WANAFUNZI
WA KITANZANIA – CHUO KIKUU CHA URAFIKI LUMUMBA, MOSCOW-URUSI.
Mhe. Waziri Mkuu
Peter Mizengo Pinda,
Tunaomba
kuanza kwa kukupa pole kwa majukumu mazito uliyo nayo katika ujenzi wa
taifa letu. Pia tunakupongeza kwa uimara na ushupavu wako katika
kusimamia masuala mbalimbali ya kimaendeleo nchini.
Mhe. Waziri
Mkuu,sisi wanafunzi wa kitanzania katika Chuo Kikuu Cha Urafiki –
Lumumba kilichopo jijini Moscow inchini Urusi tunaishukuru sana
Serikali yetu kwa kuweza kutupatia udhamini wa masomo ya elimu ya juu
kupitia Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Kwani fursa hiyo ni
moja ya njia za kuelimisha taifa na pia kuongeza idadi ya watendaji
bora katika sekta mbalimbali nchini.
Mhe. Waziri Mkuu,
lengo kuu la waraka huu kwako ni kukufikishia malalamiko yetu moja kwa
moja juu ya kero mbalimbali tunazozipata kuhusiana na zoezi zima la
mikopo hii tunayopatiwa na serikali yetu. Tumeamua kufikisha malalamiko
haya kwako kwa sababu wahusika wakuu (WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA
UFUNDI pamoja na BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU) hawataki
kusikiliza kilio chetu. Tumeawaandikia barua nyingi sana kuhusiana na
malalamiko yetu pasipo kujibiwa jibu lolote, na sisi hatuwezi kuendelea
kukaa kimya huku tukizidi kuumia, wakati serikali ina kila sababu ya
kutusikiliza kwani hii ni haki yetu ya msingi kabisa.
Mhe. Waziri Mkuu,
malalamiko yetu ni haya yafuatayo:
1:UTARATIBU MBOVU
WA MALIPO YA FEDHA ZA ADA.
Kila mwaka bodi imekuwa na utaratibu wa kutokulipa ada kamili
za wanafunzi kwa wakati. Baadhi ya wanafunzi hufikia hatua ya kutoa
fedha zao za kijikimu ili kufidia mapungufu hayo katika malipo ya ada.
Mfano:
Mwaka 2008/2009 baadhi ya
wanafunzi walilazimika kulipa sehemu ya ada toka katika fedha zao za
kujikimu. Na pia mpaka leo haijulikani sehemu ile ya ada za wanafunzi
hao ilikwenda wapi licha ya kuuliza mara kwa mara juu ya suala hilo
Wizarani na Bodi kwenyewe.
Mwaka huu 2010/2011, bodi imechelewa kutulipia ada kwa
takrirban miezi 9 (kwani ada ilitakuwa kulipwa mwezi wa 9 mwaka
jana(2010) lakini imekuja kulipwa mwaka huu wa 2011 mwezi wa 5, wakati
ndiyo mhula wa pili unaisha. Na cha kusikitisha zaidi wanafunzi walio
wengi wamelipiwa ada pungufu kwa zaidi ya dola 1000 kwa kila mwanafunzi,
na wengine hawakulipiwa kabisa.
Mhe. Waziri Mkuu, hii ni kero kubwa sana kwani mara
kwa mara tumekuwa tukifukuzwa madarasani kwa sababu hatujalipa ada.
Tunadharirika sana. Na hata sasa baadhi yetu wametangaziwa kutokufanya
mitihani yao ya kuhitimu shahada ya kwanza(degree) na wengine mitihani
yao ya kufunga mwaka. Na hali hii hutokea kila mwaka.
2:MAKATO KATIKA
FEDHA ZA KUJIKIMU
Mhe.
Waziri Mkuu, tunasikitika sana kusema kuwa ni jambo lililozoeleka sasa
kwa Bodi kutukata fedha zetu za kujikimu kila mwaka . na kila mara
tunapodai kiasi kilichokatwa, wamekuwa wakisema fedha zinapungua kwa
sababu ya rate of exchange pale wanapobadili fedha za kitanzania
(shilingi) kwenda dola za kimarekani (USD), lakini cha ajabu ni kwamba
wakati mwingine ada inapopungua bodi huwa inafidia kiasi kilichopungua.
Je, ina maana fedha zetu za kujikimu tu ndizo zinazostahili kuathiriwa
na rate of exchange na kutokufidiwa kiasi kinachopelea kila mwaka?
Mfano mzuri ni
mwaka huu wa 2010/2011. Bodi imetuma kwa kila mwanafunzi fedha pungufu
za kujikimu kwa wastani wa dola za kimarekani 477 na bado wakatueleza
eti ni kwa sababu ya rate of exchange. Tumewaomba sana watutumie fedha
hizo kwani sisi tunaathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na makato hayo,
lakini mpaka leo hatujapatiwa jibu lolote wala hatuoni dalili zozote za
suala letu hilo kushughulikiwa na Bodi ya mikopo wala Wizara ya elimu.
3:KUTOKUTUMIWA
FEDHA ZA BIMA YA AFYA .
Mhe. Waziri Mkuu, mwaka huu wa 2010/2011, serikali haikutupatia
kabisa fedha za kulipia bima ya afya. Kwa masharti ya chuoni na Nchini
urusi, mwanafunzi kama HUJALIPIA BIMA YA AFYA HUWEZI KUPATIWA HUDUMA
YOYOTE ILE YA AFYA, HUWEZI KURUHUSIWA KUFANYA USAJILI WALA KUPATWA
VIZA(kila mwaka huwa tunahitajika kuomba viza mpya na kufanya usajili
ili tuweze kuruhusiwa kuendelea na masomo kwa mwaka unaofuata). Licha ya
kuikumbusha wizara na bodi juu ya kutupatia fedha hizo, lakini mpaka
leo mwaka unaelekea kuisha hatujapatiwa fedha hizo wala hakuna jibu la
aina yoyote ile.
4:MWAMBATA WA
ELIMU.
Mhe. Waziri
Mkuu, ni miaka mingi sasa imepita tangu tuanze kuiomba wizara kutuletea
mwambata wa elimu nchini urusi. Matatizo yetu mengi yanachelewa sana
kupatiwa ufumbuzi na wakati mwingine yanashindikana kabisa kupatiwa
ufumbuzi kwa sababu hatuna mwambata wa elimu nchini urusi. Mara kwa mara
tumelazimika kupeleka matatizo yetu kwa maofisa wa ubalozi ambao nao
pia wana majukumu yao mengine tofauti tofauti, tunashukuru wamekuwa
wakijitahidi kutusaidia. Lakini kukosekana kwa Mwambata wa elimu bado ni
tatizo kubwa sana linalotuathiri wanafunzi nchini urusi.
5: OMBI LA NYONGEZA
KATIKA FEDHA ZA KUJIKIMU.
Mhe. Waziri Mkuu, mara kwa mara tumekuwa tukiilalamikia na
kuiomba Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi stadi kutupatia nyongeza ya
fedha za kujikimu pasipo mafanikio yoyote. Mji tunaoishi (MOSCOW) ni
mojawapo ya miji ghali sana duniani, maisha yetu huku yameendelea kuwa
duni sana na wakati mwingine tunashindwa hata kupata baadhi ya huduma
muhimu. Mara kwa mara tumeijulisha wizara ya elimu, na hata tumeweza
kuipatia michanganuo inayoonesha jinsi fedha wanazotupatia kwa sasa
zinaishia katika kulipia mambo mbalimbali ya lazima na wakati mwingine
tunabakiwa na kiasi kidogo sana cha pesa ambacho ndicho tunalazimika
kukitumia kwaajili ya chakula(japokuwa wengi wetu tunakula aidha mlo
moja au miwili tu kwa siku). Kwa kweli tunaiomba serikali kutufikiria
katika jambo hili kwani hali tuliyonayo kwa sasa ni mbaya sana, pia
ikizingatiwa kuwa nchini Urusi KILA MWAKA MWEZI WA 9 BEI ZA BIDHAA NA
GHARAMA ZA HUDUMA MBALIMBALI HUPANDISHWA na hivyo kuzidi kutuathiri
zaidi sisi wanafunzi wa kigeni.
Mhe. Waziri Mkuu,
tunatumaini kuwa malalamiko, vilio na maombi yetu, utayapokea na
kuyafanyia kazi mapema. Tunakutakia afya tele na mafanikio mema katika
shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa letu.
Asante sana.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)