Bunge kwa Mujibu wa
Kanuni za Bunge ambazo tunashaka hata kama mwandishi wa gazeti hili
anazifahamu vyema.
Ni
kwa kuzingatia hilo aliwaeleza bayana Waandishi wa habari siku
alipofanya nao mahojiano ambapo mwandishi wa gazeti hili pia hakuwepo,
kuwa taratibu la kuchukua posho kwa Mbunge huenda sanjali na kusaini
mahudhurio Bungeni (Mbunge anayehudhuria Bunge ndiye anayelipwa posho),
kwa maana huwezi kumlipa posho Mbunge asiyekuwepo Bungeni. Mahudhurio
ya Mbunge ni pale anaposaini fomu ya Mahudhurio. Kwa mantiki hii,
kanuni zinamtaka bayana kila mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge.
Kanuni ya 143 inatamka kuwa:
(1) kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati ni wajibu wa kwanza wa kila mbunge.
(2)
Mbunge yeyote atakaeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu
mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza
Ubunge wake kwa mujibu wa ibara ya 71 (1) ya katiba na Spika ataiarifu
Tume ya Uchaguzi.
(3) Mbunge atakapokosa kuhudhuria nusu ya vikao vya Mkutano mmoja bila ya sababu ya msingi atapewa onyo.
Hivyo
basi kwa mantiki hiyo, Mbunge atakayeshindwa kusaini fomu za
mahudhurio kwa mtiririko huo hapo juu atakuwa amepoteza sifa zake za
kuwa Mbunge kwa mujibu wa Kanuni.
ii.
Aidha ni kwa uvivu wa kufikiri au kwa makusudi kabisa, mwandishi wa
gazeti hili ameandika yale aliyohisi ni sahihi na kufanya utafiti katika
kiwango ambacho hajaeleza ni kwa kutumia vigezo gani bila hata
kujaribu kuuliza misingi halisi aliyoizungumzia Mhe. Spika kuhusu
uhalali wa mahudhurio ya Mbunge sanjali na ulipwaji wake posho awapo
kazini.
Hivyo
madai ya kuwa Spika hana madaraka ya kumfukuza Mbunge Bungeni hayana
mantiki na wala madaraka ya Spika kuhusu kumfukuza Mbunge hayakuwa
sehemu ya mahojiano na waandishi na Spika wa Bunge kama anavyodai, na
Kanuni zimeeleza bayana kazi za Spika Bungeni. Kumbuka madaraka ya
Spika, wajibu wa Wabunge na hata Miongozo mingine Bungeni huratibiwa kwa
mujibu wa kanuni za Kudumu za Bunge.
Hatujui
lengo la mwandishi ni lipi hasa kwa kuweza kutoa taarifa zenye
upotoshaji mkubwa kwa umma na zenye kuleta dharau kwa kiongozi wa Bunge
na Bunge kwa ujumla kwa kuzingatia kuwa kiongozi huyu amechaguliwa na
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
3.0 HITIMISHO
Ofisi
ya Bunge inapenda kuwaarifu wanahabari wote kuwa Idara yake ya Habari
imekuwa ikitoa ushirikiano wa kutosha kuwaarifu waandishi kwa taarifa
zozote wanazohitaji na inasikitishwa kwa kiasi kikubwa na uandishi
unaojali hisia na wenye kulenga uchochezi badala ya kuelemisha.
Licha
ya mwandishi wa habari hii kutokuwepo Dodoma na wala hakushiriki
mahojiano hayo na Mhe. Spika, habari husika iliyoandikwa imelenga kutoa
taarifa potofu bila kushirikisha hata upande wa pili kwa ufafanuzi. Kwa
kuzingatia hilo Ofisi ya Bunge inamtaka Mhariri wa Gazeti la Dira ya
Mtanzania kuomba radhi kwa uzito ule ule waliotoa habari yao ya
kupotosha umma.
Deogratios Egidio
Kny: KATIBU WA BUNGE
21 Juni, 2011
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)