Ndugu zangu,
NIONAVYO, kuna upepo mgumu wa kisiasa unaovuma sasa kwenye nchi yetu. Ndio, upepo mwingine ni mgumu wenye kutingisha matawi ya miti na hata makoti tuyavaayo. Kamata-kamata hii ya sasa na matumizi ya nguvu ni ishara za upepo mgumu wa kisiasa unaovuma.
Hii
ni nchi yetu. Tunaipenda nchi yetu tuliyozaliwa na ndio maana ya
kuyaandika haya. Na naamini, kuwa msingi wa haya tunayoyaona ni
mapambano ya vyama na makundi katika kuwania kushika mamlaka za dola.
Na
katika upepo huu mgumu wa kisiasa uvumao sasa, ni vema tukaongozwa na
busara badala ya kuruhusu kuongozwa na hisia zetu. Tufanye hivyo kama
kweli tuna mapenzi ya dhati kwa nchi yetu tuliyozaliwa. Maana,
tukionacho sasa ni kazi ifanywayo na baadhi ya wanasiasa ya kupandikiza
chuki miongoni mwetu.
Na tusiombe chuki hii ikaachwa ikomae, maana, sote, kwa njia moja au nyingine, tutalipa
gharama ya ujinga huu wa wanasiasa wa kutanguliza maslahi yao binafsi,
ya vyama na makundi yao badala ya yale ya nchi yetu tuliyozaliwa.
Na katikati ya upepo
huu mgumu wa kisiasa uvumao sasa tunauona mpambano mkali baina ya chama
tawala – CCM na chama kikuu cha upinzani – Chadema. Siasa sasa
inafanywa kuwa uhasama badala ya kuwa nyenzo ya kidemokrasia katika
kuiendeleza nchi yetu. Katika nchi zetu hizi, na katika upepo huu wa
mabadiliko, Serikali ya chama tawala Afrika haina maana ya Serikali inayoongozwa na watendaji wote walio wanachama au wafuasi wa chama tawala.
Hivyo
basi, katika mpambano huu, tunaona, kuwa chama tawala, kwa namna moja
au nyingine kinapotumia dola katika kuikabili Chadema kinaongeza nyufa
za kiuongozi. Huu ni mkakati wa kimakosa na wa hatari sana. Na Mwana-CCM
yule Fredrick Sumaye aliyesomea masuala ya Utawala kule Havard Marekani
alipata kukitahadharisha chama chake, kuwa kisitumie Serikali kwa maana
ya dola kujibu hoja za Chadema, badala yake, CCM ipambane na Chadema
kwa hoja za kisiasa majukwaani. Sumaye alikuwa na hoja ya msingi, sina
hakika kama wenzake kwenye CCM walimwelewa ipasavyo.
Ndio,
tuko sasa kwenye mapambano ya kisiasa ya vyama yenye ushabiki mkubwa
bila misingi ya hoja za kisiasa na kutanguliza maslahi ya nchi. Na
Afrika ukikuta jogoo wawili wanagombana, basi, hapo hapakosi mashabiki. Na
kila shabiki aliyesimama kutazama mpambano wa majogoo hao, ujue, kuwa
ana jogoo wake anayemshabikia. Na jogoo anayemshabikia akishindwa
pambano, shabiki ataondoka akisononeka. Kuna ambao watakosa hata hamu ya
chakula siku hiyo. Kisa? Jogoo wake kagalagazwa!
Na kama jogoo mmoja ni mnene na mwingine ni mwembamba, ujue, kuwa jogoo mwembamba ana mashabiki wengi. Lakini mie ni mmoja kati ya wachache, ambao, kwenye pambano kama hilo, hujitahidi kusimama katikati, hata kama ni kazi ngumu. Nawasilisha.
Maggid,
Dar es Salaam, Juni 9, 2011.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)