ZIARA YA BIRMINGHAM CITY HATARINI KUOTA MBAWA. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

ZIARA YA BIRMINGHAM CITY HATARINI KUOTA MBAWA.

         
Ziara ya Birmingham City kuzuru Tanzania mwezi Julai kwa michezo kadhaa ya kirafiki iko katika hatihati, na endapo kama wenyeji wao Simba SC watashindwa kuthibitisha ratiba na malipo stahili kwa ziara hiyo ifikapo saa sita kamili mchana wa leo huenda ikaahirishwa, Globu ya Jamii inaweza kuthibitisha.

 Habari za uhakika zilizotufikia kutoka London zinasema Birmingham City imemuandikia Mwenyekiti wa Simba SC, Mh. Alhaj Ismail Aden Rageh kwamba wamepatwa na wasiwasi baada ya Wekundu wa Msimbazi hao kuchelewa kutoa uhakika wa ratiba ya ziara kwa muda ulioafikiwa awali na pande hizo mbili.
 Kwa mujibu wa barua hiyo toka kwa  Julia Shelton, Mkuu  wa Utawala wa Mpira wa Klabu hicho cha Premier League ya Uingereza, ambayo Globu ya Jamii inayo nakala yake, Birmingham imetishia kufuta kabisa ziara hiyo endapo kama mkataba wa ziara hiyo haujasainiwa na kufikishwa kwao ifikapo saa sita kamili za mchana leo  - yaani masaa matatu kuanzia sasa.
 Katika barua hiyo Julia Shelton ametahadharisha pia kwamba tayari Birmingham wameishaingia gharama kibao za maandalizi ikiwa ni pamoja na kukodi ndege maalum kwa ajili ya ziara hiyo, chanjo kwa wachezaji iliyopangwa kufanyika Mei 23  pamoja na gharama zingine muhimu ambazo, amesisitiza huenda ‘zikaongelewa’ huko mbeleni.
 Julia Shelton pia ameongelea athari za yatayojiri kwenye vyombo vya habari vya kimataifa zitapozungumzia kadhia hii kwa ubaya endapo kama mkataba huo haujasainiwa na ziara kutofanyika baada ya maandalizi makubwa.
 Glolu ya Jamii imewasiliana na Mh. Rage asubuhi hii naye amethibitisha kwamba ziara hiyo ina hati hati kwani Simba hawatoweza kusaini mkataba huo kabla ya mechi yao na Wydad Casablanca iliyopangwa kuchezwa Cairo Mei 28, 2011 kwa kuhofia kwamba endapo watashinda hawatoweza kucheza na Birmingham kwani watakuwa na kibarua kingine cha Ligi ya Mabingwa Afrika.
 Mechi  hiyo ya kutafuta timu itakayocheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Wydad Casablanca ya Morocco itachezwa Mei 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Petrosport jijini Cairo, Misri.
 Simba, ambayo ilishatolewa kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa mabao 6-3 na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imerudishwa tena kufuatia ushindi wa rufaa yake dhidi ya Mazembe baada ya mabingwa hao mara mbili wa Afrika kumtumia mchezaji Janvier Besala Bokungu bila kukamilisha taratibu za usajili.
 Baada ya kushinda rufaa hiyo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likapanga mechi ya Simba na Casablanca ambayo nayo ilishatolewa kwenye kinyang’anyiro hicho na Mazembe ichezwe mkondo mmoja uwanja huru, katika mechi  ambayo  ikiisha bila kufungana ndani ya dakika 90, mshindi atapatikana kwa mikwaju ya penati.
 “Kwa kweli nimesikitishwa sana kwa haya kujitokeza kwani tayari makampuni kibao yalishakubali kuwa wadhamini na wengine kama vile bodi ya Taifa ya Utalii (TTB) walikuwa tayari kwenye Birmingham kutangaza vivutio vya utalii kwa mashabiki ambao wangeambatana na timu hiyo”, Mh. Rage ameiambia Globu ya Jamii.
 Akaendelea:  “Wenzetu huwa wanataka kupata uhakika kwa ziara kama hiyo siku 60 kabla nasi kwa kusema kweli kusaini mkataba leo kabla ya saa sita inakuwa ngumu kwani kama tukipita katika mchezo na Wydad kule Cairo hiyo Mei 28 hatutoweza kuwakaribisha Birmingham City.
 “Kinachonisikitisha zaidi sio sana mchezo wenyewe bali fursa kubwa ya kutangaza utalii wetu ambapo mashabiki 1000 walikuwa waje na timu, na tena waliomba wafikie hoteli za Kariakoo na sio katikati ya jiji ili wawe karibu zaidi na wenyeji.
 “Awali mashabiki kama 5000 hivi walikuwa wanajiandaa kuja lakini tukasita kuwakubalia kwani idadi hiyo ni kubwa mno kwa sisi kuweza kuwa-accomodate katika jiji la Dar ingawa ingekuwa jambo safi sana kiutalii…
“Kesho nitakutana na waandishi wa habari na kutoa msimamo endapo kama ziara ya Birmingham itafanyika au la kwani hapa nilipo bado hatujatoa uamuzi kamili kwamba tusaini mkatana huo ama vipi maana muda bado.

Source: Michuzi Blog

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages