1.Baba Askofu umewahi kunukuliwa ukisema “gharama ya
kuilinda amani iliyopo ni ndogo kuliko gharama ya kuirudisha amani
ikishapotea” je kimsingi una maana gani baba Askofu ?
JIBU
Maana yangu ilikuwa ni kuitahadharisha jamii itafakari kwa kina
kuhusu matokeo ya kuvunjika kwa amani. Hakuna uamuzi usiokuwa na
gharama. Uamuzi wa kuivunja amani una matokeo kinyume na kuwepo kwa
amani yenyewe. Matokeo hayo kinyume ni pamoja na kupanda kwa gharama za
maisha, kwa sababu uzalishaji pamoja na huduma za kijamii zinazotolewa
wakati wa amani vitakoma, na jamii italazimika kujitafutia njia mbadala
za kujikimu ambazo zitakuwa ni ngumu na aghali sana.
Hapo sizungumuzii suala la kuongezeka kwa majeruhi wa vita na
machafuko ambayo wahusika pamoja na kuachishwa uzalishaji; lakini
watahitaji tiba ambazo ama hazitakuwepo kabisa, au zikiwepo zitakuwa ni
aghali hazinunuliki, matokeo yake ni wengi kupoteza maisha au kuwa na
vilema vya maisha.
Si hayo peke yake, hata juhudi za kujaribu kuirejesha amani
iliyotoweka nako kutagharimu zaidi. Maana itatuchukua muda mrefu zaidi
kuirejesha. Isitoshe, wapo wengine ambao hawatakubali amani irejee kwa
sababu tu wananufaika na mazingira ya vita na machafuko.
Sasa basi, kwa mwananchi wa kawaida ambaye mpaka hivi, katika
mazingira ya utulivu bado maisha yake ni shida tupu; je! hali yake ya
maisha itakuwaje pale ambapo gharama za maisha zitapanda ghafla na
kudumu kwa muda usiojulikana wa kutokuwepo kwa amani? Nilitaka jamii
ilitafakari hili.
2. Uhuru wa vyombo vya habari unaongeza uelewa miongoni mwa
wananchi na pia unachochea tabia na mienendo ya wananchi kiasi kwamba
kumeibuka hali ya vuta nikuvute baina ya viongozi na wananchi, je
unaliongeleaje hili? Unadhani ni kweli kuna uhuru wa habari? Una
manufaa gani?
JIBU
Kuna tofauti kati ya kuwa na “uhuru wa habari” na “matumizi sahihi
ya uhuru wa habari”. Tukifanya tathmini kuanzi miaka 20 iliyopita, (kwa
sisi tulioshuhudia mwanzo wa uhuru, azimio la Arusha mpaka Azimio la
Zanzibar), hakuna wa kubisha kwamba Tanzania tunao uhuru wa habari.
Hata kama uhuru wenyewe sio asilimia mia moja, lakini upo tena
unaotushinda hata kule kuutumia ipasavyo.
Tatizo kubwa tena linaloelekea kuwa sugu ni dalili za kuwepo kwa
“matumizi yasiyo sahihi ya uhuru wa habari”. Bila shaka, tatizo hili
linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mazingira mapya ya utandawazi,
uchanga wa uwezo wa umilikaji wa vyombo vya habari pamoja na ukiukwaji
wa maadili ya habari.
Kwa hiyo, kile kinachoonekana kuwa ni “hali ya vuta nikuvute baina
ya viongozi na wananchi” hakikusababishwa na kuwepo kwa uhuru wa habari
bali matumizi yasiyo sahihi ya uhuru wa habari.
3. Wewe kama mmoja wa wadau wa maadili kwenye taifa, je
umelipokeaje swala la baadhi ya wabunge kutaka kupigana bungeni? Na una
ushauri gani?
JIBU
Kwanza, bado tunapaswa kukumbuka kwamba demokrasia yetu bado ni
changa. Pili, kwa mujibu wa taratibu za kuwapata viongozi wa
kutuwakilisha katika ngazi za udiwani, ubunge hata urais, maadili kama
maadili katika maana yake halisi bado si kigezo kinachopewa uzito
unaostahili. Tafuta mwenyewe uone sifa za mtu kugombea nafasi ya
uongozi katika ngazi husika, sifa ya maadili haimo.
Kwa hiyo, si ajabu kama kutajitokeza dalili za ukiukwaji wa maadili
katika Nyanja za uongozi. Ni vema tukumbuke kwamba mlango wa kukiukwa
kwa maadili umeachwa wazi tangu awali kwenye sifa za kuwapata viongozi
katika ngazi husika. Hapa itabidi tusubili ujio wa katiba mpya pengine
tutapata ufumbuzi wakati huo ukifika. Nikiwa na maana kwamba kigezo cha
maadili kama mojawapo ya sifa ya kupata viongozi kitazingatiwa
kikamilifu.
4.Rushwa umekuwa ni mwiba sasa kwa taifa letu licha ya kazi
za TAKUKURU na sheria zilizopo, je nini nafasi ya viongozi wa dini
katika kupambana na rushwa?
JIBU
Hili ni swali zito na muhimu. Siwezi kulijibu kwa haraka na kwa
ufupi katika jukwaa lako. Linahitaji mjadala mzito, tena wa kuwahusisha
kikamilifu viongozi wa dini. Nasema hivi kwa sababu rushwa sio tu
kuwekewa TAKUKURU na sheria za nchi, lakini pia imeandikwa katika
misahafu ya dini zetu.
Nafasi pekee ya viongozi wa dini, katika kupambana na rushwa, ni
kurejea upya maagizo na sheria zilizomo katika misahafu ya dini husika.
Kipaumbele kisiwe kukomea katika kukemea rushwa katika jamii, badala
yake uzito mkubwa uelekezwe katika kurejesha maadili ya kiimani ambapo
rushwa inatafsiriwa kuwa ni dhambi mbaya na hatari hivyo lazima iogopwe.
Kila mwamini aelimishwe bayana kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa
dhambi ya rushwa ni Jehanamu ya moto. Pasipo mtu kuwa na hofu ya Mungu
siku ya kiyama hakuna silaha itakayofaulu katika kudhibiti rushwa.
5. Kumekuwa na tuhuma za baadhi ya viongozi wa dini kutumiwa
na wanasiasa nchini kufanikisha malengo yao, je wewe kwa upande wako
limewahi kukukuta? Na je ni kweli lipo hili au ni uzushi tu?
JIBU
Mimi nami nimezisikia kama wewe. Kwa kumbukumbu zangu binafsi
zijawahi “Kutumiwa na siwezi kutumiwa” na wanasiasa kwa malengo yao.
Kila mahali popote niliposhirikiana na viongozi wa kisiasa chimbuko
lake ni ubunifu wangu na ushawishi wangu kwao na kunipa fursa ya
kutimiza malengo ya wito wangu kwa Mungu na kwa taifa. Siwezi kuwasemea
wengine katika hili sababu sina ushahidi wala uthibitisho.
6. Matumizi ya mabavu dhidi ya wananchi hususani kutoka kwa
vyombo vya usalama limekuwa ni tatizo siku za karibuni, je wewe kama
kiongozi wa kiroho na mwananchi unaliongeleaje hili?
JIBU
Tatizo la msingi katika hili haliko kwenye vyombo vya usalama wala
jamii. Tatizo liko kwenye mfumo uliopo wa mahusiano kati ya pande
husika. Mfumo huu unaweza kurekebishwa vizuri pale ndoto za katiba mpya
zitakapotimia.
7. Rais wa Jamhuri ya Muungano amewataka viongozi wa dini
kujiepusha na biashara haramu ya madawa ya kulevya tena ameonya kuwa
baadhi ya viongozi wa dini wanajihusisha na biashara hii haramu na
baadhi ya viongozi wa dini wakaja juu wakimtaka athibitishe madai yake
kwa kuwataja wahusika, je! wewe unalipokeaje hili?
JIBU
Hili nimelipokea kama bomu ambalo limelipukia kwenye kambi ya
madhehebu ya dini. Hii ni kashfa nzito. Aliyeiweka hadharani ni mtu
mzito, mkuu wa nchi mwenye vyombo vya dola. Wenzangu wamesema lakini
mimi bado natafakari kwanza. Nasali kwa Mungu anipe ufunuo wa lipi
niseme, niseme kwa nani na ili iweje.
8. Tiba ya Loliondo imekuwa ni moja kati ya mambo yaliyovuta
hisia za viongozi wa dini huku baadhi wakipinga na wengine wakiunga
mkono, je wewe kama mmoja wa viongozi wa dini unaliongeleaje hili? Na
upi msimamo wako katika tiba ya Loliondo?
JIBU
Tangu habari hizi zianze kupewa uzito wa pekee na vyombo vya habari,
kila nilipohojiwa jibu langu lilikuwa moja, “nafanya utafiti”. Kusema
kweli mpaka sasa bado nafanya utafiti. Utafiti ninaoufanya ni kujua kwa
hakika kwa kupitia maandiko matakatifu ya Biblia kama bado Mungu anatoa
mafunuo na maagizo ya tiba kupitia dawa, vitambaa, maji ya Baraka, nk.
Nikikamilisha utafiti wangu nitasema wakati huo. Msimamo wangu
utajengwa kwenye taarifa ya utafiti ninaofanya hivi sasa.
9. Mihadhara ya kidini imekuwa sio tena sehemu ya
kufundishana dini bali kukashfiana na pole pole uvumilivu wa kidini
umeanza kutoweka, je unadhani kuna haja ya kupiga marufuku mihadhara ya
kidini?
JIBU
Nani apige marufuku na kwa mamlaka ya nani? Je! Huu si ndio uhuru wa
kuabudu na kueneza imani kwa mujibu wa haki za binadamu? Haya ni
maswali yanayogongana akili mwangu lakini si majibu ya swali lako.
Majibu ni kwamba, katiba mpya ndio ufumbuzi wa hii mitafaruku ya kidini
ambayo inaonekana kuwa kero.
Unaweza kucheka kila ninapojibu kwa kutaja hoja ya “katiba mpya”.
Lakini nina maana kamili katika kujibu hivi. Nami nimejiandaa kushiriki
kikamilifu na uzito wangu utajikita katika nafasi ya “Haki na Uhuru wa
kuabudu na kueneza dini; pamoja na mahusiano yanayotakiwa kuwepo
“kikatiba” kati ya dini na serikali.
10. Mwisho kabisa baba kwenye changamoto lukuki kama
maandamano ya CHADEMA, ugumu wa maisha, malumbani ya wanasiasa, migomo
ya vyuo vikuu na ajali za barabarani za mara kwa mara zinazolikumba
taifa letu nini mtazamo wako, maoni na ushauri wako kwa viongozi wa
dini, serikali na jamii kwa jumla?
JIBU
Majibu yangu, mtazamo wangu, na ushauri wangu kwa viongozi wa dini,
serikali na jamii kwa jumla ni kuwa na “katiba mpya”! Asante sana
mhariri.
Na Nova Kambota
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)